Na Anna Nkinda – Maelezo , Lindi
Wazazi mkoani Lindi wametakiwa kusimamia elimu ya watoto wao kwa
kuhakikisha kuwa wanaenda shule, wanakagua madaftari yao na
kuwarekebisha pale ambapo wamekosea kwa kufanya hivyo watafaulu vizuri katika masomo na kufanikiwa kimaisha kwani elimu ni msingi wa maendeleo.
Wito
huo umetolewa jana na mke wa Rais Mama Salma Kikwete kwenye kilele cha
sherehe za maadhimisho ya miaka 36 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) zilizofanyika kimkoa katika kata ya Rondo wilaya ya Lindi vijijini.
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM taifa toka
wilaya ya Lindi mjini alisema kuwa maendeleo ya elimu si mazuri katika
mkoa huo hivyo basi kina baba washirikiane na wake zao kuhakikisha kuwa
watoto wanahudhuria shule na kufanya vizuri katika masomo yao.
“Ninyi watoto nawasihi msome kwa bidii mkumbuke kuwa huu si wakati wa mtoto kukatisha masomo kwa ajili ya kupata ujauzito kwani mkiwa na elimu kutakuwa na uhakika wa kupatikana kwa wataalamu mbalimbali katika mkoa huu na kutatua tatizo la kutokuwa na wataalamu ambalo limedumu kwa muda mrefu”, alisema Mama Kikwete.
Aidha
Mjumbe huyo wa Halmashauri kuu ya CCM taifa aliwataka wanawake
kutosubiri nafasi za upendeleo za viti maalum bali wagombee nafasi
mbalimbali za uongozi ndani na nje ya chama ili wafike katika ngazi ya maamuzi na kuachana na fikira kuwa wao hawawezi kumwaga sera wakati wa uchaguzi.
Alimalizia kwa kuwataka wakazi wa mkoa huo kudumisha amani, upendo na utulivu, kufanya kazi
kwa bidiii, maarifa na kujituma, wakulima walime kilimo cha kisasa
ambacho kitawafanya wavune mazao mengi zaidi pia wafanyakazi watumie muda wa kazi kufanya kazi na kuwahudumia wananchi.
Mama
Kikwete pia alifungua jengo la ofisi ya CCM lenye thamani ya shilingi
milioni 35 ambalo limejengwa na Mbunge wa jimbo la Mtama ambaye ni
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Benard Membe.
Waziri Membe alisema kuwa jengo hilo lina vyumba sita ambavyo ni ofisi
za jumuia zote za chama hicho ambazo ni Vijana, Wanawake, Wazazi, pia
kuna ofisi za Mbunge, Mjumbe wa NEC na chumba cha mikutano.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo Ally Mtupa aliwataka wanachama wa chama hicho kuwa na mahusiano mazuri baina yao na viongozi
wanaowaongoza. Wakisikia jambo wasiwe na papara ya kukimbilia
kuandamana bali wafanye upelelezi kwanza na wakishabaini ukweli ndipo
wachukue hatua.
Mtupa
alisema, “Hivi sasa kuna watu wanapita mitaani na kupotosha ukweli kuwa
Serikali yetu haijaleta maendeleo, wamesahau kuwa wanatembea katika
barabara na kutibiwa katika Hospitali zilizojenga na CCM, tunawaomba watu hawa wawaheshimu viongozi wanaotawala kwani hata vitabu vya dini vinasisitiza umuhimu wa kuwatii viongozi waliopewa mamlaka ya kutawala”.
Sherehe
hizo zilienda sambamba na mchango wa matembezi ya mshikamono ambapo
zaidi ya shilingi milioni mbili zilipatikana, ufunguzi wa ofisi za CCM,
ufanyaji wa usafi wa mazingira , kuwatembelea wagonjwa mahospitalini,
utoaji wa kadi kwa wanachama wapya ambapo wanachama wa kawaida 286 ,
jumuia ya wazazi 63 na kutoka vyama vya upinzani 23 walipewa kadi.
No comments:
Post a Comment