KWA MAWASILIANO ZAIDI: E-mail: yusuf.badi2@gmail.com.

NSSF

TANGAZO

Wednesday, April 24, 2013

WAZAZI WATAKIWA KUTOA ELIMU YA UZAZI KWA WATOTO WAO.

Na Anna Nkinda – Maelezo
Wazazi nchini wametakiwa kutoa  elimu ya uzazi na ujinsia kwa watoto wao ili waweze kukabiliana na changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo  kipindi cha kubalehe.
Wito huo umetolewa leo na mke wa Rais Mama  Salma Kikwete wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa siku mbili wa Chama cha uzazi na malezi bora Tanzania (UMATI) unaofanyika katika hoteli ya Blue Pearl jijini Dar es Salaam .
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa miaka ya nyuma jamii ilikuwa inampa mtoto mafunzo maalum mara baada ya kubalehe mafunzo hayo yaliweza kumsaidia mtoto kuepukana na mazingira hatarishi ikiwa ni pamoja na yale yanayopelekea  upatikanaji wa ujauzito.
“Mtoto anaweza kupata ujauzito kutokana kwa kutofahamu elimu ya uzazi na kutambua mabadiliko ya mwili wake, ikitokea kwa bahati mbaya amepata ujauzito wazazi washirikiane kwa pamoja kuhakikisha kuwa mtoto anarudi shule na kupata elimu, jukumu hili wasiachiwe kina mama peke yao”, alisema Mama Kikwete.
Kuhusiana na vifo vinavyotokana na uzazi hapa nchini Mama Kikwete alisema kuwa ni vifo 454 katika vizazi hai laki moja lakini idadi ya vifo hivyo inaweza kupungua iwapo huduma na elimu kuhusu afya ya uzazi na uzazi wa mpango itawafikia wanawake wengi zaidi.
Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema, “Ninawashukuru UMATI kwa kazi nzuri mnayoifanya  ya kutoa elimu na huduma bora za afya ya uzazi na ujinsia aidha nawasihi muongeze bidii na kasi ya kuzifikisha huduma hizi karibu zaidi na wananchi wanaozihitaji hususan maeneo ya vijijini ambako watanzania wengi wanaishi”.
Akiongea kuhusu jitihada zinazofanywa na UMATI za kumuwezesha mtoto wa kike Josephine Mwankusye ambaye ni Mkurugenzi mtendaji alisema kuwa wameweza  kuwapatia elimu ya afya ya uzazi na ujinsia kupitia vituo vya vijana na kliniki zao   na katika kipindi cha mwaka 2012 waliwafikia  watoto wa kike zaidi ya laki mbili na nusu.
Aliendelea kusema kuwa wanatengeneza mazingira mazuri kwa mtoto wa kike ili aweze  kujimudu katika maisha na kutokuwa tegemezi, elimu ya ujasiliamali hutolewa kwa vijana na baadaye hupewa  mitaji midogo midogo na kutoa mfano wa kituo chaTemeke ambako watoto wa kike walioacha shule baada ya kupata ujauzito wameweza kusaidiwa kutekeleza shughuli za kuwapatia kipato kama vile uokaji wa mikate, utengenezaji wa batiki, ushonaji na kozi ya usimamizi wa hoteli.
Mwankusye alisema, “Kupitia mradi wa vijana wa kike walio katika sekta zisizo rasmi  kwa kipindi cha mwaka 2008 - 2012 vikundi 14 vilipatiwa elimu ya ujasiliamali  na kupewa mtaji wa   shilingi laki saba  kwa kila kikundi katika mkoa wa Kilimanjaro”.
Alimalizia kwa kusema kuwa wanatetea haki za mtoto wakike katika mlengo wa elimu, afya na kutokomeza vitendo vya ukatiki. Pi wamekuwa mstari wa mbele katika kutetea ubadilishwaji wa sera ya elimu ili mtoto wa kike anayepata ujauzito akiwa shuleni aruhusiwe kuendelea na masomo mara tu anapojifungua..
UMATI ilianzishwa mwaka 1959 na kujikita katika kutoa elimu na huduma mbalimbali za afya ya uzazi. Kauli mbiu ya mkutano huo ni  “Elimu na Afya ya Uzazi ni Haki ya mtoto wa kike, Timiza wajibu wako”.

No comments: