Na Mwandishi Wetu, Songea
KAMPUNI ya Mantra Tanzania jana
imeanda washa yenye lengo la kuelimisha kamati ya Ushauri (RCC) Mkoa wa Ruvuma
juu ya madini ya urani ikiwa na lengo la kuongeza uelewa kwa wananchi mkoani
humo juu ya matumizi ya madini hayo.
Warsha hiyo iliyohudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Said Mwambungu iliwakutanisha
wadau mbalimbali kutoka katika Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), Baraza la Mazingira la Taifa (NEMC),
Wizara ya Nishati na Madini (MEM) na wawakilishi kutoka kampuni ya Mantra
Tanzania.
Akizungumza wakati wa warsha hiyo, Mkurugenzi wa Mantra Tanzania Asa
Mwaipopo alisema kuwa warsha hiyo ni mwendelezo wa elimu kwa umma kwa wananchi
wanaozunguka mradi wao wa Mto Mkuju pamoja wananchi waliopo pembezoni na mradi
huo.
"Matumizi mazuri ya urani duniani ni katika uzalishaji wa umeme kutoka
nishati ya nyuklia. Hivi sasa, kuna riakta za nyuklia 437 duniani ambazo
uzalishaji wake kwa jumla ni megawati 375,000
za umeme ambazo ni kadirio la asilimia 15 ya uzalishaji wa umeme dunia nzima.
Mwaipopo alisema kuwa matumizi ya madini yatakaochimbwa kwenye mradi wa Mto
Mkuju yatatumika kwa njia za amani huku akisisitiza kuwa kampuni yake pamoja na
wawekezaji wapo tayari kuendeleza mradi huo hata kama soko la madini hayo
limeendelea kuporomoka siku hadi siku.
"Tukio la Fukushima limeathiri kwa kiasi kikubwa soko la urani lakini Kampuni
ya Uranium One pamoja na wawekezaji wake wanaona kwamba ni suala la muda mfupi.
Tunaimani kuwa mradi wa Mto mkuju utajenga mahusiano ya muda mredu baina ya
waeekezaji wake, serikali na wananchi kwa jumla," aliongeza.
Aidha Bw. Lemigos Kawala kutoka Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC)
wakati akiwasilisha mada juu ya jukumu la TAEC katika utunzaji wa mazingira na
kuulinda umma dhidi ya mionzi na katika kukuza matumizi salama ya teknolojia ya
nyuklia alisema kuwa kiwango cha mionzi katika maeneo ya madini kinapimwa na
kufanyiwa tathmini.
Naye Dkt. Madoshi Makene Afisa Mazingira kutoka Baraza la
Taifa la Mazingira (NEMC) wakati wa warsha hiyo alisema kuwa kuna haja ya kuwa
na miradi endelevu inayokidhi mahitaji
ya leo na kesho bila kuathiri mazingira
kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Mwakilishi toka Wizara ya Nishati
na Madini, Zacharia Bongole aliwataarifu
wananchi kuwa Mradi wa Mto Mkuju umeruhusiwa na kupatiwa leseni chini ya Sheria
ya Madini ya mwaka 2010 ambayo ina vipengele vipya ambavyo vinajadiliwa katika
Mkataba wa Maendeleo ya Madini na wawekezaji. Aliitaarifu RCC kuwa serikali ina
sera ya Madini ya mwaka 2009 inayohusiana na Urani kama madini.
Mbunge wa Namtumbo, Mhe. Vita Kawawa wakati wa warsha alisisitiza kwamba
kuna umuhimu wa kampuni mbalimbali za madini kuhakikisha kwamba jamii zinazozunguka
migodi zipo katika nafasi nzuri ya kufaidika na uendeshaji wa migodi hiyo.
"Licha ya misaada ya kijamii kutoka katika miradi hiyo, serikali za
mitaa zipatiwe kodi kutoka kwa miradi hiyo ambayo itasadia kuinua maeneo hayo kwa
kiasi kikubwa kama itatumika vizuri," Kawawa alisitiza.
No comments:
Post a Comment