Na. Aron Msigwa –MAELEZO
Dar es salaam.
Serikali imezindua rasmi baraza la
wataalam wa kurekebisha upeo wa macho kuona nchini kwa lengo la
kusimamia, kudhibiti na kuratibu utoaji wa huduma bora za macho nchini
litakalofanya kazi zake kwa mujibu wa sheria ya Optometria Na.12 ya
mwaka 2007.
Akizindua baraza hilo lenye
wajumbe 12 leo jijini Dar es salaam, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii
Dkt. Hussein Mwinyi amesema kuwa baraza hilo lina wajibu wa kuhakikisha
kuwa huduma bora za macho zinaendelea kutolewa kwa kuzingatia taratibu
na viwango vilivyowekwa pia kuzingatia umuhimu wa macho katika mwili wa
binadamu.
Amesema maisha ya kila siku ya
binadamu yanategemea uono wa macho na kuongeza kuwa hali ya kutoona
inasababisha maisha ya mwanadamu kuwa hatarini na wakati mwingine
kupoteza nguvu kazi ya taifa na kurudisha nyuma maendeleo ya taifa.
"Kila mmoja wetu anafahamu umuhimu
wa macho kikiwa kiungo muhimu sana katika mwili wa binadamu kama
vilivyo viungo vingine na tusipoona kutokana na matatizo ya macho maisha
yetu yanakuwa hatarini".
Amefafanua kuwa baraza hilo lina
wajibu wa kuhakikisha kuwa watoa huduma na wapokea huduma wanakua na
uhusiano mzuri na kulitaka baraza hilo kutoa elimu ya afya ya macho kwa
wananchi juu ya namna ya kutunza macho yao kabla ya madhara kutokea.
Dkt. Mwinyi amesema licha ya
Tanzania kukabiliwa na changamoto ya uhaba wa wataalam wa macho serikali
inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa huduma za macho
zinawafikia wananchi wengi hasa maeneo ya vijijini.
Amelitaka baraza hilo kuweka
mikakati ya kukabiliana na biashara holela ya miwani isiyokidhi viwango
iliyoenea hapa nchini kwa kushirikiana na Halmashauri za manispaa ili
kuondoa hatari inayoweza kulikumba taifa kutokana na kutumia miwani
isiyokidhi viwango.
"Hivi sasa biashara ya miwani
inayouzwa na wamachinga imeenea kila mahali nchini, jambo hili ni hatari
kwa afya ya macho kwa watanzania nafahamu linatokana na utandawazi
uliokithiri lakini ninyi kama baraza lazima mtafute mbinu ya kukabiliana
nalo" amesisitiza.
Kwa upande wake mwenyekiti wa
baraza hilo Bw. Adam Simbeye amesema kuwa baraza hilo jipya linachukua
nafasi ya baraza lililozinduliwa mwaka 2009 na kudumu kwa muda wa miaka
3.
Amesema pamoja na mambo mengine
baraza hilo katika kipindi cha miaka 3 limefanikiwa kujenga na kulinda
maadili ya watumishi wa fani hiyo, kulinda na kudhibiti vituo vya
kutolea huduna, kufanikisha zoezi la kusajili vituo vya kutolea huduma
nchini na kuhamasisha utii na ufuataji wa kanuni na taratibu za taaluma.
Aidha amesema kuwa baraza
linakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa fedha na kukosa ofisi maalum ya
kuendesha majukumu yake, aidha amesema baraza hilo limeshindwa
kusimamia suala la wafanyabisahara ndogo ndogo (wamachinga) kuuza miwani
holela mitaani.
Kwa upande wake mjumbe wa baraza
hilo Bw. Anamringi Macha akizungumza kwa niaba ya wajumbe wenzake
amesema kuwa uzinduzi wa baraza hilo unawapa nguvu kisheria kutekeleza
majukumu yake kwa kipindi cha miaka 3.
Amesema watafanya kazi kwa
uadilifu kwa lengo la kuhakikisha kuwa watanzania wote wanapata huduma
bora za macho kwa mujibu wa kanuni tarattibu na viwango vilivyowekwa.
"Kuzinduliwa kwa baraza hili
kunatupa nguvu kisheria kusimamia, kudhibiti na kuhakikisha huduma za
macho nchini zinatolewa kwa viwango na kwa kuzingatia kanuni na taratibu
na hili ndilo jukumu letu kuhakikisha maisha na afya za watanzania
zinakua salama" Amesema.
Wakati huo huo serikali kwa
kushirikiana na shirika la UNFPA, Mfuko wa Dunia na serikali ya Uholanzi
imekabidhi magari 9 ya kubebea wagonjwa na pikipiki 107 kwa ajili ya
kurahisisha huduma za ukusanyaji wa taarifa za afya, kusafirisha
wagonjwa na kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto katika maeneo
mbalimbali nchini.
Akikabidhi magari hayo kwa
wawakilishi wa hospitali zilizopewa magari na pikipiki hizo Waziri wa
Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hussein Mwinyi amesema magari na pikipiki
hizo yamegharimu fedha nyingi na kuwataka viongozi ambao maeneo yao
yamepewa vifaa hivyo kuvitunza ili vidumu na kuendelea kutoa huduma
husika.
" Vifaa vilivyo katika magari haya
vinatakiwa kutunzwa ili visiharibike au kuibwa ni muhimu sana
kukabidhiana kwa maandishi kila inapotokea watumishi wanabadilishana
zamu za kutoa huduma katika magari haya" amesisitiza Dkt. Mwinyi.
Amesema magari yenye vifaa vyote
yamegharimu shilingi milioni 250 kila moja na yatapelekwa kutoa huduma
ya kubebea wagonjwa katika Taassisi ya Mifupa nchini (MOI), Hospitali ya
KCMC ,Hospitali za wilaya ya Maswa, Hospitali ya mama Maria wa Kanisa
na wilayani Longido.
Aidha amesema magari mengine
yatapelekwa katika vituo vya afya wilayani Kahama na Bukombe na kuongeza
kuwa baadhi ya pikipiki zilizonunuliwa tayari zimepelekwa katika
halmashauri 26 nchini.
Pia amesema kuwa katika
kuhakikisha kuwa wagonjwa wanaobebwa katika magari hayo wanakuwa salama
hata kama hali zao ni mbaya wizara kwa kutumia wataalam wake imeandaa
orodha ya vifaa vinavyotakiwa kuwemo katika gari linalotumiwa kubeba
wagonjwa na kusambaza orodha ya vifaa hivyo kwa wadau husika.
No comments:
Post a Comment