Jamal
Emil Malinzi ndiye Rais mpya wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF). Malinzi ameshinda wadhifa huo katika uchaguzi wa Kamati ya
Utendaji ya TFF uliofanyika juzi (Oktoba 27 mwaka huu) jijini Dar es
Salaam.
Aliibuka
na ushindi wa kura 73 dhidi ya mpinzani wake pekee Athuman Jumanne
Nyamlani aliyepata kura 52. Nafasi ya Makamu wa Rais imetwaliwa na
Wallace Peter Karia aliyepata kura 67 na kuwashinda Ramadhan Omari
Nassib kura 52 huku Imani Omari Madega akipata kura sita.
Akizungumza
mara baada ya kuchaguliwa, Rais Malinzi ametaka ushirikiano kutoka kwa
wadau wote akiwemo mpinzani wake Nyamlani katika kuhakikisha mpira wa
miguu nchini unasonga mbele.
Pia
ametoa msamaha kwa watu wote waliokuwa wamefungiwa kuanzia ngazi ya
wilaya, mkoa na TFF. Msamaha huo hauwahusu wale waliofungiwa kwa makosa
ya rushwa au kupanga matokeo. Vilevile msamaha huo hauhusu adhabu
zilizotolewa katika ngazi ya klabu.
Rais Malinzi pia amevunja kamati zote za TFF ambapo ataziunda upya kwa kushirikiana na Kamati ya Utendaji.
Kwa
upande wa wajumbe wa Kamati ya Utendaji walioshinda ni Kalilo Samson
(Kanda namba 1- Geita na Kagera) aliyepata kura 102 za ndiyo na 17 za
hapana. Kanda namba 2- Mara na Mwanza, mshindi ni Vedastus Lufano
aliyepata kura 51 dhidi ya Jumbe Odessa Magati (11), Mugisha Galibona
(24), na Samwel Nyalla (39).
Epaphra
Swai ndiye mshindi wa Kanda namba 3- Shinyanga na Simiyu kwa kura 63
dhidi ya Mbasha Matutu aliyepata 61. Kanda namba 4- Arusha na Manyara
mshindi ni Omali Walii Ali aliyepata kura 53 dhidi Elley Mbise (51), Ally Mtumwa (19).
Kanda namba 4- Kigoma na Tabora, mshindi ni Ahmed Idd Mgoyi aliyepata kura 92 dhidi ya 28 za Hamisi Yusuf Kitumbo.
Ayubu
Nyaulingo na Blassy Mghube Kiondo ameshinda Kanda namba 6- Katavi na
Rukwa kwa kura 73 dhidi ya Ayubu Nyaulingo aliyepata 52. Ayoub Shaibu
Nyenzi ndiye mshindi wa Kanda namba 7- Iringa na Mbeya kwa kupata kura
59 na kuwapiku David Samson Lugenge (8), John Exavery Kiteve (12) na
Lusekelo Elias Mwanjala (46).
Kanda
namba 8- Njombe na Ruvuma inawakilishwa na James Patrick Mhagama
aliyepata kura 93 dhidi ya 31 za Kapteni mstaafu Stanley William
Lugenge. Athuman Kingombe Kambi ndiye mshindi wa Kanda namba 9- Lindi na
Mtwara kwa kura 84 akiwazidi Francis Kumba Ndulane (30) na Zafarani
Mzee Damoder (11).
Hussein
Zuberi Mwamba ametetea ujumbe wa Kanda namba 10- Dodoma na Singida kwa
kura 63 akiwapiku Stewart Masima (58) na Charles Komba (4). Geofrey
Irick Nyange ameshinda Kanda namba 11- Morogoro na Pwani akipata kura 78
dhidi ya Juma Pinto (26), Farid Nahdi (14), Riziki Juma Majala (5) na
Twahil Twaha Njoki (2).
Kanda
namba 12- Kilimanjaro na Pwani, Khalid Abdallah Mohamed ndiye
aliyeibuka kidedea kwa kura 69 dhidi ya 54 za mpinzani wake Davis Elisa
Mosha. Kidao Wilfred Mzigama ameshinda Kanda namba 13- Dar
es Salaam kwa kupata kura 60 dhidi ya wapinzani wake Muhsin Said
Balhabou (50), Omar Isack Abdulkadir (10) na Alex Crispine Kamuzelya
(4).
KIM AITA 30 FUTURE YOUNG TAIFA STARS
Kocha
Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen ametaja kikosi cha wachezaji 30 wa
timu ya pili (Future Young Taifa Stars) kitakachoingia kambini Novemba 9
mwaka huu ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya michuano ya Kombe la
Chalenji.
Kipa
Ivo Mapunda wa Gor Mahia ya Kenya ni miongoni mwa wachezaji walioitwa
na Kim kwenye kikosi hicho ambacho hukitumia kuangalia uwezo wa
wachezaji kabla ya kuwajumuisha kwenye timu ya wakubwa.
Kikosi
hicho kamili ambacho Novemba 13 kitacheza mechi ya kirafiki na Taifa
Stars kinaundwa na; makipa Aishi Manula (Azam), Hussein Shariff (Mtibwa
Sugar) na Ivo Mapunda (Gor Mahia, Kenya).
Mabeki
ni David Luhende (Yanga), Hassan Mwasapili (Mbeya City), Himid Mao
(Azam), Issa Rashid (Simba), Ismail Gambo (Azam), John Kabanda (Mbeya
City), Kessy Khamis (Mtibwa Sugar), Michael Pius (Ruvu Shooting), Miraji
Adam (Simba), Mohamed Hussein (Kagera Sugar), Said Moradi (Azam) na
Waziri Salum (Azam).
