Anna Nkinda – Maelezo, aliyekuwa Mbeya
VIONGOZI wa Serikali, Dini na Vyama vya Siasa nchini
wametakiwa kuondoa tofauti zao na kutumia majukwaa kuhubiri amani na
upendo ili kudumisha mshikamano na utulivu ndani ya jamii.
Rai hiyo imetolewa hivi karibuni na Mchungaji wa Kanisa la Moravian
Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi Ushirika wa Itiri Daniel Siame
wakati wa ibada ya mazishi ya Ditective Sagenti Christopher Kyendesya
aliyefariki Juni 19 mwaka huu wilayani Kisarawe mkoani Pwani kwa ajali
ya Pikipiki.
Mchungaji Siame alisema kuwa Serikali haina dini bali jamii ndiyo
inadini mbalimbali zikiwemo za Ukristo, Uislamu na Upagani na kuwaomba
viongozi hao pale wanapokutana na wananchi kuhubiri mambo yanayompendeza
Mwenyezi Mungu.
“Inawezekana kuwa ndani ya dini zetu kuna watu ambao wanamapokeo ya dini
tu na siyo kumtangaza Mwenyezi Mungu hivyo basi sisi kama viongozi wa
Serikali, Dini na Vyama vya siasa tunakazi kubwa ya kutangaza mambo ya
kumpendeza Mwenyezi Mungu na amani na siyo mambo ya uchochezi”, alisema
Mchungaji Siame.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro alimshukuru
mchungaji huyo kwa kuwahimiza watu wote wakiwemo viongozi na wananchi
kuhusu umuhimu wa amani na upendo katika jamii.
Kandoro alisema kuwa ni jukumu lao viongozi wa Serikali, Dini na
wanasiasa kutumia lugha ya kuwajenga watanzania ili waone kuwa amani ni
silaha ya maisha yao ya kila siku kwani ikivurugika msingi mkubwa wa
maisha unaharibika na hakuna hata mmoja atakayefurahi kuona kuwa amani
na upendo vinatoweka.
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ni miongoni mwa viongozi mbalimbali
waliohudhuria mazishi hayo wakiwemo pia maofisa wa Jeshi la Polisi,
wanasiasa, wasomi na watendaji wa Serikali.
No comments:
Post a Comment