KWA MAWASILIANO ZAIDI: E-mail: yusuf.badi2@gmail.com.

NSSF

TANGAZO

Wednesday, December 4, 2013

PROGRAM YA UTOAJI MATONE YA VITAMINI A YA NYONGEZA KWA WATOTO WALIO KATIKA UMRI WA MIEZI 6 HADI MIAKA MITANO.



Utangulizi
Upungufu wa vitamini na madini ni mojawapo ya matatizo makubwa ya kilishe yanayowaathiri hasa watoto na wanawake walio katika umri wa kuzaa hapa Tanzania. Takwimu za kitaifa juu ya demografia na afya ya jamii (Demographic and Health Survey) za mwaka 2010 zinaonesha kuwa hapa Tanzania upungufu wa vitamini A unaathiri asilimia 33 au theluthi moja ya watoto walio chini ya miaka mitano na asilimia 37 au zaidi ya theluthi moja ya wanawake walio katika umri wa kuzaa. Upungufu wa madini chuma unaathiri asilimia 59 au zaidi ya nusu ya watoto wadogo na karibu asilimia 41 au karibu ya nusu ya akina mama wajawazito, na pia upungufu wa madini joto unakadiriwa kuathiri asilimia 7 ya Watanzania. Utoaji wa matone ya vitamini A kwa watoto ni njia mojawapo ambayo inatumika kupunguza madhara ya upungufu wa Vitamini A. 
Kwa kuanzia tuangalie chanzo cha upungufu wa vitamini A
.
      Vitamini A ni mojawapo ya vitamini isiyotengenezwa na mwili na hivyo ni lazima itokane na vyakula viliwavyo na binadamu na wanyama
      Vyakula vyenye vitamini A kwa wingi
     Mboga na matunda hasa yenye rangi ya kijani na njano
     Samaki hasa dagaa
     Mafuta ya mawese
     Maini
Sababu za Upungufu
              Ulaji duni usiokidhi mahitaji ya Vitamini A mwilini
              Unyonyeshaji watoto maziwa ya mama usiokidhi mahitaji ya mtoto                (Sub optimal breastfeeding)
              Magonjwa ya mara kwa mara
              Utunzaji duni wa makundi husika
              Mgawanyo mbaya wa rasilimali (usiotoa kipaumbele kwa makundi maalum yaani kina mama na watoto

Waadhirika wakuu:
      Watoto walio katika umri wa chini ya miaka mitano
      Wanawake walio katika umri wa uzazi.
      Asilimia 33 ya watoto walio katika umri wa chini ya miaka 5 wana upungufu wa vitamini A
      Asilimia 37 ya akina mama walio katika umri wa kuzaa wana upungufu wa vitamini  A
Madhara ya Upungufu wa vitamini A
      Kutokuona vizuri kwenye mwanga hafifu
      Upofu
      Maradhi ya mara kwa mara kutokana na kupungua kwa kinga ya mwili
      Vifo hasa vya watoto
      Kushuka kwa elimu
      Kupungua kwa tija (maradhi yanayotokana na upungufu wa vitamini A huifanya familia husika kutumia rasilimali fedha na muda mwingi kwa ajili ya kumtibia mtoto).
Njia zinazotumika kupambana na tatizo
      Unyonyeshaji sahihi wa watoto
      Ulaji wa vyakula vyenye virutubishi hasa vya vitamin A kwa wingi na vya mchanganyiko
      Ulaji wa matunda na




mboga za majani kwa wingi (Vyenye rangi ya kijani kibichi na njano)
      Kutoa matone ya vitamini A kwa watoto walio katika umri wa miezi 6 hadi miaka mitano.
Utoaji wa matone ya vitamin A
Zoezi la utoaji wa matone ya vitamini A hutolewa kwa watoto walio katika umri wa miezi 6 hadi miaka mitano mara mbili kwa mwaka (Juni na Desemba).  Zoezi hili hufanyika sanjari na utoaji wa dawa za minyoo, dawa hizi hutolewa kwa watoto wenye umri wa mwaka 1 hadi miaka 5.
Watoto wa umri wa miezi 6 hadi miezi 12 hupewa kidonge chenye IU 100,000
Watoto wa umri wa mwaka mmoja hadi miaka mitano hupewa kidonge chenye IU 200,000.
Matone yanatolewa katika vituo vya afya na vituo vya muda (mobile clinics).  Lengo la kufanya hivyo ni kutaka kuwafikia watoto wengi zaidi. 
Kwa Tanzania zoezi limekuwa likiwafikia watoto zaidi ya asilimia 80.
Changamoto zinazolikabili zoezi
      Upatikanaji wa takwimu sahihi dhidi ya walengwa ili kupata matone ya vitamini A ya kukidhi mahitaji ya walengwa.
      Upatikanaji kwa takwimu za Idadi ya watoto waliopata matone ya vitamini A na kuzifikisha taarifa hizo katika ngazi husika kwa wakati ili ziweze kufanyiwa maamuzi.
            Kuweza kuwafikia walengwa wote hasa maeneo ambayo ni magumu kufikika – kisiwani, milimani nk.
Wazazi na walezi wanapaswa kufahamu nini? Ujumbe muhimu
Kila mzazi / mlezi wa mtoto aliye chini ya umri wa miaka 5 anapaswa kufahamu umuhimu wa vitamini A kwa ukuaji, maendeleo mazuri, afya na uhai wa mtoto. Ni muhimu wazazi/ walezi wafahamu kuwa vyakula  tunavyokula havikidhi mahitaji ya vitamini A mwilini kwa watoto, watoto  hula kiasi kidogo cha vyakula vyenye vitamini A wakati mahitaji yao ni makubwa.   Hivyo  hawana budi kupewa matone ya vitamini A mara mbili kila mwaka ili kukidhi mahitaji hayo.   Pia wanapaswa kufahamu wakati na mahali ambapo zoezi la utoaji wa matone ya vitamini A hufanyika ili waweze kuwapeleka watoto wao kila baada ya miezi sita.

No comments: