Tanzania
inatarajia kuwa mmoja wa wazalishaji wakubwa wa chuma barani Afrika kwa
kuzalisha tani milioni moja kwa mwaka pindi uzalishaji wa madini hayo utakapoanza
mwaka 2018/19 katika eneo la Liganga wilayani Ludewa.
Hayo
yamebainishwa na Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa Shirika la Taifa la
Maendeleo (NDC) Abel Ngapemba wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo.
Alisema mradi huo wa
uzalishaji chuma utakaotekelezwa chini ya kampuni ya Tanzania China Mineral
Resources Limited (TCIMRL), ambayo ni kampuni ya ubia kati ya Shirika la Taifa
la Maendeleo (NDC) na Shirika la Sichuan Hongda Group (SHG) ya China utaenda
sambamba na uzalishaji wa madini ya Titanium na Vanadium.
“Mradi
huo ukikamilika tutaweza kuzalisha tani milioni 219 za chuma ambazo zitadumu
kwa zaidi ya miaka 70, na madini mengine yatakayotokana na mgodi huo ni
Titanium tani 175,400 kwa mwaka na Vanadium tani 5,000 kwa mwaka”. Alisema
Ngapemba.
Aidha Ngapemba alisema
kuwa uzalishaji huo utaiwezesha Tanzania kushika nafasi ya nne ikizifuatia nchi
za Afrika Kusini inayozalisha bidhaa za chuma tani milioni 8.5 kwa mwaka, Misri
tani milioni 8.0 na Libya tani milioni 2.0 kwa mwaka.
Mradi huu ni moja ya
miradi miwili iliyopo katika mkataba kati ya NDC na SHG uliotiwa saini Septemba
21, 2011 ya uanzishwaji wa mgodi wa makaa ya mawe na ujenzi wa kituo cha kufua
umeme wa megawati 600 katika eneo la Mchuchuma.
Miradi
mingine ni pamoja na ujenzi wa msongo wa umeme wa kilovoti 220 kati ya
Mchumchuma na Liganga, na uanzishwaji wa mgodi wa chuma pamoja na ujenzi wa kiwanda cha kuchenjua chuma ,
kiwanda cha kuzalisha bidhaa za chuma na ujenzi wa barabara kati ya Mchuchuma
na Liganga.
Chuma kinachozalishwa
duniani ni takribani tani bilioni 1.55 kwa mwaka, mzalishaji mkubwa ikiwa ni
China inayotoa tani milioni 711 kwa mwaka ambayo ni sawa na asilimia 46 ya
chuma chote kinachozalishwa duniani.
Miradi hii itakayogharimu
Dola za Kimarekani bilioni 3 inatarajiwa kuliingizia Taifa mapato ya Dola
bilioni 1.7 kwa mwaka itakapoanza uzalishaji wake.
No comments:
Post a Comment