Na Anna Nkinda – Maelezo, Geita
Vijana wametakiwa
kushiriki katika suala la ulinzi na usalama wa maeneo wanayoishi kwa
kujiunga na vikundi vya ulinzi shirikishi ili kulinda na kusimamia
rasilimali za vijiji vyao.
Hilo litafanikiwa endapo vijana watakuwa na moyo wa kujituma na kutambua kuwa wanajukumu la kujenga taifa kwa kuhakikisha kuwa wanajiletea maendeleo yao na nchi kwa ujumla kutokana na kazi mbalimbali wanazozifanya.
Rai hiyo imetolewa mjini hapa jana na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara wakati
akiongea kwa nyakati tofauti na wanavikijiji vya Bugalama na Kitigiri
vilivyopo wilayani Geita alipozitembelea baadhi ya Vyama vya Kuweka
Akiba na Kukopa (SACCOS) zilizopata mkopo kupitia mfuko wa maendeleo wa vijana na fedha za maendeleo ya mfuko wa Halmashauri.
Dk. Mukangara alisema kuwa maendeleo ya nchi yanawategemea vijana ambao ndiyo nguzo ya taifa hivyo
basi wizara yake kupitia halmashauri za wilaya itahakikisha kuwa inatoa
mafunzo ya kuwajengea uwezo vijana jambo la muhimu ni kujiunga katika
vikundi vya maendeleo ili waweze kufikiwa kwa urahisi.
“Uongozi wa kijiji uhakikishe kuwa unawahimiza vijana na kuwajengea uwezo katika mtazamo wa kujitengemea, kujituma na kufanya kazi na kujiunga kwenye vikundi vya maendeleo ili iwe rahisi kupata mkopo kupitia SACCOS zilizopo vijijini mwenu” alisema Dk. Mukangara.
Aliwataka wanakijiji hao kuwasimamia vijana wao ili wanawajibike na kutambua kuwa
wanajukumu kubwa la kuhakikisha kuwa wanashiriki katika shughuli za
kilimo cha chakula na biashara jambo ambalo litasababisha kuwa na
chakula cha kutosha na kuepukana na janga la njaa.
Dk. Mkangara alisema, “Najua
nyinyi ni wakulima wazuri ila mnatakiwa kuboresha kilimo chenu ili
muweze kuzalisha mazao mengi na ya ziada , vijana wenu washiriki
katika kilimo hasa cha mazao ya biashara na siyo kuwaachia wazee peke
yao, wawe tayari kujituma na kuhakikisha kuwa chakula wanachokula
wamekitolea jasho kwa namna moja au nyingine”.
Naye
Mwenyekiti wa Kikundi cha Bucha la nyama ya ng’ombe ambacho kilipata
mkopo wa shilingi milioni mbili kutoka SACCOS ya Bugalama Mathias
Lucas alisema kuwa mkopo walioupata umewawezesha kupanuka kwa biashara
na mtaji, kuongezeka kwa wanachama kutoka wanne hadi kumi na kujenga bucha kubwa la kuuzia nyama.
“Mkopo tulioupata umetusaidia kujikwamu kiuchumi na kuweza kukabiliana na hali ngumu ya maisha , tumeweza kuwaajiri
na vijana wengine ambao hawakuwa na ajira lakini tunakabiliwa na
changamoto ya kutokuwa na mtaji wa kutosha na kufungwa kwa mnada wa
ng’ombe wilayani Geita .
Tunaiomba Serikali iweze kutuongezea fedha ya mtaji kwa kutupatia mkopo mkubwa zaidi na tupewe mafunzo ya ujasiriamali ili tuweze e kujua umuhimu wa kuweka akiba na kukopa”, alisema Lucas .
Akisoma taarifa ya kikundi cha Tupendane ambacho kilipata mkopo wa shilingi 1,400,000/= kutoka SACCOS ya Vijana Bukondo na kujishughulisha na kazi za ushonaji wa nguo
za kike mwenyekiti wa kikundi hicho Meshaka Philipo alisema kuwa
wamefanikiwa kuajiri mafundi cherehani vijana watatu na kuuza nguo kwa
wanakijiji na hivyo kupata fedha za kuinua mtaji wao.
Philipo
alizitaja changamoto zinazowakabili kuwa ni pamoja na mtaji mdogo,
elimu duni ya utunzaji wa kumbukumbu za fedha na ujasiliamali, upungufu
wa vitendea kazi kwa ajili ya ushonaji na usafiri ambao ni baiskeli kwa
ajili ya kupeleka nguo kwenye masoko ya nje ya kijiji.
Katika
kijiji cha Bugalama waziri Dk. Mukangara alitembelea vikundi vya Bucha,
Bodaboda na ushonaji ambavyo vilipata mkopo kutoka SACCOS ya kijiji
hicho kutipia mkopo wa halmashauri ya wilaya ya Geita wa shilingi
milioni tano na katika kijiji cha Kitigiri alikagua
vikundi vya Tupendane na Nyakalalo ambavyo vilipata mkopo kutoka SACCOS
ya Vijana Bukondo ambayo ilipata shilingi milioni tano kupitia mfuko wa
maendeleo ya vijana.
No comments:
Post a Comment