KWA MAWASILIANO ZAIDI: E-mail: yusuf.badi2@gmail.com.

NSSF

TANGAZO

Friday, January 24, 2014




TAMKO LA WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII
MHE DKT. SEIF SELEMAN RASHIDI (MB) KATIKA KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA UKOMA DUNIANI TAREHE 26/01/2014


Ndugu Wananchi,
Kwa zaidi ya miaka 50, siku ya Ukoma Duniani imekuwa ikiadhimishwa ulimwenguni kote kila Jumapili ya mwisho ya mwezi Januari. Siku hii iliasisiwa na mwandishi wa habari mfaransa Raoul Follereau aliyetumia muda wake mwingi kuzunguka dunia kueleza hali duni ya maisha ya watu walioathirika na ugonjwa wa ukoma. Siku hii ilianzishwa ili kuhimiza jamii kutoa kipaumbele kwa kuwapatia huduma stahiki wagonjwa wa ukoma na watu wenye machungu ya athari za ukoma.

Ndugu Wananchi,
Lengo kuu la maadhimisho haya ni kukumbusha umma wa watanzania juu ya ugonjwa huu. Ni dhahiri kuwa ugonjwa wa ukoma umekuwa ukiogopwa sana katika jamii yetu toka enzi na enzi hasa kutokana na ukweli kwamba unasababisha ulemavu wa kudumu mwilini na kufanya waathirika kuwa tegemezi na kutothaminiwa.

Ndugu Wananchi,
Tanzania ni miongoni mwa nchi 17 duniani ambazo bado zina viwango vya juu vya ugonjwa wa ukoma. Mwaka 2013, nchi yetu ilisaini makubaliano katika mkutano uliofanyika Bangkok Thailand  yalioazimia kuwa na dunia bila ugonjwa wa ukoma. (Bangkok declaration towards a leprosy - free world). Serikali yenu itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kubaini na kuendeleza jitihada sahihi za kutokomeza ukoma nchini.
Ndugu Wananchi,
Siku hii inatupa fursa ya kutathmini mwelekeo wa jitihada zetu nchini mwetu na zile za kimataifa katika kupambana na ugonjwa huu. Kauli mbiu katika maadhimisho ya mwaka huu ni “KABILI CHANGAMOTO ZA KUTOKOMEZA UKOMA. ONGEZA UBUNIFU.” (OVERCOMING THE REMAINING CHALLENGES. BE INNOVATIVE.” Kauli mbiu hii, inatutaka kubuni mikakati endelevu ili tuweze kutoa utatuzi wa changamoto zilizobaki katika kuutokomeza ugonjwa wa ukoma nchini Tanzania.

Miongoni mwa changamoto zinazotukabili ni uwezo wa watumishi wa afya kutambua kwa urahisi ugonjwa wa ukoma, jamii kuendelea kushikilia imani potofu juu ya ukoma na wagonjwa kuchelewa kujitokeza kupata matibabu hadi wanapopata ulemavu.

Ndugu Wananchi,
Dalili ya awali kabisa ya ukoma ni baka au mabaka kwenye ngozi yasiyo na uwezo wa kuhisi. Kwa kawaida hayawashi wala hayaumi. Mabaka haya hukosa hisia ya joto, mguso au maumivu.

Dalili nyingine za ukoma ni pamoja na vijinundu  vyenye rangi ile ile ya ngozi sehemu yo yote ya mwili. Naomba kutoa rai tuonapo mojawapo ya dalili hizi unashauriwa kwenda kwenye Kituo cha Afya kilicho karibu na wewe kwa uchunguzi na matibabu. Ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa anawahi kwenda kwenye Kituo cha Afya kwa uchunguzi pindi anapoona kuwa ana mabaka ya aina yoyote katika ngozi ya mwili wake. Hii itawawezesha wataalam wa afya kuchunguza na kubainisha kama mgonjwa ana Ukoma katika hatua za awali ili apate tiba sahihi mapema na kupona na hata kuepusha ulemavu usio wa lazima.

Ugonjwa wa ukoma hutibiwa na dawa mseto (Multi drug therapy au MDT). Tiba ya ukoma inachukua kati ya miezi sita hadi mwaka mmoja kulingana na aina ya ukoma. Mgonjwa ambaye ameanza tiba, siyo rahisi kuambukiza mtu mwingine na hivyo hakuna sababu ya kumtenga na anaweza kuendelea na shughuli za kawaida za maisha. Tiba ya Ukoma inapatikana nchini kote na hutolewa bila malipo kwa wagonjwa wote.

Ndugu Wananchi,
Kwa sasa takwimu zetu zinaonyesha ya kuwa nchini Tanzania, kwa miaka mitano iliyopita, idadi ya wagonjwa wapya wa ukoma inazidi kupungua kutoka 3,248 mnamo mwaka 2008 hadi 2,548 kwa mwaka 2012. Kampeni kabambe zinazoendeshwa katika maeneo ambayo ugonjwa wa ukoma bado ni tatizo kubwa na haujatokomezwa, zimeweza kupelekea wagonjwa kuzidi kupungua mwaka hadi mwaka. Kushuka huku kwa takwimu za ugonjwa wa ukoma kumetokana na juhudi  mbalimbali zinazofanywa na Serikali na Wahisani kwa kushirikiana na jamii kuhamasisha ugunduzi wa mapema wa wagonjwa wa ukoma. Kwa mwaka 2012, kampeni mahsusi zilifanyika katika wilaya za Liwale, Nanyumbu na Nkasi na kugundua wagonjwa Nanyumbu (74), Nkasi (100) na Liwale (91). Wote hawa wanaendelea kupata matibabu.

Kwa ujumla bado kuna wilaya 15 ambazo hazijafikia kiwango cha kutokomeza ukoma cha chini ya mgonjwa 1 kati ya watu 10,000 katika jamii husika. Wilaya hizi ni Liwale, Nachingwea, Mkinga, Pangani, Muheza, Rwangwa, Mvomero, Kilwa, Masasi DC, Chato, Nanyumbu, Lindi DC, Kisarawe, Newala na Songea DC.

Napenda kutoa rai kwa Halmashauri ambazo bado zina wagonjwa wengi, kutenga fedha  kwa ajili ya kuhamasisha wananchi kutambua dalili za awali za ukoma ili kuwahi matibabu na kuzuia maambukizi mapya. Kumbuka ukoma ni ugonjwa wa kuambukiza unaoletwa na vimelea hai na unaosambazwa kwa njia ya hewa kutoka kwa mgonjwa kwenda kwa mtu ambaye hana vimelea hivyo. Hivyo basi, ni muhimu kumuhimiza mwenzio aliyeathirika kwenda kupata tiba, ili kukata mnyororo wa maambukizi. 




Ndugu Wananchi,
Athari kuu ya ugonjwa wa ukoma ni ulemavu wa kudumu. Ulemavu unatokana na kuchelewa kwa uchunguzi na matibabu sahihi. Hapa Tanzania asilimia kumi  na moja (11%) ya wagonjwa wapya wa ukoma wanaojitokeza katika vituo vyetu kwa ajili ya uchunguzi na kuanza matibabu wanakuwa tayari wana ulemavu wa kudumu. Aidha, mgonjwa yeyote wa ukoma akigundulika tayari ameshapata ulemavu, ni dalili mbaya. Hii ina maana kuwa mgonjwa amechelewa kugundulika mapema na akapata ulemavu. Vile vile, ameendelea kusambaza vimelea vya ukoma katika jamii na kuaambukiza wengine.

Wito wangu kwenu leo hii, ni sote tujenge tabia ya kuchunguza miili yetu na pale tunapoona mabadiliko yoyote yanajitokeza twende mapema katika vituo vyetu vya huduma kuchunguzwa ili tupate ushauri na matibabu stahili.

Ndugu Wananchi,
Tatizo jingine ni unyanyapaa kwa wale waliougua na walioathirika na ukoma. Sababu kuu ni imani, mila potofu na ukosefu wa uelewa kuhusu ugonjwa huu. Ukweli ni kwamba ukoma ni ugonjwa unaoambukizwa kwa njia ya hewa na chanzo cha maambukizi ni mgonjwa wa ukoma ambaye hajagunduliwa wala kuanza matibabu. Mgonjwa akianza na kuzingatia matibabu hawezi kuambukiza tena na wale wote wanaouguza athari za ukoma baada ya kukamilisha matibabu ni walemavu wa viungo na siyo wagonjwa.

Ndugu Wananchi,
Ningependa kuchukua fursa hii kuwahakikishia ya kwamba, Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii itaendelea kushirikiana na Wahisani pamoja  na Halmashauri zote kuhakikisha kuwa:
1.    Dawa za kutosha zinapatikana na kusambazwa nchi nzima katika Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali zote.
2.    Huduma kwa wagonjwa wa ukoma zinapanuliwa kwa kushirikisha sekta binafsi na kutolewa bila usumbufu wowote kwa wagonjwa.
3.    Tiba sahihi kwa wale waliopata ulemavu utokanao na ukoma inatolewa ipasavyo.

Ndugu Wananchi,
Tunapofanya maadhimisho haya napenda kuchukua nafasi hii kwa niaba ya Serikali ya Tanzania kuyashukuru Mashirika mbalimbali ya ndani na nje kwa michango yao katika kuimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukoma hapa Tanzania.  Aidha,
inatubidi kukabili changamoto zilizopo na kuongeza ubunifu katika harakati zetu za kutokomeza ukoma.  Asanteni sana kwa kunisikiliza.

No comments: