NA MWANDISHI WETU
KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana leo
amekutana na mabalozi wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na
kuwa na mazungumzo nao kwa nyakati tofauti, ofisini kwake, katika Ofisi
Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, jijini Dar es Salaam.
Mabalozi hao wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini ni Athumani Juma
Mpango wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo aliyetangulia kuwasili
ofisini kwa Katibu Mkuu na baada ya mazungumzo yao alifuatia Balozi, Dk.
Ben Rugangizi wa Rwanda.
Katika mazungumzo yao, mabalozi hao walimpongeza Kinana kwa
kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM, na kueleza kwamba vyama tawala
katika nchi zao vimepokea kwa furaha uteuzi huo.
"Chama chetu cha
PPRD kinakupongeza sana kwa uteuzi wako, na tunakutakia kila la kheri
katika kutekeleza jukumu hili kubwa ulilokabidhiwa", alisema Balozi wa
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mpango.
Mabalozi hao walisema wanakishukuru Chama Cha Mapinduzi kwa namna
wanavyosaidia nchi zao. Kwa wake Balozi Mpango alisema, Chama cha PPRD
kinapongeza juhudi zinazofanywa na CCM na Serikali yake kwa namna
kinavyosaidia jitihada za kuleta amani nchini DRC.
Kwa upande wa Balozi Dk. Rugangizi, alisema RPF ina mengi ya
kujifunza kwa upande wa Tanzania na CCM kama chama tawala kwa kuzingatia
uzoefu kilichonacho. Walisisitiza kuendeleza uhusiano uliopo hasa kwa
viongozi kutembeleana kama wafanyavyo sasa.
Ili kuonyesha mshikamano na ushirikiano, Katibu Mkuu wa CCM,
amemwalika Katibu Mkuu wa PPRD kuhudhuria sherehe za miaka 36 ya
kuzaliwa kwa CCM zitakazofanyika kitaifa mkoani Kigoma. Hatua hiyo
ilitokana na Balozi Mpango kuonyesha wasiwasi wake juu ya kuzorota kwa
uhusiano wa CCM na PPRD uliokuwapo hapo nyuma.
Hii ni mara ya tano kwa Katibu Mkuu kutembelewa na mabalozi wa nje wanaoziwakilisha nchi zao nchini.
No comments:
Post a Comment