SAMSUNG E-WARRANTY YAMWAGA ZAWADI KWA WATEJA.
Meneja
Mauzo na Usambazaji wa Samsung, Silyvester Manyara (kushoto), Mkaguzi wa Bodi
ya Michezo ya Kubahatisha, Bakari Maggid (katikati) na Meneja Mkuu wa Samsung, Kishor
Kumar kwa pamoja wakionesha baadhi ya zawadi zinazoshindaniwa katika droo ya
mfumo wa "E-Warranty" ambazo zinazoshindaniwa na wateja wanaonunua
bidhaa za Samsung. Hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam. (Picha na
Francis Dande)
Meneja Mauzo na Usambazaji wa Samsung, Silyvester Manyara akizungumza na mmoja washindi wa droo ya mfumo wa "E-Warranty" iliyofanyika leo jijini Dar es Salaam.
DAR ES SALAAM, Tanzania
KAMPUNI
ya vifa vya ki-elekroniki ya Samsung Tanzania, jana imewatangaza
washindi saba kati ya 10 wa programu yake ya ‘E-Warranty,’ ambapo Zelina
Baragamu wa Dar es Salaam aliibuka mshindi wa televisheni ya kisasa
(LED Tv) ya inchi 32.
Hafla
ya kuwapata na kuwatangaza washindi wa Julai wa program hiyo
inayomuwezesha mnunuzi wa bidhaa za Samsung kujua halisi na bandia
‘feki,’ ilifanyikajijini Dar es Salaam, huku washindi wa mikoa ya Kilimanjaro na
Arusha wakishindwa kupatikanana.
Katika droo hiyo, iliyowezesha kuwapata washindi kutoka
mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mbeya na Mwanza, Nolbert Julius na Rolliec
Chuwa wote wa Dar es Salaam walijishindia simu za mkononi aina ya Samsung
Galaxy.
Droo hiyo iliyochezeshwa chini ya usimamizi wa Bodi ya
Michezo ya Kubahatisha Tanzania, washindi wengine walikuwa ni Michael Mwaigande
wa Dodoma, aliyetwaa kompyuta mpakato ‘lap top’ ya Samsung, wakati Idda Johnson
wa Mwanza akijinyakulia Samsung Camera.
Washindi wengine wa ‘E-Warranty’ katika droo hiyo walikuwa
ni Joshua Jackson wa Mbeya aliyeshinda Home Theater, zawadi ambayo pia
alijinyakulia Lesehe Mehejigin wa Mwanza.
Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja Mkuu wa Samsung
Tanzania, Kishor Kumar, aliwataka Watanzania kujisajili kupitia programu ya
‘E-Warranty,’ iliyoonesha mafanikio makubwa katika kuwabana wazalishaji wa
bidhaa feki ndani na nje ya nchi.
“Huu ni mfumo sahihi kwa wateja wa bidhaa za simu za Samsung,
utakaomuwezesha mteja kujua kama simu anayotaka kununua ni halisi au feki, au
kujua kama ina dhamana ya miezi 24, mpya au ya zamani au kama imeibiwa na
inatafutwa,” alisema Kumar.
SHINDANO JIPYA LA TANZANIA TOP MODEL LAZINDULIWA JIJINI DAR ES SALAAM


SERIKALI YAGAWA PIKIPIKI KWA MAAFISA TARAFA
Mkuu
wa mkoa wa Shinyanga Mhe.Ally N.Rufunga akizungumza na Maafisa Tarafa
wa Mkoa wa Shinyanga kabla hajawakabidhi pikipiki zao jana ofisini kwake
( ofisi ya Mkuu wa Mkoa)
Baadhi ya Maafisa Tarafa wa Mkoa wa Shinyanga wakimsikiliza Mhe.Mkuu wa Mkoa kabla hawajakabidhiwa pikipiki.
Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Dkt.Anselm Tarimo akitoa maelekezo ya utendaji kazi kwa Maafisa Tarafa Mkoani Shinyanga.
Baadhi
ya pikipiki walizokabidhiwa Maafisa tarafa Mkoani Shinyanga ili
ziwasaidie katika katika utendaji wa kazi zao za serikali.
SHINYANGA, Tanzania
SSerikali mkoani Shinyanga imewataka Maafisa Tarafa kufanya
kazi kwa kufuata misingi ya maadili ya utumishi wa umma ili kuiboresha kada
hiyo inayoonekana kusahaulika siku hadi siku.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,Mhe. Ally N. Rufunga amewaasa
Maafisa Tarafa ofisini kwake jana,kabla ya
kuwakabidhi pikipiki 14 aina ya YAMAHA kwa ajili ya tarafa zote za mkoa
wa Shinyanga, ili kuwasaidia kuboresha utendaji wao wa kazi za serikali.
Mhe. Rufunga amewaeleza kuwa,serikali ya mkoa wa Shinyanga
imeamua kubadili mfumo, na kuanzia sasa itawatumia Maafisa Tarafa kikamilifu
kwani wao wanawajibika kwa Serikali kuu na Mamlaka za serikali za mitaa katika
shughuli zote kuanzia kusimamia ulinzi na usalama hadi usimamizi wa miradi ya
maendeleo katika maeneo yao.
Amewakumbusha pia kuhusu utaratibu wa kuratibu utendaji
kazi za serikali katika shughuli mbalimbali katika tarafa zao, na jukumu la
kutunza pikipiki hizo.
Nae Katibu Tawala Mkoa Dkt. Anselm Tarimo amewakumbusha
Maafisa Tarafa hao wajibu na maadili ya kazi yao na kuwaeleza kuwa wanatarajiwa
sana na serikali katika kupata taarifa sahihi za utekelezaji wa shughuli
mbalimbali kwenye tarafa, ili serikali iongeze nguvu pale ambapo wenyewe
watakwama.
Awali, Maafisa tarafa walieleza changamoto zinazowakabili
ni pamoja na kutoshirikishwa katika shughuli za utekelezaji wa miradi ya
maendeleo, hata kutoitwa kwenye vikao vya kisheria na hivyo inakuwa vigumu kwao
kuwajibika kwenye shughuli hizo, ambapo uongozi wa Mkoa umeahidi kuzifanyia
kazi changamoto hizo kwa kukutana na Wakurugenzi wa Halmashauri zote, ili
sheria na kanuni zilizowekwa zifuatwe.
Na Magdalena Nkulu
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa,
Shinyanga. RAIS JAKAYA KIKWETE NA MAKAMU WAKE DKT. BILAL WAWAONGOZA WAOMBOLEZAJI KUAGA MWILI YA KAKA WA WAZIRI MSTAAFU MAOKOLA MAJOGO
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akitoa heshima za mwisho mbele ya Jeneza
lenye mwili wa marehemu, Meinrad Diones Maokola, ambaye ni Kaka wa
Waziri Mstaafu, Maokola Majogo, aliyefariki jana jijini Dar es Salaam. Shughuli ya kuagwa mwili wa marehemu ilifanyika Masaki jijini Dar es Salaam. Picha na OMR
Rais
Jakaya Kikwete, Makamu wake Dkt. Mohammed Gharib Bilal na mke wa Rais
Mama salma Kikwete, wakitoa heshima za mwisho mbele ya Jeneza lenye mwili wa marehemu, Meinrad Diones Maokola, ambaye ni Kaka wa Waziri Mstaafu, Maokola Majogo.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akiwafariji wafiwa wakati alipofika kuaga mwili wa marehemu, Meinrad
Diones Maokola.
Rais
Jakaya Kikwete, Makamu wake Dkt. Mohammed Gharib Bilal, mke wa Rais
Mama salma Kikwete na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, wakijumuika na
waombolezaji wakati wa shughuli ya kuaga mwili wa marehemu, Meinrad
Diones Maokola.
Rais
Jakaya Kikwete, akiwafariji wafiwa wakati alipofika kuaga mwili wa
marehemu, Meinrad Diones Maokola, ambaye ni Kaka wa Waziri Mstaafu,
Maokola Majogo.
MAONI YA MSEMAJI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
MAONI
YA MSEMAJI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, WIZARA YA SHERIA NA
KATIBA, MHESHIMIWA TUNDU A.M. LISSU KUHUSU MUSWADA WA SHERIA YA
MAREKEBISHO YA SHERIA YA MABADILIKO YA KATIBA, YA MWAKA 2013 (Kanuni ya
86(6) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2013)
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Huu
ni Muswada wa marekebisho ya pili ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,
Sura ya 83 ya Sheria za Tanzania. Kama Bunge lako tukufu
litakavyokumbuka, Sheria hii ilifanyiwa marekebisho ya kwanza kwa
kupitishwa kwa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba,
Na. 2 ya mwaka 2012, mwezi Februari ya mwaka jana. Mabadiliko hayo ya
kwanza yalihusu Sehemu ya Tatu na ya Nne ya Sheria hii, na yalilenga
vifungu mbali mbali vinavyohusu Tume ya Mabadiliko ya Katiba na
utekelezaji wa majukumu yake.
Muswada
huu wa sasa unalenga kufanya marekebisho katika Sehemu ya Tano ya
Sheria inayohusu ‘Kuitisha Bunge Maalum.’ Sambamba na mapendekezo haya,
kuna mapendekezo ya kufanya marekebisho katika Sehemu ya Sita kwa kufuta
vifungu vya 32 hadi 36 vya Sheria vinavyohusu utaratibu wa kura ya
maoni kwa ajili ya kuhalalisha ‘Katiba Inayopendekezwa.’ Marekebisho
haya yamewekwa katika aya ya 57 ya Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni,
2013. Mapendekezo ya Muswada huu ni muhimu lakini yana utata mkubwa.
Mheshimiwa Spika,
Katika
kutekeleza majukumu yake ya kuuchambua Muswada huu, Kamati ya Bunge
lako tukufu ya Katiba, Sheria na Utawala ilikutana na wadau wengi mbali
mbali. Hivyo, kwa mfano, Kamati ilipata maoni ya taasisi za kidini na za
kiraia; taasisi za elimu ya juu na za kitaaluma; vyama vya siasa na
asasi nyingine. Kwa sababu ambazo Kamati haikuelezwa vizuri na uongozi
wa Bunge hili tukufu, mapendekezo ya Kamati kwenda Zanzibar kwa lengo la
kukusanya maoni ya wadau wa Zanzibar juu ya Muswada huu muhimu kwa
mustakbala wa Jamhuri ya Muungano yalikataliwa.
Kwa
maana hiyo, ni muhimu Bunge lako tukufu lifahamu ukweli huu kwamba
wadau pekee walioshirikishwa kutoa maoni yao juu ya Muswada ni
Watanzania Bara tu. Wazanzibari hawakupatiwa fursa hiyo na
hawakushirikishwa kabisa, licha ya Sheria yenyewe kuwa na mambo mengi
yanayoihusu Zanzibar. Kwa vile wadau wa Zanzibar walishirikishwa
kikamilifu kutoa maoni yao kuhusu Muswada uliopelekea Sheria hii
kutungwa mwaka 2011, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua ni
kwa nini uongozi wa Bunge na wa Serikali umeona si busara na sahihi
kuwapatia Wazanzibari fursa ya kutoa maoni yao kuhusu Muswada huu wa
kurekebisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo inawahusu pia
Wazanzibari na nchi yao.
URAIS WA KIFALME KWA MARA NYINGINE TENA!!!!
Mheshimiwa Spika,
Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni imepigia kelele jitihada za serikali hii ya
CCM kudhibiti mchakato wa Katiba Mpya kwa kuendeleza kile tulichokiita
miaka miwili iliyopita, “... kivuli kirefu cha Urais wa Kifalme katika
mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya.” Hapo tulikuwa tunazungumzia
mamlaka ya Rais ya uteuzi wa Wajumbe na watendaji wa Tume ya Mabadiliko
ya Katiba, na tulisema kwamba mamlaka hayo yalikuwa na lengo moja tu:
“kuhakikisha kwamba matokeo ya kazi ya Tume hiyo ni yale tu yanayotakiwa
na Rais na Serikali yake na chama chake cha CCM.”
Mheshimiwa Spika,
Katika
Maoni yetu wakati wa kutungwa kwa Sheria hii mwezi Novemba mwaka 2011,
Kambi Rasmi ya Upinzani ilipinga vikali mapendekezo ya kumwezesha Rais
kuteua Wajumbe wa Bunge Maalum wasiotokana na Bunge lako tukufu na
Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Tulisema yafuatayo kuhusiana na jambo
hili: “... wajumbe ... wanaopendekezwa kuteuliwa kwenye Bunge la Katiba
kwa mujibu wa ibara ya 20(2)(e) na (4) ya Muswada Mpya sio, na hawawezi
kuwa, wawakilishi wa wananchi. Kwanza, hawajachaguliwa na mtu yeyote na
wala taasisi zao kuwawakilisha katika Bunge la Katiba kwa sababu Muswada
Mpya unapendekeza wateuliwe na Rais.”
Kwa
sababu ya upinzani huo, mapendekezo ya kumfanya Rais kuwa mteuzi wa
wajumbe wa Bunge Maalum wasiokuwa wabunge na Wawakilishi yaliondolewa
katika Muswada huo wa Sheria hii. Badala yake, kifungu cha 22(1)(c) cha
Sheria iliyotungwa na Bunge lako tukufu kiliweka wazi kwamba “wajumbe
mia moja sitini na sita [watateuliwa] kutoka ...” taasisi zilizotajwa
katika kifungu hicho.
Mheshimiwa Spika,
Ni
kweli kwamba kifungu cha 22(1)(c) kama kilivyotungwa kilileta giza
badala ya mwanga katika suala la uteuzi wa wajumbe hao. Kama
tulivyoieleza timu ya wataalamu wa Serikali kufuatia mkutano wetu na
Rais Jakaya Kikwete uliofanyika Ikulu tarehe 26 Novemba, 2011: “Toleo la
Kiswahili la Sheria linasema kwamba wawakilishi wa makundi mengine
‘watakaoteuliwa kutoka’ kwenye makundi yaliyoorodheshwa. Toleo la
Kiingereza linasema wajumbe hao watakuwa ‘drawn from’ (kwa tafsiri ya
Kiswahili ‘watachukuliwa kutoka’). Maana za maneno haya hazifanani na
wala hayako wazi kuhusu nani ‘atakayewateua’ au ‘kuwachukua’ wajumbe hao
kutoka kwenye taasisi zao.”
Kwingineko
katika mkutano wetu na Rais Kikwete tulimweleza kwamba: “Wajumbe 166
wengine wanaowakilisha taasisi nje ya Wabunge na Wawakilishi
hawajachaguliwa na mtu yeyote na wala na taasisi zao kwani Sheria
haisemi ni nani atakayewateua na/au kuwachagua.” Kwa sababu hiyo,
tulipendekeza kwamba “Sheria iweke wazi kwamba wajumbe hawa ‘watateuliwa
na’ taasisi zilizotajwa. Hii itaondoa utata juu ya uwakilishi wao na
juu ya mamlaka yao ya uteuzi.”
Mheshimiwa Spika,
Mapendekezo
ya marekebisho yaliyoko kwenye Muswada huu yanaonyesha wazi kwamba
ushauri wetu kwa Rais Kikwete na kwa timu yake ya watalaamu umepuuzwa.
Badala yake, serikali hii sikivu ya CCM imeamua kuturudisha nyuma kwa
zaidi ya miaka miwili kwa kuibua tena pendekezo la kumfanya Rais kuwa
mteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalum wasiotokana na Wabunge au Wawakilishi
wa Zanzibar. Hii ni kwa sababu aya ya 3 ya Muswada inapendekeza kwamba
wajumbe hao sasa wateuliwe Rais. Hiyo ni sawa na kusema kwamba
kilichokuwa hakifai miaka miwili iliyopita sasa kinafaa; na
kilichokataliwa wakati ule sasa kinakubalika!
Ili
kuficha ukweli kwamba mwenye mamlaka ya uteuzi wa wajumbe wa Bunge
Maalum wasiokuwa Wabunge au Wawakilishi ni Rais, ambaye pia ni
Mwenyekiti wa CCM, Muswada unapendekeza kuongezwa kwa vifungu vidogo
vipya viwili katika kifungu cha 22. Kwanza, inapendekezwa kuwe na
kifungu kidogo cha (2A) ambacho kitamruhusu Rais kualika kila kundi
lilioainishwa katika kifungu kidogo cha 1(c) “kuwasilisha kwake orodha
ya majina ya watu wasiozidi watatu ili kuteuliwa kuwa wajumbe.” Pili,
inapendekezwa kuwe na kifungu kidogo cha (2B) kitakachomlazimu Rais
kuzingatia sifa na uzoefu wa watu waliopendekezwa, na usawa wa jinsia
wakati wa kufanya uteuzi wa wajumbe hao.
Mheshimiwa Spika,
Mapendekezo
ya kumpa Rais mamlaka ya kuteua wajumbe wa Bunge Maalum hayakubaliki na
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaliomba Bunge lako tukufu
lisiyapitishe kuwa Sheria. Kwanza, mapendekezo haya yanarudisha dhana
kwamba wajumbe hawa watakuwa watu wa Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa
CCM. Rais Kikwete na chama anachokiongoza ni wadau wakubwa wa mchakato
wa Katiba Mpya na wana maslahi halisi na makubwa ya kuhakikisha kwamba
matakwa ya chama chao ndio yanakuwa Katiba Mpya ya nchi yetu.
Ushahidi
wa maslahi haya ya CCM ni kile kinachoitwa Ufafanuzi Kuhusu Rasimu ya
Kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Wanachama na
Viongozi wa CCM uliotolewa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya
CCM tarehe 10 Juni, 2013. Katika Ufafanuzi huo, CCM imekataa mapendekezo
yote muhimu yaliyoko kwenye Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume.
Needless to say, Rais Kikwete ni Mwenyekiti wa vikao vyote vya Kamati
Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM. Kumpa Rais, na Mwenyekiti wa CCM
Taifa, mamlaka ya kuteua wajumbe wa Bunge Maalum litakaloijadili – na
kuikubali au kuikataa – Rasimu ya Katiba ambayo chama chake
kimekwishaikataa ni sawa na kuipa CCM fursa nyingine ya kujaza Bunge
hilo na makada wake kwa lengo la kutekeleza matakwa ya chama hicho.
Pili,
hata bila wajumbe hawa kuteuliwa kwa namna inayopendekezwa, tayari CCM
peke yake ina zaidi ya 72% ya wajumbe wote wa Bunge Maalum wanaotokana
na Wabunge na Wawakilishi. Kumpa Mwenyekiti wa CCM mamlaka ya kuteua
wajumbe wengine zaidi, kama inavyopendekezwa katika Muswada huu, ni
kutoa mwanya kwa CCM kutumia kivuli cha makundi ya kiraia, taasisi za
kidini na makundi mengine ili kujiongezea wajumbe wengine zaidi, na
hivyo kuhakikisha kwamba Bunge Maalum litatekekeleza matakwa ya
kuendeleza status quo.
Kwa
maneno mengine, Serikali hii ya CCM na Wabunge wake inataka Mwenyekiti
wao wa Taifa ayachagulie makanisa na awachagulie Wakristo wawakilishi
wao katika Bunge Maalum; awachagulie Waislamu wa BAKWATA, Baraza Kuu,
JUMAZA na taasisi nyingine za Kiislamu wawakilishi wao katika Bunge
hilo; avichagulie vyama vya siasa vinavyoipinga CCM wawakilishi wao;
awachagulie wafanyakazi, wakulima, wafugaji, wahadhiri, wanafunzi,
wafanyabiashara, walemavu na makundi mengine ya kijamii wawakilishi wao
katika Bunge Maalum! Kama ni hivyo, hilo halitakuwa Bunge Maalum la
Watanzania, bali litakuwa Bunge Maalum la CCM na Mwenyekiti wao. Hili
halikubaliki kwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na, tunaamini,
halitakubalika kwa wananchi wa Tanzania katika ujumla wao.
Tatu,
kwa jinsi yalivyo kwa sasa, mapendekezo haya hayawezi kutekeleza
matakwa ya kifungu cha 22(1)(c) cha Sheria kinachotaka wajumbe wa Bunge
Maalum wasiotokana na wabunge au wawakilishi kuwa mia moja sitini na
sita. Hii ni kwa sababu, hata kama watu wote waliopendekezwa na makundi
yaliyoainishwa na kifungu hicho watateuliwa kuwa wajumbe, bado idadi yao
itakuwa wajumbe ishirini na saba kwa kuwa makundi yenyewe yako tisa tu!
Muswada uko kimya juu ya wajumbe wengine mia moja thelathini na tisa
watatoka wapi na watateuliwa na nani na kwa utaratibu upi.
Kuna
hoja kwamba utaratibu wa uteuzi wa wajumbe unaopendekezwa na Muswada
unafanana na uteuzi wa wajumbe wa Tume ulioko kwenye kifungu cha 6(6)
cha Sheria ambapo Rais alialika vyama vya siasa, jumuiya za kidini,
asasi za kiraia, n.k., kuwasilisha orodha ya majina ya watu ili
kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume. Hoja hii sio sahihi. Kwanza, Tume ya
Katiba sio sawa na Bunge Maalum. Tume ni chombo cha kitaalamu chenye
majukumu ya kitaalamu ya kukusanya maoni ya wananchi, kuandaa ripoti
pamoja na Rasimu ya Katiba. Uhalali wa Tume unatokana na utaalamu wa
wajumbe wake na weledi katika kutekeleza majukumu yao ya kitaalamu.
Kwa
upande mwingine, Bunge Maalum ni chombo cha uwakilishi ambacho wajumbe
wake wana majukumu ya kisiasa ya kuwakilisha wananchi wa makundi mbali
mbali kwenye kazi ya kisiasa ya kuandika Katiba Mpya. Uhalali wa Bunge
Maalum unatokana na upana na ubora wa uwakilishi wake wa makundi mbali
mbali ya kisiasa na kijamii. Chombo cha uwakilishi cha aina hii lazima
kitokane na wananchi na/au makundi ya kijamii kinachoyawakilisha ili
kiwe na uhalali wa kisiasa. Dhana ya Rais – na Mwenyekiti wa CCM –
kuteua Wajumbe wa Bunge Maalum inavuruga au kuondoa kabisa dhana ya
uwakilishi wa wananchi na uhalali wa kisiasa katika mchakato wa Katiba
Mpya.
Pili,
kumpa Rais mamlaka ya kuteua wajumbe wasiokuwa Wabunge au Wawakilishi
wa Zanzibar kunaleta dhana ya ubaguzi. Hii ni kwa sababu, Rais hana
mamlaka ya kuteua wajumbe wa Bunge Maalum watakaotoka kwenye Bunge la
Jamhuri ya Muungano na Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Hawa wataingia
katika Bunge Maalum kwa mujibu wa nafasi zao Bungeni au katika Baraza na
sio kwa fadhila ya Rais. Swali la kujiuliza hapa ni kwa nini Rais awe
na mamlaka ya kuteua wajumbe wasiokuwa Wabunge au Wawakilishi wakati
hana mamlaka hayo kuhusu Wabunge na Wawakilishi? Needless to say,
ubaguzi huu unaenda kinyume na matakwa ya ibara ya 13(2) ya Katiba ya
sasa na, kwa hiyo, haukubaliki.
Tatu,
uteuzi wa wajumbe wa Tume uliofanywa na Rais na ambao unatumiwa kama
mfano wenyewe ulikuwa na walakini kubwa. Katika hili, kuna ushahidi wa
wawakilishi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Baraza la
Kikristo Tanzania (CCT) na asasi mbali mbali za kiraia zikiwemo za
walemavu waliowasilisha maoni ya taasisi zao kwa Kamati juu ya Muswada
huu. Wawakilishi hao waliiambia Kamati kwamba ijapokuwa waliandikiwa na
Rais kuwasilisha majina ya wajumbe wao kwa ajili ya kuteuliwa kwenye
Tume, na walifanya hivyo, hakuna hata moja ya majina waliyopendekeza
aliyeteuliwa na Rais kuwa wajumbe wa Tume.
Badala
yake, Rais aliteua watu aliowaona yeye na washauri wake wanafaa. Kama
taarifa za wadau hawa ni za kweli maana yake ni kwamba Rais na
Mwenyekiti huyu wa CCM Taifa hawezi kuaminika tena kuteua wajumbe halisi
wa taasisi hizi katika Bunge Maalum ambalo ndilo litakalojadili na
kuipitisha – au kuikataa - Rasimu ya Katiba Mpya ambayo tayari CCM na
wapambe wao wametamka wazi kwamba wanaikataa!
WAJUMBE WA BUNGE MAALUM WAONGEZWE
Mheshimiwa Spika,
Ili
kutatua mkanganyiko huu, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza
Bunge lako tukufu lirejee na kukubali mapendekezo yetu kwa Timu ya
Wataalamu wa Serikali ya Januari mwaka jana:
“Sheria iweke wazi kwamba wajumbe hawa ‘watateuliwa na’ taasisi
zilizotajwa. Hii itaondoa utata juu ya uwakilishi wao na juu ya mamlaka
yao ya uteuzi;
“Sheria itaje kwamba idadi ya wajumbe wa Bunge Maalum watakaotokana na
kila taasisi iliyoorodheshwa katika kifungu cha 22(1)(c) itakuwa 354
kama walivyoorodheshwa hapa chini:
(a)
“Asasi zisizokuwa za kiserikali zilizotajwa katika aya (i) zifafanuliwe
kuwa ni makundi yanayounganisha asasi hizo, yaani, ANGOZA, TANGO,
TACOSODE na Jukwaa la Katiba na kila moja ya makundi hayo itakuwa na
wajumbe watano kwa jumla ya wajumbe 20;
(b)
“Asasi za kidini zilizotajwa katika aya (ii) zifafanuliwe kuwa ni
makundi yanayounganisha asasi hizo, yaani, BAKWATA, Baraza Kuu, JUMAZA,
TEC, CCT na PCT na kila moja ya makundi hayo itakuwa na wajumbe watano
kwa jumla ya wajumbe 30. Aidha, Waadventista wa Sabato (SDA), Hindu,
Shia Ithnaasheri na Sikh watakuwa na mjumbe mmoja mmoja, kwa jumla ya
wawakilishi 35 wa taasisi za kidini;
(c)
“Vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu vilivyotajwa katika aya (iii)
vitakuwa na wajumbe 72 watakaogawanywa katika makundi mawili: 1) vyama
vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu vitakuwa na wajumbe 42 ikiwa ni
wajumbe wawili kwa kila chama; 2) vyama vya siasa vyenye uwakilishi
Bungeni vitakuwa na wajumbe 30 ikiwa ni CCM 18, CHADEMA 7, CUF 3 na
NCCR-Mageuzi, TLP na UDP 3 kwa ujumla wao. Hii ni kufuatana na uwiano wa
kura zote za Wabunge ambazo vyama hivyo vilizipata kwenye Uchaguzi Mkuu
wa 2010;
(d)
“Taasisi za elimu ya juu zilizotajwa katika aya (iv) zifafanuliwe kuwa
ni vyuo vikuu 28 vinavyotambuliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU)
na vyuo vya elimu ya juu 16 vinavyotambuliwa na Baraza la Elimu ya
Ufundi la Taifa (NACTE). Taasisi hizi zitakuwa na mjumbe mmoja kwa kila
moja kwa jumla ya wajumbe 44;
(e)
“Taasisi za elimu ya juu zinahusisha pia vyama vya wanafunzi wa vyuo
vya elimu ya juu ambavyo vitakuwa na mjumbe mmoja mmoja kwa chama cha
wanafunzi kwa jumla ya wajumbe 44;
(f)
Taasisi za elimu ya juu zinahusisha pia vyama wahadhiri/wakufunzi wa
vyuo vya elimu ya juu ambavyo vitakuwa na mjumbe mmoja mmoja kwa kila
chama kwa jumla ya wajumbe 44;
(g)
“Makundi yenye mahitaji maalum yaliyotajwa katika aya (v) yafafanuliwe
kuwa ni mashirika yanayowakilisha wenye ulemavu wa macho, ngozi,
viziwi/bubu, viwete na walemavu wa aina nyingine ambayo yatakuwa na
wajumbe 10 kwa ujumla wao;
(h)
“Vyama vya wafanyakazi vilivyotajwa katika aya (vi) vifafanuliwe kuwa
ni vile vilivyosajiliwa na vitakuwa na wajumbe 40 ikiwa ni wajumbe
wawili kutoka kila chama cha wafanyakazi kilichosajiliwa;
(i)
“Jumuiya ya wakulima iliyotajwa katika aya (vii) itakuwa na wajumbe 10
watakaotokana na vyama vya wakulima wa mazao kama vile pamba, kahawa,
korosho, chai, katani, karafuu, miwa na wavuvi;
(j)
“Jumuiya ya wafugaji iliyotajwa katika aya (viii) itakuwa na wajumbe 10
watakaotoka Baraza la Mashirika yasiyo ya Kiserikali ya Wafugaji na
Wawindaji/wakusanya matunda ya porini (PINGOS Forum);
(k)
“Vikundi vingine vya watu wenye malengo yanayofanana vilivyotajwa
katika aya (ix) vifafanuliwe kumaanisha Chama cha Waajiri Tanzania
(ATE), Chama cha Wenye Viwanda Tanzania (CTI), Chama cha
Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Chama cha
Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC); Chama cha Wafanyabiashara ya
Madini na Nishati (TCME); vyama/mashirika ya wachimbaji madini wadogo
wadogo; Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOWAT), Chama cha
Waandishi Habari/Jukwaa la Wahariri Tanzania, Chama cha Mawakili
Tanganyika (TLS), Chama cha Mawakili Zanzibar (ZLS), Chama cha Madaktari
Tanzania (MAT), Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET) na Chama cha
Wakandarasi Tanzania (CATA). Makundi haya yatakuwa na wajumbe wawili kwa
kila moja kwa jumla ya wajumbe 26.”
Mheshimiwa Spika,
Kwa
mujibu wa kifungu cha 22(1) cha Sheria kama ilivyo sasa, Bunge Maalum
litakuwa na jumla ya wajumbe 604, yaani Wabunge 357, Wawakilishi 81 na
wajumbe 166 wanaowakilisha makundi mbali mbali. Mapendekezo haya ya
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni yatafanya uwakilishi katika Bunge Maalum
kupanuka hadi wajumbe 792 kwa Tanzania yenye idadi ya watu milioni 45
kwa takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012.
Hili,
kwa vyovyote vile, ni ongezeko kubwa la wajumbe wa Bunge Maalum. Hata
hivyo, ukubwa huu unaopendekezwa hauna tofauti kubwa sana na Mabunge
Maalum ya nchi nyingine ambazo zimekamilisha utungaji wa Katiba Mpya kwa
kutumia utaratibu huu. Kwa mfano, Bunge Maalum la Jamhuri ya Nepal la
mwaka 2011 lilikuwa na wajumbe 601 kwa nchi yenye idadi ya watu milioni
26; Bolivia (2009) lilikuwa na wajumbe 255 katika nchi yenye watu
milioni 9; Kenya (2005) lilikuwa na wajumbe 629 kwa idadi ya watu
milioni 31; Eritrea (1997) lilikuwa na wajumbe 527 kwa idadi ya watu
milioni 3.2, wakati Bunge Maalum la Ufaransa ya Mapinduzi ya 1789
lilikuwa na wajumbe 1145 katika nchi iliyokuwa na idadi ya watu milioni
28.
Kikubwa
na muhimu zaidi, kwa mapendekezo haya, ni kwamba Bunge Maalum la Katiba
litakuwa na sura ya Kitanzania zaidi badala ya utaratibu wa sasa
unaolifanya Bunge Maalum kuonekana la kiCCM zaidi. Kwa kuongezea tu,
Mheshimiwa Spika, wadau karibu wote waliotoa maoni yao kwenye Kamati
walipendekeza kuongezwa kwa idadi ya wajumbe wa Bunge Maalum. Kwa kigezo
chochote kile, kwa hiyo, mapendekezo haya ni ya kidemokrasia na
tunaliomba Bunge lako tukufu liyaunge mkono ili kuiwezesha nchi yetu
kujipatia Katiba Mpya yenye sura halisi ya kitaifa kuliko
inavyopendekezwa sasa.
UWAKILISHI WA ZANZIBAR KATIKA BUNGE MAALUM
Mheshimiwa Spika,
Tume
ya Mabadiliko ya Katiba imekwishatoa Rasimu ya Katiba kwa mujibu wa
kifungu cha 19(1)(d) cha Sheria. Rasimu hiyo imepndekeza mabadiliko
makubwa katika muundo wa Jamhuri ya Muungano kwa kupendekeza muundo wa
shirikisho lenye serikali tatu. Baada ya kukamilika kwa mchakato wa
kutoa maoni juu ya Rasimu hii kwa mujibu wa kifungu cha 18, Tume
itawasilisha ripoti kwa Rais na kwa Rais wa Zanzibar kwa mujibu wa
kifungu cha 20(1). Baada ya hapo, Rais, “... atachapisha Rasimu ya
Katiba katika Gazeti la Serikali na kwenye magazeti mengine pamoja na
maelezo kwamba Rasimu ya Katiba itawasilishwa kwenye Bunge Maalum kwa
ajili ya kupitishwa Katiba inayopendekezwa.”
Mheshimiwa Spika,
Ili
kutimiza matakwa haya ya Sheria na kwa kuzingatia mapendekezo ya Rasimu
ya Katiba iliyotolewa na Tume, Bunge lako tukufu linahitaji kuangalia
upya suala la uwakilishi wa Zanzibar katika Bunge Maalum. Kwa mujibu wa
kifungu cha 22(2) cha Sheria, idadi ya wajumbe wa Zanzibar katika Bunge
Maalum watakaotokana na makundi yaliyoainishwa katika kifungu cha
22(1)(c) “... haitapungua theluthi moja ya wajumbe hao.” Hii ina maana
kwamba, kwa uchache kabisa, wajumbe hao wa Zanzibar hawatapungua 55.
Rasimu
ya Katiba itakayojadiliwa na Bunge Maalum inahusu Katiba ya Jamhuri ya
Muungano peke yake. Rasimu hiyo imependekeza kwamba masuala yote yasiyo
ya Muungano ya Washirika wa Muungano, yaani Tanzania Bara na Zanzibar,
yashughulikiwe na Katiba za Washirika hao.
Kwa
sasa Wabunge wanaotoka Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya Muungano ni
83, wakati Baraza la Wawakilishi Zanzibar lina wajumbe 76. Kwa ujumla,
kwa hiyo, ili kutekeleza matakwa ya kifungu cha 22(1) na (2) cha Sheria,
Zanzibar itakuwa na wajumbe 219 katika Bunge Maalum lenye wajumbe 604,
sawa na takriban 36% ya wajumbe wote. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inataka kujua: kama ilikuwa busara na sahihi kwa nusu ya wajumbe wa Tume
ya Mabadiliko ya Katiba kutoka Zanzibar, kwa nini isiwe busara na
sahihi vile vile kwa nusu ya wajumbe wa Bunge Maalum litakaloijadili na
kuipitisha Katiba Mpya hiyo kutoka Zanzibar? Au ndio kusema kwamba hoja
za usawa kati ya nchi Washirika wa Muungano huu ni kelele za majukwaani
tu?
Mheshimiwa Spika,
Profesa
Palamagamba J.A.M. Kabudi wa Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam na mjumbe wa Tume aliwahi kusema kwenye Semina ya Wabunge Juu ya
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba iliyofanyika hapa Dodoma
tarehe 12 Novemba 2011 kwamba: “Katika kuandika katiba mpya, wabia wa
Muungano wanarudi kwa usawa.” Kwa sababu hiyo, na kwa kuzingatia
mapendekezo ya ‘hadhi na haki sawa’ baina ya Washirika wa Muungano
yaliyoko katika Rasimu ya Katiba, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inapendekeza kwamba idadi ya wawakilishi wa Zanzibar katika Bunge Maalum
iongezwe hadi kufikia nusu ya wajumbe wote wa Bunge Maalum.
Hili
linawezekana kwa namna mbili. Kwanza, kwa kuongeza idadi ya wajumbe
waliotajwa katika kifungu cha 22(1)(c) hadi 354 kama tulivyopendekeza
katika Maoni haya. Na pili, kwa kurekebisha kifungu cha 22(2) ili
kisomeke kwamba idadi ya wajumbe kutoka Zanzibar ‘haitapungua asilimia
hamsini na tano ya wajumbe hao.’ Kama pendekezo hili litakubaliwa na
Bunge lako tukufu, wajumbe wa Bunge Maalum kutoka Zanzibar wataongezeka
kutoka 214 kwa mujibu wa Sheria ilivyo sasa, hadi 323. Muhimu zaidi,
Bunge Maalum litakuwa limetimiza matakwa ya usawa wa Washirika wa
Muungano kwa kuwa na idadi sawa ya wajumbe katika Bunge hilo. Hili
litaondoa manung’uniko yanayoweza kujitokeza baadae kwamba Wazanzibari
hawakutendewa haki sawa katika Bunge la Katiba.
WATUMISHI WA BUNGE MAALUM
Mheshimiwa Spika,
Muswada
unapendekeza marekebisho mengine katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Hivyo basi, aya ya 4 inapendekeza marekebisho ya kifungu cha 24(4) kama
ifuatavyo: “Katibu wa Bunge Maalum baada ya kushauriana na Naibu wake
na taasisi husika, atateua kutoka katika Bunge, Baraza la Wawakilishi na
taasisi husika idadi ya watumishi kama itakavyoonekana inafaa kwa
utekelezaji wa majukumu na mamlaka ya Bunge Maalum.” Kama kilivyo hivi
sasa, kifungu hicho kinasomeka kama ifuatavyo: “Katibu wa Bunge Maalum
baada ya kushauriana na Naibu Katibu wa Bunge Maalum watateua watumishi
kutoka kwenye Bunge na Baraza la Wawakilishi kwa idadi watakayoona
inafaa kwa ajili ya kutekeleza kwa ufanisi majukumu ya Bunge Maalum.”
Mheshimiwa Spika,
Kama
inavyoonekana wazi, mabadiliko pekee yanayopendekezwa na Muswada ni
maneno ‘taasisi husika.’ Maneno haya hayajatafsiriwa mahali popote
katika Sheria, na Muswada uko kimya juu ya maana yake. Hata Maelezo ya
Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria mbele ya Kamati yako kimya juu ya
maneno hayo.
Ukimya
huu una mwangwi mkubwa. Kama pendekezo hili litakubaliwa, kutakuwa na
uwezekano wa watumishi wa Bunge Maalum la Katiba kuteuliwa kutoka katika
taasisi na idara mbali mbali za serikali, au hata taasisi zisizokuwa za
kiserikali. Kwa sababu Bunge Maalum litatekeleza majukumu yake kwa muda
maalum unaopendekezwa katika aya ya 6 ya Muswada huu, ni wazi watumishi
hao watatumikia Bunge Maalum on secondment kutoka kwenye taasisi zao za
mwanzo. Kwa maana hiyo, watumishi hao watawajibika kwa taasisi zao na
wanaweza kutumiwa na taasisi zao kutoa taarifa au siri muhimu juu ya
shughuli za Bunge Maalum kwa taasisi zao.
Kwa
upande mwingine, watumishi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wamepewa
kinga ya kikatiba inayowakataza kupokea maelekezo kutoka taasisi
nyingine nje ya Bunge. Kama kifungu cha 4(3) cha Sheria ya Uendeshaji
Bunge, Na. 14 ya 2008, inavyoweka wazi, katika utekelezaji wa majukumu
yao, watumishi wa Bunge “... hawatapokea maelekezo kutoka mahali popote
nje ya Utumishi (wa Bunge).” Katika mazingira haya, Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inapendekeza kwamba mapendekezo ya kurekebisha kifungu
cha 24(4) hayakidhi matakwa ya uhuru wa Bunge Maalum na, kwa sababu
hiyo, yasikubaliwe na Bunge lako tukufu.
Mheshimiwa Spika,
Kuna
hoja kubwa zaidi juu ya pendekezo hili. Hoja hii inahusu mamlaka ya
Katibu wa Bunge Maalum na Naibu wake kuteua watumishi wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano na Baraza la Mapinduzi Zanzibar kuwa watumishi wa
Bunge Maalum chini ya kifungu cha 24(4) cha Sheria, na pendekezo la
Muswada la kukifanyia marekebisho.
Kwa
mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Bunge, Katibu wa Bunge hana mamlaka ya
kuteua watumishi wa Bunge peke yake. Hayo, kwa mujibu wa Sheria hiyo, ni
mamlaka ya pamoja kati ya Katibu na Tume ya Utumishi wa Bunge na
utekelezaji wake unahitaji mashauriano kati ya vyombo hivyo viwili. Kwa
sababu hiyo, na kwa kuzingatia utaratibu wa Sheria hiyo, Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inapendekeza watumishi wa Bunge Maalum wateuliwe kutoka
miongoni mwa watumishi wa Bunge na Baraza la Wawakilishi baada ya
mashauriano kati ya Katibu wa Bunge Maalum na Naibu wake pamoja na
Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum. Pendekezo hili lina
faida kwamba watumishi wa Bunge Maalum watakuwa wameteuliwa na
watawajibika kwa Bunge Maalum na siyo kwa taasisi nyingine nje ya Bunge
Maalum. Kwa maana hiyo, pendekezo la Muswada juu ya uteuzi wa watumishi
wa Bunge Maalum nje ya Bunge la Jamhuri ya Muungano na Baraza la
Wawakilishi Zanzibar halina umuhimu na linapaswa kukataliwa.
TAFSIRI YA RASIMU YA KATIBA
Mheshimiwa Spika,
Muswada
unapendekeza marekebisho ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba inayohusu tafsiri ya maneno mbali mbali. Mapendekezo ya Muswada
yanahusu tafsiri ya maneno ‘Rasimu ya Katiba’ na ‘Kanuni.’ Pendekezo la
kutafsiri neno ‘Kanuni’ halina utatanishi wowote na Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inaliunga mkono. Kwa upande mwingine, Kambi Rasmi
Upinzani Bungeni inapinga tafsiri inayopendekezwa ya maneno ‘Rasimu ya
Katiba.’ Kwa mujibu wa aya ya 2 ya Muswada, maneno ‘Rasimu ya Katiba’
yatakuwa na maana ya “... Rasimu ya Katiba ambayo imetayarishwa na Tume
kutokana na maoni na mapendekezo ya wananchi chini ya Sheria.”
Pendekezo
hili linapingana na maudhui ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Kwanza,
pamoja na kwamba maoni ya wananchi ni chanzo muhimu cha ripoti ya Tume
na Rasimu ya Katiba, maoni hayo sio chanzo pekee cha ripoti ya Tume na
Rasimu ya Katiba. Kwa mujibu wa kifungu cha 17(4) cha Sheria, Tume
inatakiwa kupitia “na kuchambua michango, mawazo, maoni, taarifa na
mapendekezo yaliyokusanywa na kufanyiwa tathmini siku za nyuma....”
Kifungu hicho kimeorodhesha nyaraka nyingi muhimu na za kihistoria
ambazo zimejenga taswira ya kikatiba ya nchi yetu tangu uhuru wa
Tanganyika mwaka 1961. Tume inawajibika kuzipitia na kuzichambua nyaraka
zote hizo “katika kutekeleza majukumu yake chini ya Sheria hii....”
Pili,
Tume pia inawajibika kutumia “tafiti za kiuchambuzi na kitaalam
zitakazofanywa na Tume”, na “nyaraka nyingine zozote ambazo Tume itaona
ni muhimu.” Vyanzo vyote hivi vinatakiwa kutumika katika matayarisho ya
Rasimu ya Katiba. Kwa maana hiyo, madhara ya mapendekezo ya Muswada juu
ya tafsiri ya maneno ‘Rasimu ya Katiba’ ni ya wazi na mabaya. Kama
yatakubaliwa na kuwa Sheria, vyanzo vyote hivi vya ripoti ya Tume na
Rasimu ya Katiba vitakuwa redundant.
Aidha,
mapendekezo ya Tume na Rasimu ya Katiba yanayotokana na vyanzo hivyo
yatakuwa kinyume cha Sheria na yatabidi yaondolewe kwenye ripoti na
Rasimu ya Katiba. Kwa sababu hizi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inapendekeza kwamba maneno ‘Rasimu ya Katiba’ yatafsiriwe kumaanisha
“... Rasimu ya Katiba ambayo imetayarishwa na Tume kwa mujibu wa Sheria
hii.” Tafsiri hii inayopendekezwa inajumuisha maoni ya wananchi pamoja
na vyanzo vingine vyote vya ripoti ya Tume na Rasimu ya Katiba
vilivyoainishwa kwenye Sheria.
UHALALISHAJI WA KATIBA MPYA
Mheshimiwa Spika,
Muswada
unapendekeza marekebisho katika kifungu cha 31 cha Sheria ya Mabadiliko
ya Katiba kinachohusu ‘uendeshaji wa kura ya maoni.’ Inapendekezwa
kwamba kifungu hicho kifutwe na badala yake kiwekwe kifungu kipya
kitakachosema kwamba “masharti yote yanayohusu uendeshaji wa kura ya
maoni utawekwa na Sheria ya Kura ya Maoni.” Kwa vile tayari kuna Muswada
wa Sheria ya Kura ya Maoni, 2013, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inakubaliana na pendekezo hili.
Hata
hivyo, kifungu cha 31 sio kifungu pekee katika Sheria hii chenye
masharti ya uendeshaji wa kura ya maoni. Kuna vifungu vingine
vinavyotaja au kuweka utaratibu wa kura ya maoni. Ukweli ni kwamba
Sehemu ya Sita yote inayohusu ‘uhalalishaji wa Katiba Inayopendekezwa’
inahusika na masuala mbali mbali ya kura ya maoni. Vile vile, kifungu
cha 4(1)(n) na (2) navyo pia vinataja kura ya maoni. Kwa maoni ya Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, vifungu hivi pamoja na Sehemu ya Sita yote
vinahitaji kurekebishwa kwa kufutwa.
