KWA MAWASILIANO ZAIDI: E-mail: yusuf.badi2@gmail.com.

NSSF

TANGAZO

Wednesday, September 25, 2013

MAMA KIKWETE AKIOMBA CHUO KIKUU CHA MONMOUTH KUFUNDISHA LUGHA YA KISWAHILI.

Na Anna Nkinda – New York

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete amekiomba chuo kikuu cha Monmouth cha mjini New Jersey nchini Marekani  kufundisha wanafunzi wake lugha ya Kiswahili kama lugha ya kigeni ili wakazi wa eneo hilo waweze kuitumia katika mawasiliano pale itakapohitajika.

Mama Kikwete ambaye pia  ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA)  ametoa  ombi hilo leo wakati akiongea na uongozi wa chuo hicho alipowatembelea yeye na ujumbe wake.
Alisema  hivi sasa lugha ya kiswahili  inakuwa kwa kasi na kutumika katika maeneo mengi hasa nchi za Afrika Mashariki na Kati hivyo basi nao wawafundishe wanafunzi wao ili wakienda katika nchi hizo iwe ni rahisi kwao kuwasiliana.

“Kiswahili ni lugha ya taifa letu la Tanzania ambayo tunaitumia katika mawasiliano, mkiwafundisha wanafunzi wenu lugha hii nao watawafundisha wenzao hivyo itakuwa ni rahisi kwao kuwasiliana hasa wakisafiri na kukutana na watu wanaotumia lugha hii”, alisema Mama Kikwete.
Kwa upande wake makamu rais wa chuo hicho Dk. Edward Christensen alimshukuru mama Kikwete kwa kutembelea chuo hicho na kusema kuwa ombi lake la chuo hicho kufundisha lugha ya Kiswahili wamelisikia na wataangalia jinsi gani watalifanyia kazi.

Aidha Dk. Christensen aliwaomba wakufunzi na watu wenye utaalamu wa mambo mbalimbali kutoka nchini Tanzania kwenda katika chuo hicho kufanya midahalo na wafanyakazi na wanafunzi wa chuo hicho.

Chuo hicho kinawanafunzi wapatao 6300 kutoka ndani na n je ya nchi 29 na kinatoa kozi mbalimbali zikiwemo za Sayansi na sanaa katika  ngazi ya cheti, shahada na shahada ya uzamili.

No comments: