KWA MAWASILIANO ZAIDI: E-mail: yusuf.badi2@gmail.com.

NSSF

TANGAZO

Friday, July 19, 2013

MAELEZO YA SHUKURANI YA MWENYEKITI ALIYEMALIZA MUDA WAKE WA KAMATI YA UCHAGUZI YA TFF - KWA VIONGOZI NA WADAU WA SOKA NCHINI.

1.                   Kama wote tunavyofahamu jana uongozi wangu wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ulifikia tamati kama mlivyotangaziwa na Rais wa TFF. Kwa heshima kubwa naomba kutumia fursa hii kuwashukuru viongozi na wadau wa soka kwa ushirikiano mkubwa nilioupata kutoka kwao wakati nikitekeleza majukumu mbalimbali ya TFF.

2.                   Kwa kushirikiana na viongozi wa mpira wa miguu katika TFF na mikoa yote Tanzania Bara, pamoja na wadau wa soka, nimepata fursa kulitumikia soka la nchi yetu kwa nafasi mbalimbali. Kwa pamoja tumetekeleza majukumu ya ujenzi wa misingi ya uongozi bora katika TFF na wanachama wake.

3.                   Naishukuru Kamati ya Utendaji ya TFF:

(i)             kwa kuniteua kuwa mjumbe wa Kamati ya Nidhamu ya TFF, (Jan 2005 - Jan 2007). Nawashukuru pia wajumbe wa Kamati hiyo chini ya Mhe. Said El-Maamry kwa kunichagua kuwa Katibu wa Kamati hiyo. Ushirikiano mlionipatia ulioniwezesha kulitumikia taifa katika soka na kwa pamoja kurejesha nidhamu kwa kiwango kikubwa.

(ii)           kwa kuniteua kuwa mjumbe wa Kamati Maalumu, iliyochunguza mkasa wa timu yetu ya Taifa ya wachezaji wa umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) mwezi Juni 2005. Nawashukuru wajumbe wa kamati  hiyo chini ya Dr. Hamad Ndee Mkuu wa Idara ya Michezo ya Chuo kikuu cha Dar es salaam, kwa kunichagua kuwa Katibu wa kamati hiyo iliyoandaa taratibu za mashindano ya vijana  ambazo ni msingi  wa mashindano ya vijana wa umri chini ya miaka 17  hapa nchini.

(iii)          kwa kuniteua kuwa Mjumbe wa Kamati Maalumu iliyotayarisha Programu ya kuendeleza Timu ya Taifa kwa kipindi cha miezi 15 (April 2006 hadi Juni 2007). Progamu iliyochangia Tanzania kiinua kiwango cha ubora wa soka kutoka nafasi ya 165 duniani mwezi Februari 2006 hadi nafasi ya 89 mwezi Desemba 2007.

(iv)         kwa kunipa fursa ya kuwa mjumbe wa Kamati Maalumu ya kuboresha mapato ya TFF mwaka 2009. Nikiwa mjumbe na Katibu wa Kamati hiyo nilipata ushurikiano mkubwa kutoka kwa wadau wa soka nchini  na nje ya nchi.  Nina imani kuwa TFF itakamilisha utekelezaji wa mapendekezo ya Kamati na ya wadau wa soka ikiwa ni pamoja na kuanza kutumia tiketi za elektroniki.

(v)           kwa kuniteua kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF  kwa  vipindi viwili; Februari 2009 - Machi 2011 na kuniteua tena kuiongoza Kamati hiyo kwa kipindi cha pili Machi 2011 hadi jana tarehe 18 Julai 2013. Naishukuru Kamati ya Utendaji ya TFF kwa imani kubwa iliyoonyesha kwangu na wanakamati wenzangu.
4.                   Nawashukuru wajumbe wote wa wa Mkutano Mkuu wa TFF, kwa ushirikiano mkubwa mliotoa kwangu na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kushiriki kwa amani na utulivu na kuzingatia Katiba za vyama vyenu, Katiba ya TFF na Kanuni za Uchaguzi na hivyo kufanikisha zoezi la chaguzi za viongozi katika wilaya zote na Mikoa yote ya Tanzania Bara na hivyo kuwezesha kuwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu, ambao  katika kikao chake cha kwanza baada ya chaguzi hizo kimefanya jambo la kihistoria kuweka nguzo za  Mwenendo, Maadili  na Miiko ya uongozi wa soka la nchi yetu. Nilifarijika kuwa sehemu ya Mkutano Mkuu huo nikiwa mwalikwa.

5.                   Nawashukuru viongozi na wafanyakazi wote wa Sekretarieti ya TFF, wajumbe wa Kamati zote za TFF, Wajumbe wa Kamati zote za Uchaguzi za wanachama wa TFF na wanachama wao, kwa ushirikiano mkubwa na wa dhati uliowezesha kuwatumikia wadau wa soka kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.

6.                   Nawashukuru sana wajumbe wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa ushirikiano niliopata kutoka kwao kwa muda tuliofanya kazi pamoja. Si jambo rahisi kusimamia chaguzi za mikoa yote na klabu zenye wanachama za Ligi Kuu, hata hivyo kwa kushirikiana na wadau mbalimali wa soka ambao nachukua fursa hii kuwashukuru, kwa pamoja tumeweza kutimiza jukumu hilo kikamilifu.  

7.                   Nawashukuru sana Wandishi na Wahariri wa habari za michezo na pia Wahariri Watendaji wa vyombo vya habari, kwa ushirikiano mzuri nanyi, ushirikiano na uhusiano wa uwazi ambao haukuwa na mikwaruzo ya aina yoyote kwa kipindi chote (Jan 2005-Jul 2013) tulichoshirikiana kwa pamoja kulitumikia soka la nchi yetu.

8.                   Namshukuru sana Rais wa TFF Ndg. Leodegar Tenga kwa imani kubwa aliyonayo kwangu na kwa wanakamati niliokuwa nao katika kutekeleza majukumu ya umma. Miaka ishirini na tisa (29) iliyopita nilipata fursa ya kufanya kazi ya mpira miguu kwa mara ya kwanza na Ndg. Tenga, nikiwa nahodha wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Chuo kikuu cha Dar es salaam, Desemba 1984, wakati Ndg. Tenga alipojitolea kuifundisha timu ya Chuo Kikuu cha DSM. Tangu wakati huo hadi sasa imani  na  ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu ya umma niliopata kutoka kwa Ndg. Tenga haujawai kutetereka hata kwa siku moja. Ni faraja kubwa kwangu kufanya kazi hizi za umma chini ya kiongozi anayeheshimika na kuaminika na wadau wa soka hapa nchini, Afrika Mashariki na Kati, Afrika na familia ya soka Duniani kwa ujumla.

9.                   Mwisho, kwa viongozi na wadau wote wa mpira wa miguu, nawashukuru na nawatakia kheri, baraka  na mafanikio katika Uchaguzi Mkuu wa TFF na  ujenzi wa  soka la nchi yetu..

No comments: