Sehemu ya waandishi wa habari wakati wa mkutano huo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile (katikati) akitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu matokeo ya utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya Binafsi leo jijini Dar es salaam. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa.
Na. Aron Msigwa –
MAELEZO.
Dar es
salaam.
Uwezo wa Mapato na
Matumizi ya Kaya Binafsi nchini kwa
mwaka 2011/2012 unaonyesha kuongezeka kutokana
na maboresho mbalimbali yaliyofanyika katika sekta ya elimu, afya, umiliki
wa biashara, shughuli za kilimo, umiliki wa Vifaa na Rasilimali , makazi bora,
ongezeko la shughuli za kiuchumi na ajira.
Akitoa taarifa ya Utafiti ulioendeshwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kuangalia
tathmini ya kiwango cha umasikini wa kaya kwa kutumia kipato na masuala mengine
yasiyo ya umasikini wa kipato leo jijini Dar es salaam , Katibu Mkuu wa Wizara
ya Fedha Dkt. Servacius Likwelile amesema kuwa kukua kwa kiwango cha elimu,
matumizi ya nishati ya umeme, hali ya makazi na umiliki wa rasilimali ni
miongoni mwa sababu za kuongezeka kwa uwezo wa mapato na matumizi ya kaya.
Amesema
kuwa utafiti huo ulifanyika kuanzia mwezi Oktoba 2011 hadi Oktoba 2012
ambapo jumla ya kaya 10,186 kati ya 10,400 zilizokuwa zimelengwa
zilihojiwa katika maeneo ya Dar es salaam na maeneo mengine ya mijini na
vijijini kwa Tanzania Bara.
Amesema uchumi wa
Tanzania kwa sasa umekua kutokana na kuimarika kwa sekta za ujenzi,
usafirishaji, Elimu, shughuli za mawasiliano, huduma za afya na huduma za kifedha.
“ Serikali imefanya
mambo makubwa na sasa uchumi wa Tanzania umekua kutokana na juhudi kubwa
zilizofanywa katika kuboresha miundombinu ,kuwekeza katika sekta ya elimu,
usafirishaji, mawasiliano pamoja na ongezeko la huduma za kifedha” amesema.
Amesema kumekuwa na jitihada mbalimbali zilizofanywa
na serikali zikiwemo kuongeza ujenzi wa shule Zaidi hasa zile za sekondari
ambazo zimewezesha kupanda kwa kiwango cha wanafunzi wanaojiunga katika elimu
ya sekondari kutoka 15% mwaka 2007 hadi asilimia 29% 2011/12.
Amefafanua kuwa idadi
ya kaya zinazoishi katika nyumba zilizojengwa kwa vifaa vya ujenzi vya kisasa,
paa za kisasa, vigae na matumizi ya zege na kuta imara tangu mwaka 2007 imeongezeka
kwa 66%.
Ameongeza kuwa matokeo
ya utafiti yanaonyesha kuwa asilimia 4% ya kaya zinamiliki pikipiki, 55%
zinamiliki radio na 57% ya kaya zote angalau mwanakaya mmoja anamiliki simu ya
mkononi na kufafanua kuwa kiasi cha asilimia 78 ya kaya za maeneo ya mengine ya
mjini na asilimi 88 ya kaya za Dar es salaam zinamiliki angalau simu moja ya
mkononi.
Katika hatua nyingine Dkt. Servacius ameeleza wastani wa
kiwango cha umasikini wa chakula kitaifa ni asilimia 9.7 na kuongeza kuwa kiwango hicho kinafikia asilimia 11.3 kwa
maeneo ya vijijini huku Dar es salaam ikiwa na kiwango cha chini kabisa cha
umasikini wa chakula kwa asilimia 1.0 na maeneo mengine ya mjini yakiwa na
umasikini wa chakula kwa asilimia 8.7.
Amesema miji mikubwa
ina kiwango cha chini cha umasikini wa chakula kwa asilimia 1.0 ambapo wananchi
wanaoishi maeneo mengine ya mjini wana umasikini wa chakula wa asilimia 8.7.
Ameongeza kuwa
umasikini wa mahitaji ya msingi kwa Tanzania bara ni asilimia 28.2
ikilinganishwa na asilimia 33.3 kwa maeneo ya vijini na asilimia 21.7 kwa
maeneo mengine ya mjini na kubainisha kuwa Dar es salaam ina kiwango cha chini
cha umasikini wa mahitaji ya msingi cha asilimia 4.1.
Kwa upande wake Afisa
Mwandamizi wa Benki ya Dunia Bw. Richard Martini akitoa salaam za Mkurugenzi
Mkazi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Uganda na Burundi Bw. Phillipe
Dongier, ameipongeza Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa kuzingatia vigezo vya tafiti
vya kimataifa katika kufuatilia hali ya umasikini na kipato nchini.
No comments:
Post a Comment