Mheshimiwa Spika,
Muswada
unapendekeza kufanya marekebisho katika kifungu cha 27(2) cha Sheria
kinachohifadhi ‘uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika Bunge
Maalum’ kwa kuweka kinga ya mashtaka dhidi ya wajumbe wa Bunge Maalum.
Zaidi ya hayo, Muswada unapendekeza muda usiozidi siku sabini kwa Bunge
Maalum kujadili Rasimu ya Katiba. Muda huo unaweza kuongezwa kwa siku
nyingine zisizozidi ishirini kwa ridhaa ya Rais “baada ya kukubaliana na
Rais wa Zanzibar....” Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inakubaliana na
mapendekezo yote haya ya Muswada kwa caveat kwamba pendekezo la muda wa
nyongeza lisiwekewe muda mahsusi. Hii ni kwa lengo la kuwezesha muda
kuongezwa kulingana na hali halisi ya majadiliano ndani ya Bunge Maalum.
JEDWALI LA MAREKEBISHO LA SERIKALI
Mheshimiwa Spika,
Serikali
iliwasilisha Jedwali la Marekebisho ya Muswada huu mbele ya Kamati
ikipendekeza marekebisho kadhaa katika Muswada na katika Sheria mama.
Mapendekezo haya ni ya aina mbili. Kwanza, ni mapendekezo ya marekebisho
ya Muswada uliosomwa mbele ya Bunge lako tukufu katika Bunge la Kumi na
Moja, na ambayo yalijadiliwa na Kamati na wadau mbali mbali. Haya ni
marekebisho yanayopendekezwa katika sehemu A, B na D ya Jedwali la
Marekebisho ya Serikali. Marekebisho haya yanaenda sambamba na matakwa
ya kanuni ya 84(3) na (4) ya Kanuni za Kudumu na kwa hiyo yanakubalika
kikanuni.
Kwa
upande mwingine, marekebisho yanayopendekezwa katika sehemu C na E za
Jedwali la Marekebisho ya Serikali ni mambo mapya ambayo hayakuwepo
kwenye Muswada uliosomwa kwa Mara ya Kwanza katika Bunge lililopita.
Marekebisho haya hayakujadiliwa na wadau wan je ya Bunge, na
hayajulikani kwa Wabunge wasiokuwa wajumbe wa Kamati ya Katiba, Sheria
na Utawala. Kwa sababu hiyo, marekebisho haya yanakiuka masharti ya
kanuni ya 86(7) ya Kanuni za Kudumu inayoelekeza kwamba “mjadala wakati
wa Muswada wa Sheria Kusomwa Mara ya Pili utahusu ubora na misingi ya
Muswada huo tu.” Ili kulinda heshima ya Bunge lako tukufu, Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni inakuomba, Mheshimiwa Spika, utekeleze wajibu wako
chini ya kanuni ya 5(2) ya Kanuni za Kudumu kwa kufutilia mbali sehemu C
na E za Jedwali la Marekebisho ya Serikali kwa sababu zinakiuka matakwa
ya kanuni tajwa ya Bunge lako tukufu.
Mheshimiwa Spika,
Sehemu
C ya Jedwali la Marekebisho ya Serikali tunaokuomba uifutilie mbali
inapendekeza kuongezwa kwa kifungu kipya cha 22A katika Sheria. Katika
pendekezo la awali kuhusu kifungu hicho, ilikuwa inapendekezwa kumfanya
Spika wa Bunge hili tukufu kuwa Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalum kwa
ajili ya kutengeneza Kanuni za Kudumu za Bunge Maalum, na kwa ajili ya
uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum. Baada ya
Kamati kuhoji na kuelezwa kwamba Spika/Mwenyekiti wa Muda atakuwa pia na
haki ya kugombea kuwa Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum
na hivyo kutengeneza mgongano wa wazi wa maslahi, Kamati ilielekeza
kwamba Katibu na Naibu Katibu wa Bunge Maalum watasimamia uchaguzi wa
Mwenyekiti wa Muda ambaye hatakuwa na haki ya kugombea nafasi ya
Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum. Hata hivyo, hoja ya
msingi kwamba hili ni pendekezo jipya ambalo halikuwepo kwenye Muswada
uliosomwa Mara ya Kwanza inabaki pale pale.
Kuhusu
sehemu E ya Jedwali la Marekebisho ya Serikali, sehemu hiyo
inapendekeza kufifisha matakwa ya kifungu cha 26(2) cha Sheria inayoweka
masharti ya kupitisha Katiba inayopendekezwa kwa theluthi mbili ya
wajumbe wote wa Bunge Maalum wanaotoka Tanzania Bara na idadi hiyo hiyo
ya wajumbe wanaotoka Zanzibar. Pendekezo jipya ni kupunguza idadi ya
uungwaji mkono hadi wingi wa kawaida (simple majority) ya wajumbe wote
wanaotoka Tanzania Bara na idadi hiyo hiyo ya wajumbe wanaotoka Zanzibar
endapo Bunge Maalum litashindwa kupitisha Katiba inayopendekezwa kwa
theluthi mbili baada ya kupiga kura mara mbili. Pendekezo hili nalo
linakiuka matakwa ya kanuni ya 86(7) na linapaswa kuondolewa katika
mjadala wa Muswada huu.
MENGINEYO
KUITISHWA TENA BUNGE MAALUM?
Mheshimiwa Spika,
Kuna
maeneo mengine ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo, kwa maoni ya
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, yanahitaji kufanyiwa marekebisho ili
kuwezesha utekelezaji bora wa Sheria hii. Eneo mojawapo ni masharti ya
kifungu cha 28(2) yanayoruhusu Bunge Maalum kuitishwa tena baada ya
kukamilisha majukumu yake kwa mujibu wa Sheria na kuvunjwa chini ya
kifungu cha 28(1) cha Sheria hii.
Kifungu
cha 28(1) kinasema: “Baada ya kutunga Katiba Inayopendekezwa, masharti
yatokanayo na mashrti ya mpito, Bunge Maalum litavunjwa na mamlaka ya
kutunga masharti ya Katiba inayopendekezwa, masharti yatokanayo na
masharti ya mpito yatakoma.” Kwa upande mwingine, kifungu cha 28(2)
kinatengua masharti ya kifungu cha 28(1) kwa maneno yafuatayo: "Kuvunjwa
na kukoma kwa mamlaka ya Bunge Maalum hakutachukuliwa kuwa kunaondoa
mamlaka ya Rais kuliitisha tena Bunge hilo kwa lengo la kuboresha
masharti yaliyomo kwenye Katiba inayopendekezwa.”
Mheshimiwa Spika,
Misingi
mikuu ya tafsiri za kisheria inaelekeza kwamba chombo chenye mamlaka au
majukumu ya kisheria ya kufanya jambo fulani kikishakamilisha
kutekeleza mamlaka au majukumu yake hayo kinakuwa functus officio katika
jambo hilo, yaani kinakuwa hakina mamlaka tena kisheria juu ya jambo
hilo. Huu ndio msingi wa kifungu cha 28(1) cha Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba. Athari ya kifungu cha 28(2) ni kulifufua kutoka katika wafu
Bunge Maalum ambalo, kwa mujibu wa kifungu cha 28(1), linakuwa limekuwa
functus officio baada ya kupitisha Katiba Mpya na masharti ya mpito. Na
hii inafanywa na Rais ambaye – na chama cha siasa anachokiongoza – ni
mdau mkubwa wa mchakato wa Katiba Mpya.
Katika
Maoni yetu wakati wa mjadala wa kupitishwa kwa Sheria hii mwezi Novemba
2011, tulisema yafuatayo juu ya kifungu hiki: “Maana halisi ya maneno
haya ni kwamba Rais atakuwa na mamlaka ya kuita tena Bunge la Katiba ili
lifanye marekebisho ya mambo ambayo yeye au serikali yake au chama
chake hawayapendi katika Katiba Mpya kabla haijapigiwa kura ya maoni na
wananchi! Kama chombo huru cha wananchi, Rais hawezi kujipa madaraka ya
kupingana na kauli ya wananchi kupitia Bunge la Katiba.”
Katika
mapendekezo yake kwa timu ya Wataalam wa Serikali iliyoundwa kufuatia
mkutano wa tarehe 26 Novemba, 2011 kati ya CHADEMA na Rais Jakaya
Kikwete, CHADEMA ilipendekeza kwamba kifungu cha 28(2) kifutwe kabisa.
Huu ni wakati muafaka kukiangalia upya kifungu hiki ambacho kinaweza
kuleta mgogoro usiokuwa na sababu endapo Rais ataamua kuliitisha tena
Bunge Maalum kwa sababu Serikali au chama chake hakikubaliani na Katiba
Mpya iliyopitishwa na Bunge Maalum.
MCHAKATO WA KATIBA YA TANGANYIKA NA ZANZIBAR
Mheshimiwa Spika,
Tarehe
3 Juni, 2013 Tume ilichapisha Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, 2013. Kwa kufanya hivyo, na kwa mujibu wa kifungu cha 18(5)
cha Sheria, Tume imekamilisha jukumu lake la kwanza baada ya
kukamilisha zoezi la kukusanya maoni ya Watanzania juu ya Katiba Mpya.
Rasimu hii inapendekeza mambo mengi na muhimu kwa mustakbala mzima wa
nchi yetu na tayari imezua mjadala mkali wa kitaifa. Mwanazuoni mmoja
maarufu nchini ameyaita mapendekezo ya Rasimu ‘Mapinduzi ya Kimya
Kimya’; wakati mwingine amehoji kama Rasimu hii ni ‘Mwarobaini au
Sanduku la Pandora?’ Aidha, Profesa Issa G. Shivji ambaye pengine ni
msomi maarufu wa masuala ya kikatiba katika sehemu hii ya Afrika,
ameonyesha kile ambacho amekiita ‘Utatanishi na Ukimya Katika Rasimu ya
Katiba Mpya.’
Kwa
maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kama ilivyo kwa wadau wengine
ambao wamezungumzia Rasimu hiyo ya Katiba, eneo muhimu pengine kuliko
yote ni muundo wa Jamhuri ya Muungano kama shirikisho lenye serikali
tatu. Kwa sababu hiyo, Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume imejikita
katika masuala ya Muungano tu. Na kwa mujibu wa Mwenyekiti wake, Tume
haikushughulikia masuala yasiyokuwa ya Muungano ya Tanganyika na
Zanzibar kwa sababu mambo hayo yanatakiwa kushughulikiwa na Katiba za
Washirika wa Muungano.
Kwa
maana hiyo, masuala haya sasa itabidi yashughulikiwe kwa utaratibu
mwingine wa kisheria Zanzibar na Tanganyika vile vile, ambao utakuwa
tofauti na utaratibu uliowekwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Kutokana na mapendekezo ya Rasimu ya Katiba, mchakato wa Katiba Mpya ya
Jamhuri ya Muungano hautakamilika bila ya kuwepo, na kukamilika, kwa
mchakato wa Katiba Mpya kwa masuala yasiyokuwa ya Muungano ya Tanganyika
na ya Zanzibar.
Mheshimiwa Spika,
Kuanza
na kukamilika kwa mchakato wa Katiba Mpya kwa mambo yasiyokuwa ya
Muungano ya Tanganyika na Zanzibar ni suala muhimu kwa muundo wowote wa
Serikali ya Jamhuri ya Muungano au hata bila Muungano kuwepo, kwa sababu
zifuatazo. Kwanza, hata kama muundo wa Muungano utakuwa wa serikali
moja, au mbili za sasa, au tatu zinazopendekezwa na Rasimu, ni lazima
masuala yote yanayoihusu Tanganyika yaingizwe kwenye mchakato wa Katiba
Mpya. Hii ni kwa sababu Rasimu inahusu masuala saba ya Muungano tu, na
Zanzibar ina Katiba yake tayari. Pili, hata kama wananchi wa Tanzania
watakataa kuendelea na Muungano wa aina yoyote na kudai uhuru kamili wa
Washirika wa Muungano, bado masuala ya Katiba Mpya ya Tanganyika na
Zanzibar yatahitajika kufanyiwa kazi. Tatu, bila masuala ya Tanganyika
kuamuliwa katika Katiba Mpya, mchakato mzima hautakamilika, na kwa maana
hiyo, hakuwezi kukawa na uchaguzi wowote wa Jamhuri ya Muungano kwa
upande wa Tanganyika.
Kwa
vyovyote vile, constitutional gridlock hii lazima ipatiwe suluhisho.
Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kwamba
mchakato wa Katiba Mpya ya Tanganyika na marekebisho ya Katiba ya
Zanzibar, 1984 uanze mara moja ili uendane sambamba na mchakato wa
Katiba Mpya ya Jambhuri ya Muungano. Kwa vyovyote vile, kwa maoni yetu,
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kama ilivyo sasa haiwezi kutumika kwa
ajili ya mchakato huo kwa sababu sheria hiyo ilitungwa kwa ajili ya
mchakato wa Katiba ya Muungano tu.
Tume
ya Mabadiliko ya Katiba iliundwa kwa ajili ya mchakato wa Katiba ya
Jamhuri ya Muungano. Na Tume yenyewe imekiri kwamba haikujishughulisha
na masuala yasiyokuwa ya Muungano kwa sababu hayakuwa sehemu ya majukumu
iliyokabidhiwa kisheria. Kwa muundo wake, Tume hiyo haiwezi
kujibadilisha na kuwa Tume ya Katiba ya Tanganyika. Kwa maana hiyo,
mchakato wa Katiba ya Tanganyika unatakiwa kuwekewa utaratibu mpya na
tofauti kabisa wa kisheria na wa kitaasisi. Hii itahitaji kutungwa kwa
sheria mpya kwa ajili ya mchakato huo.
Sambamba
na mchakato wa Katiba ya Tanganyika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inapendekeza kuanzishwa kwa mjadala juu ya masuala ya mpito kwa sababu
kuna uwezekano mkubwa kwamba Katiba Mpya, ya Muungano peke yake au ya
Muungano na za Washirika wake, yaani Tanganyika na Zanzibar, zisiwe
tayari kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015. Au hata kama zitakuwa tayari
kabla ya Uchaguzi Mkuu, kuna uwezekano mabadiliko makubwa ya kisheria na
ya kitaasisi yatakayohitajika kwa ajili ya utekelezaji wa Katiba Mpya,
yasiwe tayari kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao. Kwa kuangalia mfano wa Kenya,
Katiba Mpya ya nchi hiyo ilikamilika mwezi Agosti, 2010. Hata hivyo,
mabadiliko mbali mbali ya kisheria na kitaasisi kwa ajili ya utekelezaji
wa Katiba hiyo yalichukua zaidi ya miaka miwili na nusu hadi Uchaguzi
Mkuu wa mwezi Machi, 2013.
Ikumbukwe
kuwa Kenya haikuwa na suala la Muungano kama Tanzania. Sisi tuna
Muungano wa muundo ambao upande mmoja wa Muungano huo una dola yenye
Katiba na taasisi kamili za dola, wakati upande mwingine hauna dola wala
Katiba na taasisi kamili za dola. Hii ina maana kwamba maandalizi yetu
ya kisheria na kitaasisi yanaweza kuhitaji muda mrefu zaidi kuliko
ilivyokuwa kwa Kenya. Hatuna budi kuanza kuyafikiria na kuyajadili mambo
haya muhimu sasa.
------------------------------ ---------
TUNDU A.M. LISSU
WAZIRI KIVULI & MSEMAJI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI, WIZARA YA KATIBA NA SHERIA
No comments:
Post a Comment