HOTUBA YA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE,
RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,
KWENYE UZINDUZI WA MATOKEO YA AWALI YA
SENSA YA WATU NA MAKAZI YA MWAKA 2012,
VIWANJA VYA MNAZI MMOJA, DAR ES SALAAM
TAREHE 31 DESEMBA, 2012
Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal,
Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Balozi Seif Idd, Makamu wa
Pili wa
Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar;
Waheshimiwa Mawaziri;
Waheshimiwa Mabalozi;
Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;
Viongozi na watendaji wakuu wa Serikali;
Viongozi wa Vyama vya Siasa, Viongozi wa Dini, Viongozi wa
Jamii; Wanahabari;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Nashukuru kwa kunialika kuja kushiriki
kwenye tukio hili muhimu na la kihistoria la kutangaza matokeo ya awali ya Sensa
ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012. Haya ni matokeo ya kazi ya kuhesabu watu
iliyofanyika kwa siku 14 kuanzia tarehe 26 Agosti, 2012 hadi 4 Septemba, 2012.
Ndugu wananchi;
Napenda
kutumia nafasi hii kutoa pongezi za dhati kwa wale wote waliofanikisha zoezi la
kuhesabu watu na wale waliokamilisha uchambuzi unaotuwezesha leo kutangaza
idadi ya Watanzania ilivyo sasa. Kwanza
kabisa napenda kutambua Kamati ya Taifa ya Sensa iliyoongozwa na Mheshimiwa
Mizengo Peter Kayanza Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa na Mheshimiwa Balozi Seif Ali Idi,
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiwa Mwenyekiti upande wa Zanzibar. Nawashukuru kwa uongozi wao mzuri ambao
matunda yake ndiyo haya yanayotukusanya leo.
Pia nawashukuru wajumbe wa Kamati za Sensa za Mikoa na Wilaya nchini.
Pili, napenda kuwatambua viongozi na
wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya Jamhuri ya Muungano chini ya
uongozi wa Mama Albina Chuwa na wenzao wa Afisi ya Mtakwimu Mkuu wa Zanzibar
chini ya uongozi wa Ndugu Mohammed Hafidh Rajab. Nawapongeza kwa umahiri wao katika kuongoza,
kuratibu na kisimamia utekelezaji wa jukumu lenyewe la kuhesabu watu. Ni wao kuliko mtu mwingine ye yote ndiyo
waliokabidhiwa kazi ngumu ya kutengeneza mipango na taratibu za kufanya zoezi
lenyewe. Walitayarisha madodoso,
kuyachapisha, kuyasambaza, kuteua watu wa kuhesabu watu na wasimamizi wao. Waliwafundisha wajibu wao na kuwasimamia
katika utekelezaji wao. Ni wao pia waliohakikisha
kuwa madodoso yote yanakusanywa na uchambuzi unafanywa mpaka sasa tuko tayari
kutangaza matokeo.
Nawatambua
na kuwashukuru makarani wa sensa waliopita nyumba kwa nyumba kuhesabu watu na
kukusanya taarifa mbalimbali kwa mujibu wa madodoso waliyokuwa nayo. Tunatoa shukrani na pongezi maalum kwao kwa
sababu ni wao hasa waliowezesha kupatikana taarifa itakayotangazwa leo na
nyingine zitakazofuatia siku za usoni.
Kama si wao tusingekusanyika hapa
leo. Nawapongeza kwa umakini wao na moyo
wao wa uvumilivu na uzalendo. Haikuwa
kazi rahisi kwa ukubwa wa kazi yenyewe. Pia,
walikumbana na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na baadhi ya maeneo kuwa na
mazingira magumu ya kufanyia kazi kama vile ya usafiri. Lakini pia kulikuwa na
ugumu wa kupata taarifa kutoka kwa wanaoulizwa. Baadhi hawakutoa ushirikiano
unaotakiwa. Yalikuwepo pia matatizo ya
kupata huduma stahiki za kufanyia kazi na hasa posho. Nafahamu kuwa wapo bado wanaodai stahili zao. Hazina wamekiri hilo na kuahidi watalimaliza
haraka.
Ndugu
wananchi;
Kufanya sensa ni kazi kubwa na ghali
sana. Hata hivyo nchi zote duniani
hufanya sensa kwa sababu ya umuhimu wake.
Kupitia Sensa, hupatikana taarifa muhimu za kutumiwa na Serikali kupanga
mipango ya maendeleo ya nchi na jinsi ya kuhudumia wananchi. Taarifa hizo hutumika na wadau mbalimbali
katika shughuli zao za kuwahudumia wanadamu.
Ndiyo maana madodoso yalikuwa na mambo mengi na ndiyo maana tumeambiwa
kuwa taarifa ya leo ni ya mwanzo tu.
Zipo taarifa zitakazofuatia zenye uchambuzi wa mambo mbalimbali. Naomba tuwe na subira kwa taarifa mbalimbali tunazozitaka, kwani tutazipata
wakati wake utakapofika. Kwa niaba yenu
niwaombe wahusika wafanye kila wawezalo kuhakikisha kuwa taarifa hizo
zinapatikana kwa wakati uliopangwa.
