Anna Nkinda – Maelezo, aliyekuwa Mbeya
Taasisi ya Wanawake na Maendelea (WAMA) imetoa msaada wa
cherehani ya kudarizi kwa mjane Fatma Almasi ambaye ni mkazi wa Ilomba
jijini Mbeya.
Makabidhiano ya Cherehani hiyo yalifanyika hivi karibuni Ikulu jijini Mbeya.
Akimkabidhi cherehani hiyo Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa WAMA
alisema kuwa moja ya kazi anazozifanya ni kumuinua mwanamke kiuchumi
hivyo basi alitoa cherehani hiyo ili iweze kumsaidia mjane huyo katika
maisha yake.
Mama Kikwete alisema kuwa cherehani hiyo ni moja ya vyerehani
walivyovipata kutoka nchini China kwani watu wanapoomba kusaidiwa siyo
kama vitu wanavyovihitaji vipo bali nao wanatafuta sehemu mbalimbali
wakipata wanafikisha kwa wahitaji.
“Nakutakia kila la heri katika kazi zako ila usisahau kuleta mrejesho
kama kazi inaendelea au la, isije ikatokea baada ya muda cherehani
ikauzwa hiyo siyo maana yake bali ifanye kazi ya kuzalisha ili nawe
uweze kujiinua kiuchumi”, alisema Mama Kikwete.
Kwa upande wake Fatma Almasi alimshukuru Mama Kikwete kwa msaada
aliompatia kwani amekuwa akihitaji kuwa na cherehani ya kudarizi kwa
kuwa uwezo wa kudarizi anao lakini hakuwa na kitendea kazi na aliahidi
kuongeza cherehani kingine kutokana na nguvu zake mwenyewe.
Fatma alisema, “Kinamama tujitahidi kujikwamua kimaisha kwani mwanamke
akiwezeshwa anaweza, tusiwe wategemezi kwa kina baba na mtu asijione
kuwa yeye ni mjane au anaishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) hawezi
kufanya jambo lolote na kuona kuwa ni mwisho wa maisha bali ajitahidi
kuwa mjasiriamali kwa kufanya hivyo ataweza kukabiliana na hali ngumu
ya maisha”.
Aliwaomba wanawake kumuunga mkono na kumtia nguvu Mama Kikwete kwani
ana moyo wa huruma na upendo wa kuwasaidia kina mama na watoto wa kike.
Taasisi ya WAMA imekuwa ikiwainua wanawake kiuchumi, kutoa ufadhili wa
masomo kwa watoto wa kike ambao hawakupata nafasi ya kusoma, kuimarisha
afya ya mama wajawazito na watoto na kuwasaidia watoto yatima na
wanaoishi katika mazingira hatarishi.
No comments:
Post a Comment