Wakati
timu ya Ivory Coast imewasili nchini jana usiku (Juni 13 mwaka huu) kwa
ndege maalum, kocha wa timu hiyo Sabri Lamouchi na mwenzake wa Taifa
Stars, Kim Poulsen watakutana na waandishi wa habari kuzungumzia mechi
yao.
Mkutano
huo utafanyika kesho (Juni 15 mwaka huu) saa 4 kamili asubuhi kwenye
ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Mkutano huo pia
utajumuisha makocha wa timu zote mbili. Ivory Coast inafanya mazoezi
yake ya kwanza leo (Juni 14 mwaka huu) saa 9 alasiri kwenye viwanja vya
Gymkhana.
Timu
zote kesho (Juni 15 mwaka huu) zitafanya mazoezi ya mwisho kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Ivory Coast watafanya mazoezi saa 9
kabla ya kuwapisha Stars saa 10 kamili. Maandalizi yanaendelea vizuri
ikiwemo kuwasili kwa maofisa wote wa mechi itakayochezwa Jumapili saa 9
kamili alasiri.
Wakati
huo huo, mauzo ya tiketi kwa ajili ya mechi hiyo yameanza leo mchana
(Juni 14 mwaka huu) katika vituo vya Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa,
Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom
Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, City Sports Lounge iliyoko Mtaa wa
Samora na Azikiwe, Dar Live Mbagala, BMM Salon iliyoko Sinza Madukani na
Uwanja wa Taifa.
Mauzo
yataendelea kesho katika vituo hivyo, wakati siku ya mchezo yatafanyika
Uwanja wa Taifa. Viingilio katika mechi hiyo ya mchujo ya Kombe la
Dunia, Kanda ya Afrika katika kundi C ni sh. 5,000, sh. 7,000, sh.
10,000, sh. 15,000 VIP C, sh. 20,000 VIP B na VIP A sh. 30,000. Pia kuna
kadi maalumu 100 kwa viti vya Wageni Maalumu (VVIP) zinazopatikana kwa
sh. 50,000 katika ofisi za TFF.
TFF YATOA NOTISI YA MKUTANO MKUU
Rais
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga ametoa
notisi kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalumu wa Shirikisho utakaofanyika
Julai 13 mwaka huu kwenye ukumbi wa NSSF Waterfront jijini Dar es Salaam
ukiwa na ajenda moja ya marekebisho ya Katiba.
Notisi
hiyo imetolewa juzi (Juni 12 mwaka huu). Rais ameitisha Mkutano huo kwa
mujibu wa Ibara ya 25(1) ya Katiba ya TFF baada ya kupata maagizo
kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kwa barua yake
ya Aprili 29 mwaka huu.
Ajenda
rasmi na taarifa nyingine zitatumwa kwa wajumbe siku 15 kabla ya
Mkutano huo kwa mujibu wa Ibara ya 25(4) ya Katiba ya TFF. Wanachama wa
TFF ambao ni vyama vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu
wanatakiwa kutuma majina ya wajumbe halali.
TFF
inapenda kuwakumbusha wanachama wake kutuma majina ya wajumbe halali
ili kufanikisha maandalizi ya Mkutano huo. Ni vizuri kuhakikisha kuwa
jina linalotumwa ni la mjumbe halali wa Mkutano Mkuu kwa mujibu wa
Katiba ya TFF.
No comments:
Post a Comment