Ndugu
Wananchi;
Nitakuwa mwizi wa fadhila kama sitawatambua
watu wengine wafuatao: Wa kwanza ni Hajat Amina Mrisho,
Kamishna wa Sensa ambaye tulimkabidhi jukumu la kutoa uongozi wa kisiasa katika
kazi ya kuhesabu watu na kuwa kiungo kati ya wataalamu na uongozi wa
Serikali. Vile vile, tulimpa kazi ya kusaidia
kufikisha ujumbe pande zote ili kuona kuwa mambo yanakwenda vizuri. Bahati nzuri mwenyewe ni mjuzi wa masuala ya
takwimu. Alitokea huko kabla ya
kumchukua na kumleta katika shughuli za uongozi wa kisiasa. Hivyo, kazi ilikuwa mikononi kwa mwenyewe. Namshukuru kwa kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi
mkubwa. Anao mchango mkubwa katika
mafanikio haya. Wa pili ni wananchi wa Tanzania.
Nawashukuru kwa ushirikiano wao.
Kabla na wakati wa Sensa, kulikuwa na purukushani na maneno mengi ya
upotoshaji na kutishia kuvuruga zoezi lenyewe.
Wapo wenzetu walioamua kuendesha kampeni ya kutaka watu wasusie. Wapo walioamua kufanya maandamano na mikutano
ya siasa wakati huo na jitihada zote za kuwasihi wasubiri siku 14 zipite walizipuuza. Wakati mwingine unashindwa kuelewa baadhi
yetu tuna dhamira gani katika kujihusisha na shughuli za siasa? Hivi inakuwaje
washindwe kutambua umuhimu wa kuhakikisha jambo kubwa kama hili linafanikiwa?
Hivi zoezi la sensa lisipofanikiwa kiongozi wa siasa au wa dini unanufaika
nini? Ndiyo maana nawashukuru sana
wananchi kwa ushirikiano wao uliofanya njama za kuvuruga zoezi kushindwa.
Ndugu
wananchi;
Wa
tatu
ni Wajumbe wa Kamati za Sensa za Mikoa na Wilaya kwa kufanikisha zoezi la Sensa
katika Mikoa na Wilaya zao. Nawashukuru Wakuu wa Mikoa na Wilaya wote nchini
kwa uongozi wao mzuri. Wa nne ni viongozi wa kijamii wakiwemo wa vyama vya
siasa, madhehebu ya dini na wa kimila waliosimama kidete kuhamasisha wafuasi
wao kushiriki katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi. Tunawashukuru kwa mchango
wao muhimu. Wa tano ni wamiliki wa vyombo vya habari na wana habari. Nawashukuru kwa kufanya kazi kubwa na nzuri
ya kuhamasisha na kuelimisha jamii katika kipindi chote cha utekelezaji wa
zoezi la Sensa. Wito wangu kwenu ni kwamba, endeleeni kuelimisha na kuhamasisha matumizi ya taarifa za Sensa kwa
maendeleo ya taifa letu.
Wa
mwisho, lakini siyo kwa umuhimu, nawashukuru sana washirika
wetu wa maendeleo wakiwemo UNFPA, DFID, JICA, CIDA na Benki ya Dunia kwa
mchango na msaada wao mkubwa. Nawashukuru Wenzetu hawa wametupa ushirikiano
mkubwa uliotuwezesha kufanikisha zoezi la Sensa hadi kufikia hatua hii ya sasa ya
kutoa matokeo ya awali. Naomba washirika
wetu wa maendeleo waendelee kushirikiana nasi kukamilisha kazi hii na pia
katika kuimarisha sekta ya takwimu nchini.
Ndugu
wananchi;
Baada ya kusema maneno hayo sasa nipo
tayari kuzindua rasmi matokeo ya awali ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka
2012. Kwa heshima na unyeyekevu mkubwa
natangaza kuwa kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika kwa siku 14
kuanzia Agosti 26, 2012, Tanzania ina watu 44,929,002
ambapo Tanzania Bara kuna watu 43,625,434 na Zanzibar kuna watu 1,303,568.
Katika Sensa ya tatu ya mwaka 2002 tulikuwa milioni 34.4 hivyo tumeongezeka kwa watu milioni 10.5 ongezeko ambalo ni sawa na asilimia 2.6 kwa mwaka.
Naomba taarifa hizi zitumike kwa madhumuni yaliyokusudiwa ambayo ni
kuboresha maisha ya kila Mtanzania.
Ndugu
Zangu;
Hii ni Sensa ya nne kufanyika nchini
tangu kuasisiwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1964. Sensa ya kwanza ilifanyika mwaka 1967 ambapo
nchi yetu ilikuwa na watu 12,313,054. Tanzania Bara ilikuwa na watu 11,958,654 na Zanzibar watu 354,400. Kwa maana hiyo, katika miaka 45 tangu Sensa ya kwanza na hii,
Watanzania wameongezeka kwa watu milioni
33.
Ndugu
Wananchi;
Kama kasi ya ongezeko la watu la asilimia 2.6 halitapungua ifikapo mwaka
2016 nchi yetu itakuwa na watu milioni 51.6.
Inawezekana idadi hiyo ikaonekana kuwa siyo tatizo la kuumiza kichwa kwa
nchi kubwa kama yetu, lakini ni mzigo mkubwa kwa taifa, jamii na uchumi kuwahudumia. Inabidi pawepo na mikakati madhubuti na
ionekane katika mipango ya maendeleo kuanzia sasa jinsi ya kuhudumia watu hao 51.6 na zaidi ya hao miaka
inayofuata. Kwa familia, lazima tutambue
umuhimu wa kupanga uzazi, vinginevyo hali ya maisha itashuka sana. Kwa ujumla hatuna budi kufanya kazi kwa bidii
zaidi na nguvu zaidi.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment