KWA MAWASILIANO ZAIDI: E-mail: yusuf.badi2@gmail.com.

NSSF

TANGAZO

Monday, December 17, 2012

TENGA AWASHUKURU WALIOPIGIA KURA WARAKA

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amewashukuru wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa kupigia kura waraka wa marekebisho ya Katiba, kwani wametimiza wajibu wao.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Dar es Salaam leo, Rais Tenga amesema marekebisho ya Katiba ni jambo muhimu, lakini lazima yapate ridhaa ya wanaohusika ambao ni wajumbe.

“Nawasukuru wajumbe kwa kupitisha jambo hili. Nawashukuru wote, waliokubali na waliokataa. Ndivyo demokrasia ilivyo. Tulitaka waseme ndiyo au hapana, hivyo tulitarajia kupata majibu yoyote kati ya hayo mawili.

Marekebisho mengine yalikuwa ni maelekezo (directives) kutoka FIFA na CAF. Katiba yetu inasema tutatekeleza maagizo ya CAF na FIFA, lakini kwa misingi ya utawala bora tuliona ni lazima tupate ridhaa kutoka kwa wajumbe,” amesema.

Jumla ya wajumbe waliopiga kura kwa njia hiyo ya waraka ni 103 ambapo 70 waliunga mkono wakati waliokataa ni 33. Idadi hiyo ni asilimia 68 ya kura zote zilizopigwa, hivyo kupatikana theluthi mbili ya kura zilizopigwa ili kufanya marekebisho kikatiba.

Vipengele vilivyoingizwa katika marekebisho hayo ni ‘club licencing’ kama ilivyoagizwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Kamati ya Rufani ya Uchaguzi wa TFF kama ilivyoshauriwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na kuondoa nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais.

Vilevile Kamati ya Utendaji itakutana Desemba 23 mwaka huu kufanya marekebisho ya Kanuni za Uchaguzi, kutokana na kupitishwa kwa marekebisho hayo ambayo yanaunda Kamati ya Rufani ya Uchaguzi wa TFF. Pia itachagua wajumbe wa Kamati ya Rufani ya TFF.

Mkutano Mkuu wa TFF ambapo pia utakuwa na ajenda ya uchaguzi utafanyika Februari 23 na 24 mwakani. Kwa mujibu wa Katiba ya TFF, wajumbe wanatakiwa kupewa taarifa ya Mkutano Mkuu siku 60 kabla.

RAMBIRAMBI MSIBA WA AMINA SINGO
Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha aliyekuwa mtangazaji wa habari za michezo katika kituo cha redio cha 100.5 Times FM, Amina Singo kilichotokea usiku wa kuamkia jana.

Msiba huo ni mkubwa katika sekta ya habari na mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti kupitia taaluma ya uhandishi wa habari, Amina alifanya kazi na TFF, hivyo mchango wake katika mpira wa miguu tutaukumbuka daima.

Tutamkumbuka kama mtangazaji wa habari za mpira wa miguu na michezo kwa ujumla.  TFF tunatoa pole kwa familia za marehemu Amina Singo, ndugu, jamaa na marafiki na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Mungu aiweke roho ya marehemu Amina Singo mahali pema peponi. Amina

SITA ZATINGA ROBO FAINALI UHAI CUP
Timu sita zimeshakata tiketi ya kucheza hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la Uhai inayoshirikisha wachezaji wenye umri chini ya miaka 20 (U20) wa klabu za Ligi Kuu ya Tanzania.

Hatua ya robo fainali ya michuano hiyo inayofanyika viwanja vya Karume na Chamazi, Dar es Salaam na kudhaminiwa na kampuni ya Said Salim Bakhresa kupitai maji Uhai itafanyika Desemba 19 mwaka huu kwenye viwanja hivyo hivyo.

Timu zilizofuzu kutoka kundi  A ni Coastal Union ya Tanga, Mtibwa Sugar ya Morogoro na JKT Ruvu ya Dar es Salaam. Kundi C ni Oljoro JKT ya Arusha na Ruvu Shooting ya Pwani wakati iliyofuzu kutoka kundi A hadi sasa ni Azam pekee.

Katika mechi zilizochezwa leo asubuhi (Desemba 17 mwaka huu) Coastal Union na Mtibwa Sugar zimetoka suluhu kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, wakati Uwanja wa Azam ulishuhudia African Lyon ikiifunga Mgambo Shooting mabao 2-1.

Nafasi mbili za robo fainali zilizobaki kutoka kundi B zinawaniwa na timu za Simba, African Lyon na Polisi Morogoro. Mechi itakayochezwa leo saa 10 jioni katika Uwanja wa Chamazi kati ya Polisi Morogoro na Simba ndiyo itakayoamua timu zitakazoungana na Azam kutoka kundi hilo.

Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments: