LIGI
Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho
(Februari 23 mwaka huu) kwa mechi tatu, lakini macho na masikio ya
washabiki wa mpira wa miguu yatakuwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es
Salaam.
Uwanja
huo wa kisasa utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Yanga na makamu bingwa
Azam. Ingawa Azam imecheza mechi moja zaidi, lakini timu hizo
zinatofautishwa kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa kwenye
msimamo wa ligi huku kila moja ikiwa na pointi 36.
Pia
vinara wa ufungaji kwenye ligi kwa sasa wanatoka katika timu hizo
mbili. Kipre Tchetche aliyepachika mabao tisa hadi sasa ndiye
anayeongoza akifuatiwa na Didier Kavumbagu wa Yanga mwenye mabao manane.
Iwapo
timu yoyote itafanikiwa kuondoka na pointi tatu katika mechi hiyo
itakayochezeshwa na mwamuzi Hashim Abdallah wa Dar es Salaam, kasi ya
mbio za kuwania ubingwa itaongezeka. Waamuzi wasaidizi watakuwa Hamis
Chang’walu wa Dar es Salaam na John Kanyenye kutoka Mbeya wakati mezani
atakuwepo Oden Mbaga.
Mechi
nyingine za kesho ni Mgambo Shooting dhidi ya JKT Ruvu itakayochezwa
Uwanja wa Mkwakwani, Tanga wakati Tanzania Prisons watakuwa wenyeji wa
Polisi Dodoma kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
Jumapili
(Februari 24 mwaka huu), Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam utakuwa katika
hekaheka nyingine kwa Simba chini ya Mfaransa Patrick Liewig kuikabili
Mtibwa Sugar inayonolewa na nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Mecky
Maxime.
FDL YAENDELEA KUSHIKA KASI
Michuano
ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) inaendelea wikiendi hii kwa mechi kumi
na moja katika viwanja tofauti. Timu hizo zinapambana kutafuta hadhi ya
kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao 2013/2014.
Kesho
(Februari 23 mwaka huu) kundi A litakuwa na mechi moja
itakayozikutanisha timu za Mkamba Rangers na JKT Mlale itakayochezwa
Uwanja wa Ruaha mkoani Morogoro.
Kundi
B lenyewe litakuwa na mechi mbili; Tessema itacheza na Ashanti United
katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam wakati Ndanda
itaikaribisha Polisi Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Nangwanda mjini
Mtwara.
Raundi
ya 12 ya ligi hiyo kundi A itashuhudia timu zote nane zikiwa viwanjani;
Pamba vs Mwadui (CCM Kirumba), Polisi Tabora vs Polisi Mara (Ali Hassan
Mwinyi), Polisi Dodoma vs Morani (Jamhuri) na JKT Kanembwa vs Rhino
Rangers (Lake Tanganyika).
Jumapili
(Februari 24 mwaka huu) kundi A litakuwa na mechi kati ya Burkina Faso
dhidi ya Kurugenzi (Jamhuri), Majimaji vs Polisi Iringa (Majimaji)
wakati kundi B ni Transit Camp vs Villa Squad (Karume), na Green
Warriors vs Moro United (Mlandizi).
FIFA KUSIKILIZA MADAI YA ASAMOAH DHIDI YA YANGA
Shirikisho
la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limesema linapeleka rasmi madai
ya mchezaji wa zamani wa Yanga, Kenneth Asamoah kwenye chombo chake cha
utatuzi wa migogoro (Dispute Resolution Chamber) baada ya klabu hiyo
kutojibu chochote.
Awali
FIFA ilipokea malalamiko ya Asamoah kuwa anaidai Yanga dola 5,000 za
Marekani ambapo ilikuwa ni sehemu ya malipo yake (signing fee) baada ya
kujiunga na klabu hiyo.
Desemba
mwaka jana FIFA iliiandikia barua Yanga kupitia Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) ikitaka maelezo yake kuhusu madai hayo ya Asamoah,
lakini hadi sasa haijajibu madai hayo.
Kwa
mujibu wa FIFA, hatua ya uchunguzi wa suala hilo umekamilika, na sasa
linapelekwa rasmi katika chombo chake cha utatuzi wa migogoro (Dispute
Resolution Chamber) kwa ajili ya kufanya uamuzi.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment