Na Anna Nkinda –
Maelezo
Dar
es Salaam,
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete kesho anatarajia kuwa mgeni rasmi kwenye
sherehe za mahafali ya kwanza ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama
iliyopo kijiji cha Nyamisati wilayani Rufiji mkoa wa Pwani.
Kwa mujibu wa
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo jijini Dar es Salaam na kusainiwa
na Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) ambayo ndiyo inamiliki
shule hiyo Daudi Nasib inasema jumla ya
wanafunzi wa kike 67 wanatarajia kuhitimu elimu yao ya kidato cha nne Novemba
mwaka huu.
Taarifa hiyo inasema
shule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama ni
matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya Taasisi ya WAMA na wadau mbalimbali wa
maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi wenye
mapenzi ya kusaidia jamii. Bodi ya Wakurugenzi ya WAMA iliamua Shule hiyo iitwe
jina hilo kwa heshima ya Bwana Hayao Nakayama kutoka Japani aliyetoa msaada uliosaidia
ujenzi wa awamu ya kwanza ya shule.
“Moja ya malengo
ya Taasisi ya WAMA ni kusaidia upatikanaji wa Elimu bora ya
Sekondari kwa watoto wa kike na watoto wengine waishio katika mazingira
hatarishi na yatima. Na ni kwa mantiki hii ndiyo maana shule ya WAMA- Nakayama
imejengwa ili kutimiza lengo hili.
Mwenyekiti wa
Taasisi ya WAMA,Mama Salma Kikwete na Bodi ya Wakurugenzi ya WAMA inapenda kutoa shukrani za dhati kwa
wadau wote wanaosaidia Shule ya WAMA- Nakayama na kuunga mkono juhudi za Taasisi
yetu”, ilisema taarifa ya Nasib.
Shule ya Sekondari
ya WAMA- Nakayama ilianza mwaka 2010 ina wanafunzi wa kike 325 kutoka Mikoa yote ya
Tanzania Bara na Visiwani ambao ni yatima na wengine wanatoka familia maskini, watoto
hawa wasingeweza kupata elimu ya
sekondari bila ya msaada wa Taasisi ya WAMA ambayo huwapatia mahitaji yao yote bure
ikiwemo; malazi, chakula, sare za shule, shajara, vitabu na nauli za kwenda
makwao kipindi cha likizo.
Taasisi ya
Wanawake na Maendeleo (WAMA) ni Taasisi isiyo ya kiserikali na isiyo ya kibiashara iliyoanzishwa na Mama
Salma Kikwete, Mke wa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, mwaka 2006 ina malengo
ya kuboresha maisha ya wanawake na wasichana katika masuala ya afya, elimu na uchumi pamoja na
kutengeneza fursa za maendeleo ya wakina mama na watoto.
No comments:
Post a Comment