Waziri wa Nchi , Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Uwezeshaji Dkt. Mary Nagu (kulia) akimkabidhi nyaraka za utendaji kazi mwenyekiti wa Baraza jipya la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bw. Omari Issa wakati wa uzinduzi wa baraza hilo jijini Dar es salaam.
Waziri wa Nchi , Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Uwezeshaji Dkt. Mary Nagu (katikati) akizungumza jambo na Mwenyekiti wa Baraza jipya la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Bw. Omari Issa (kushoto) na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Dkt. Anacleti Kashuliza jijini Dar es salaam.
Wajumbe na Viongozi wa Baraza jipya la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Nchi , Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Uwezeshaji Dkt. Mary Nagu.(Picha na Aron Msigwa - MAELEZO).
Aron Msigwa –MAELEZO
Dar es salaam.
Serikali imesema kuwa
itaendelea kuunga mkono juhudi za uzalishaji mali zinazofanywa na wananchi
waliojiunga katika vikundi mbalimbali vya
uzalishaji mali katika maeneo mbalimbali nchini.
Kauli hiyo imetolewa
leo jijini Dar es salaam na Waziri wa
Nchi , Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Uwezeshaji Dkt. Mary Nagu wakati akizindua Baraza jipya la Taifa la
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ..
Amesema kuwa serikali
inatambua na inaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na wananchi katika
kujiletea maendeleo kupitia ushiriki walio nao katika vikundi mbalimbali walivyovianzisha
katika maeneo yao na kufafanua kuwa serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea
kuunga mkono juhudi hizo kwa kuanzisha Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi
Kiuchumi.
Dkt. Nagu amesema Baraza
hilo lina jukumu kubwa ya kusimamia na kuratibu utekelezaji wa sera ya Taifa ya
Uwezeshaji wananchi kiuchumi ya mwaka 2004 na kufafanuam kuwa utekelezaji wa mikakati na malengo ya
Dira ya maendeleo ya mwaka 2025 ya
kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati itaweza kufikiwa iwapo
watanzania watashiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Ameongeza kuwa Baraza
hilo lina jukumu la kuwaelimisha
wananchi kuhusu tafsiri ya uwezeshaji Wananchi kiuchumi ambayo kwa muda mrefu imekua
ikipotoshwa na kusisitiza kuwa dhana ya uwezeshaji sio kupitia mitaji pekee
bali ni kujenga uwezo wa wananchi kuweza kuziona fursa zinazowazunguka na
kuweza kuzitumia kwa maendeleo yao.
“ Nchi zinazoweza
kuendelea ni zile ambazo zimejenga uwezo kwenye ushirika, lazima tujenge uwezo
wa vikundi vyetu ili tuweze kugundua wapi tunakwama na kutatua changamoto
zilizopo ili tupige hatua maana uwezeshaji sio kupitia mitaji au kupewa mkopo maana kuna watu tayari wana mitaji lakini
hawawezi kufanya kitu hao tunachokifanya tunawajengea uwezo” Amesisitiza Dkt.
Nagu.
Ameeleza kuwa ipo haja
kwa vikundi mbalimbali vilivyojiunga katika ushirika kuendelea kujenga uwezo
ili viweze kufanya makubwa na kuaminiwa na wadau mbalimbali pamoja na serikali
huku akitoa mfano wa uamuzi wa serikali kununua samani zinazotengenezwa na watanzania.
Dkt. Nagu amesema kuwa serikali
imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya uboreshaji wa miundombinu inayolenga
kuwawezesha wananchi kiuchumi ikiwemo huduma za afya na elimu na kuwataka
wajumbe wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kuweka umuhimu katika maeneo
yatakayoleta matokeo ya haraka na yanayogusa maisha ya wananchi wengi hususan
kwenye kilimo, Ufugaji, Uvuvi, Misitu,Ufugaji Nyuki na Utalii.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Baraza hilo Bw. Omari Issa akizungumza mara baada ya kuzinduliwa
kwa baraza hilo amesema baraza hilo litaendelea kuwajengea uwezo wananchi
kuzitumia fursa zinazowazunguka kujiletea maendeleo.
Amesema baraza
litaendelea kutoa elimu kwa wananchi kwa kuwahamasisha kujenga uwezo katika
vikundi vya ushirika ili waweze kumiliki uchumi wa nchi huku akifafanua kuwa
wananchi walio wengi wanahitaji elimu kuhusu dhana ya uwezeshaji Kiuchumi na
namna ya kutumia fursa na mikopo wanayopata kutoka katika taasisi mbalimbali za
fedha kupata faida .
No comments:
Post a Comment