Viungo
ni Amri Kiemba (Simba), Farid Mussa (Azam), Haruni Chanongo (Simba),
Hassan Dilunga (Ruvu Shooting), Jonas Mkude (Simba), Khamis Mcha (Azam),
Ramadhan Singano (Simba), Simon Msuva (Yanga), William Lucian (Simba).
Washambuliaji
ni Elias Maguli (Ruvu Shooting), Hussein Javu (Yanga), Joseph Kimwaga
(Azam), Juma Liuzio (Mtibwa Sugar), Mwagane Yeya (Mbeya City) na Paul
Nonga (Mbeya City).
Kim
amesema kikosi cha Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium
Lager chenyewe kitaingia kambini Novemba 12 jijini Dar es Salaam ambapo
siku inayofuata ndipo kitakapocheza mechi na Future Young Taifa Stars.
Baada
ya mechi hiyo, kambi ya Future Young Taifa Stars itavunjwa wakati Taifa
Stars itaondoka Novemba 14 mwaka huu kwenda Arusha ambapo itaweka kambi
na kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa kabla ya kwenda Nairobi,
Kenya kwenye michuano ya Kombe la Chalenji itakayofanyika kuanzia
Novemba 27 hadi Desemba 12 mwaka huu.
Wachezaji
16 wa kikosi cha Taifa Stars kitakachoingia kambini Novemba 12 mwaka
huu kinaundwa na Ally Mustafa (Yanga), Mwadini Ali (Azam), Aggrey Morris
(Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Shomari Kapombe (AC Cannes, Ufaransa)
na Nadir Haroub (Yanga).
Erasto
Nyoni (Azam), Vincent Barnabas (Mtibwa Sugar), Salum Abubakar (Azam),
Mwinyi Kazimoto (Markhiya, Qatar), Frank Domayo (Yanga), Athuman Idd
(Yanga), Mrisho Ngasa (Yanga), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DRC),
Mbwana Samata (TP Mazembe, DRC) na John Bocco (Azam).
Wachezaji
wengine kumi kutoka Future Young Taifa Stars baadaye wataongezwa katika
kikosi kitakachounda timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) kwa
ajili ya michuano ya Kombe la Chalenji.
PAMBANO LA THE TANZANITE LAINGIZA MIL 6/-
Pambano
kati ya timu ya Taifa ya wanawake kwa vijana wenye umri chini ya miaka
20 ya Tanzania (The Tanzanite) dhidi ya Msumbiji lililochezwa juzi
(Oktoba 26 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh.
6,190,000.
Washabiki
waliohudhuria mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza ya Kombe la
Dunia, Kanda ya Afrika iliyomalizika kwa The Tanzanite kuibuka na
ushindi wa mabao 10-0 walikuwa 5,003. Viingilio vilikuwa sh. 1,000, sh.
2,000, sh. 5,000 na sh. 10,000.
Mgawo
wa mapato hayo ulikuwa kama ifuatavyo; Kodi ya Ongezeko la Thamani
(VAT) sh. 944,237.29, gharama za kuchapa tiketi sh. 2,247,900, gharama
za mchezo sh. 599,573 wakati wamiliki wa uwanja walipata sh. 449,679.
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) lilipata sh. 149,893 huku Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) likipata sh. 1,798,718.
Mechi ya marudiano kati ya The Tanzanite na Msumbiji itachezwa kati ya Novemba 8 na 10 mwaka huu.
YANGA, MGAMBO KUUMANA UWANJA WA TAIFA VPL
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inakamilisha raundi
ya kumi na moja kesho (Oktoba 29 mwaka huu) kwa mechi tatu huku Yanga
ikiwa mwenyeji wa Mgambo Shooting kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Uwanja
wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya
Mbeya City na Tanzania Prisons. Rhino Rangers na JKT Ruvu zitacheza
katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Raundi
ya 12 ya ligi hiyo itaanza Oktoba 31 mwaka huu kwa mechi kati ya Simba
na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Novemba
Mosi mwaka huu kutakuwa na mechi kati ya Yanga na JKT Ruvu kwenye uwanja
huo huo.
Novemba
2 mwaka huu kutakuwa na mechi nne; Mgambo Shooting na Coastal Union
(Uwanja wa Mkwakwani, Tanga), Tanzania Prisons na Oljoro JKT (Uwanja wa
Sokoine, Mbeya), Azam na Ruvu Shooting (Azam Complex, Dar es Salaam), na
Mtibwa Sugar na Rhino Rangers (Uwanja wa Manungu, Morogoro).
Raundi
hiyo itakamilika Novemba 3 mwaka huu kwa mechi moja ambapo Mbeya City
itakuwa mwenyeji wa Ashanti United kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya
Sokoine jijini Mbeya.
Mechi
za kukamilisha mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo zitachezwa Novemba 6 na 7
mwaka huu. Novemba 6 ni JKT Ruvu vs Coastal Union, Ashani United vs
Simba, Kagera Sugar vs Mgambo Shooting, Rhino Rangers vs Tanzania
Prisons na Ruvu Shooting vs Mtibwa Sugar.
Novemba 7 mwaka huu, Azam itacheza na Mbeya City wakati Yanga itacheza na Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
EL MAAMRY KUONGOZA BODI YA TFF
Mkutano
Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) umemteua Said Hamad
El Maamry kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ambayo kazi yake kubwa
ni kusimamia mali za shirikisho.
El
Maamry ambaye kitaaluma ni mwanasheria na Mwenyekiti wa zamani wa TFF
wakati huo ikiwa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) ataongoza bodi
hiyo yenye jumla ya wajumbe watano.
Wajumbe
wengine wa bodi hiyo ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera ambaye
anakuwa Makamu Mwenyekiti, Dk. Ramadhan Dau, Mohamed Abdulaziz na
aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Stephen Mashishanga.
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment