Na Anna Nkinda – Singapore
Watoto waliotengwa na jamii kutokana na tabia ya kutokuwa na maadili mazuri  (watukutu)  kama watapewa nafasi ya kupata mafunzo  ya kutosha ya dini, elimu ya darasani  na kuonyeshwa msingi mzuri wa maisha wanaweza kubadilika na kuwa watoto wema.
Hayo yamesemwa leo na Mama Sahnim Sokaimi ambaye ni mkuu wa kituo cha kurekebisha tabia za watoto wa kike watukutu cha PERTAPIS kilichoko nchini Singapore wakati akiongea na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete alipotembelea kituo hicho.
Alisema
 kuwa chuo hicho kinawapokea watoto wa kike kuanzia umri wa miaka 12 
hadi 21 ambao mahakama imewakuta na makosa mbalimbali ikiwa  ni
 pamoja na uvutaji wa sigara chini ya miaka 18, utumiaji wa madawa ya 
kulevya na kufanya biashara ya kuuza mwili (sexual activities). 
“Tuliamua
 kuanzisha kituo hiki baada ya kuona kuwa kuna tatizo kubwa la 
kuharibikiwa kwa watoto ikiwa ni pamoja na utumiaji wa madawa ya kulevya
 lakini baada ya watoto hawa kuwapa misingi mizuri ya malezi na maisha 
wameweza kubadilika na kuwa wasichana  wema wanaofuata dini”, alisema Mama Sokaimi.
Aliendelea
 kusema kuwa wasichana hao wamehukumiwa na mahakama kifungo cha miezi 
sita hadi miaka mitatu kutokana na makosa mbalimbali waliyoyafanya na 
wakiwa katika kituo hicho wanapata mafunzo ambapo baada ya kumaliza 
kutumikia adhabu ya makosa yao wanakuwa wamebadilika kitabia na kurudi 
kulelewa na familia zao.  
Alimalizia
 kwa kusema kuwa wazazi wanatakiwa kuchangia gharama za watoto wao 
kupata mafunzo kituoni hapo kiasi cha dola za Singapore 250  lakini
 wazazi wengi hawafanyi hivyo jambo ambalo linasababisha kituo 
kukabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha na hivyo kuomba msaada kutoka kwa 
wadau mbalimbali.
Kwa
 upande wake mama Kikwete aliwapongeza wafanyakazi wa kituo hicho kwa 
kazi kubwa wanayoifanya ya kurekebisha tabia za watoto wa kike ambazo 
hazikubaliki na jamii na kuwafanya kuwa wasichana na wamama wazuri ambao
 wanafanya kazi mbalimbali za kujitegemea kimaisha.
Mama Kikwete alisema kuwa  jukumu la kuwalea na kurekebisha tabia za watoto ni la jamii nzima na kuwaomba wafanyakazi wa kituo hicho kuja  nchini ili nao wajifunze na kuona ni jinsi gani wanaweza kushirikiana  kwa pamoja kuwasaidia watoto wenye matatizo kama hayo.
Aidha
 mama Kikwete pia alitumia taaluma yake ya ualimu na kutumia muda mfupi 
aliokutana na wasichana hao na kuwafundisha somo la kiingereza kwa 
kuwaelekeza umoja na wingi wa baadhi ya vitu.
Kituo
 hicho chenye jumla ya wasichana 54 kilianzisha mwaka 1990 kinatoa 
mafunzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na elimu ya Sekondari na msingi kwa 
wale ambao walikatisha masomo yao, ufundi wa kujitegemea, mapishi, stadi
 za maisha, utengenezaji wa nywele, ushonaji wa nguo na mafunzo  ya kiroho.
Mama Kikwete ameambatana na mumewe rais Dk. Jakaya Mrisho Kikwete nchini Singapore kwa  ziara ya kikazi ya siku mbili.
No comments:
Post a Comment