KWA MAWASILIANO ZAIDI: E-mail: yusuf.badi2@gmail.com.

NSSF

TANGAZO

Thursday, August 29, 2013

MECHI YA YANGA, COASTAL YAINGIZA MIL 152/-

Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Yanga na Coastal Union iliyochezwa jana (Agosti 28 mwaka huu) katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 152,296,000.

Watazamaji 26,137 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo namba 14 ya VPL msimu wa 2013/2014 iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 36,947,427.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 23,231,593.22.

Mgawo mwingine ni asilimia 15 ya uwanja sh. 18,786,827.52, tiketi sh. 3,818,890, gharama za mechi sh. 11,272,096.51, Kamati ya Ligi sh. 11,272,096.51, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 5,636,048.26 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 4,383,593.09.

COPA COCA-COLA KANDA KUANZA SEPT 2
Michuano ya Copa Coca-Cola kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 inayoshirikisha mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani inaanza kutimua vumbi Septemba 2 mwaka huu katika vituo sita tofauti.

Kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa leo (Agosti 29 mwaka huu), kituo cha Mwanza mechi zake zitachezwa katika viwanja vya Alliance ambapo timu zitakazofungua dimba ni Kagera vs Kigoma, Mara vs Tabora, Simiyu vs Geita na Mwanza vs Shinyanga.

Kituo cha Mbeya ambapo mechi zitachezwa viwanja vya Iyunga ni Katavi vs Njombe, na Ruvuma vs Mbeya. Kituo cha Pwani ni Ilala vs Kaskazini Unguja, na Lindi vs Pwani.

Ufunguzi katika kituo cha Arusha ambapo mechi zake zitachezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta AMri Abeid ni Manyara vs Kilimanjaro, na Arusha vs Singida.

Uwanja wa Jamhuri ambapo utatumika kwa mechi za kituo cha Morogoro, Tanga itacheza na Dodoma wakati Morogoro itaumana na Temeke. Mjini Zanibar kwenye Uwanja wa Chuo cha Amaan ni kati ya Kaskazini Pemba na Mjini Magharibi, na Kusini Pemba dhidi ya Kusini Unguja.

USAILI WAGOMBEA TFF, TPL BOARD KUANZA KESHO
Usaili kwa wanaoomba kuteuliwa kuwa wagombea uongozi katika uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na ule wa Bodi wa Ligi Kuu (TPL Board) unaanza kesho (Agosti 30 mwaka huu).

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Agosti 30 mwaka huu ni usaili kwa waombaji uongozi wote katika Bodi ya Ligi Kuu pamoja na waombaji uongozi wa TFF kwa kanda namba 11 (Morogoro na Pwani), kanda namba 12 (Kilimanjaro na Tanga) na kanda namba 13 (Dar es Salaam).

Agosti 31 mwaka huu ni kanda namba sita (Rukwa na Katavi), kanda namba saba (Mbeya na Iringa), kanda namba nane (Njombe na Ruvuma), kanda namba tisa (Lindi na Mtwara) na kanda namba kumi (Dodoma na Singida).

Usaili kwa kanda namba moja (Geita na Kagera), kanda namba mbili (Mara na Mwanza), kanda namba tatu (Simiyu na Shinyanga), kanda namba nne (Arusha na Manyara) kanda namba tano (Kigoma na Tabora), na nafasi za Rais na Makamu wa Rais wa TFF utafanyika Septemba Mosi mwaka huu.

Waombaji wote wamepangiwa muda wao wa usaili. Kwa mujibu wa ratiba usaili ufanyika kuanzia saa 3 kamili asubuhi hadi saa 2 usiku. Wasailiwa wote wanatakiwa kuzingatia muda waliopangiwa.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments: