Mkurugenzi
wa Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Ephraimu Kwesigabo,(kushoto)
akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaa kuhusu
mfumuko wa bei kwa Mwezi Oktoba 2013
Na. Aron Msigwa –
MAELEZO.
Dar es
salaam.
Hali ya kuongezeka kwa
bei ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula katika maeneo mbalimbali
nchini imechangia kwa kiasi kikubwa kuwepo
kwa mfumuko wa bei.
Mkurugenzi wa Takwimu
za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Ephraimu Kwesigabo akizungumza na waandishi
wa habari leo jijini Dar es salaam amesema kuwa mfumuko wa bei wa Taifa kwa
Mwezi Oktoba 2013 umeongezeka hadi kufikia asilimia 6.3 kutoka 6.1 za mwezi
Septemba 2013 kutokana na kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma.
Amesema kuwa hali ya
kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula majumbani na migahawani
umeongezeka hadi kufikia asilimia 7.3 kwa mwezi Oktoba ikilinganishwa na
asilimia 6.9 za mwezi Septemba, 2013.
Kwa upande wa bidhaa
zisizo za vyakula Kwesigabo ameeleza kuwa kumekuwa na ongezeko dogo hadi
asilimia 6.1 kwa mwezi Oktoba 21013 ukilinganisha na asilimia 6.0 za mwezi
Septemba.
Amefafanua kuwa taarifa
za matokeo ya mfumuko wa bei kwa kipimo
cha mwezi zinaonyesha kuwa mwezi Oktoba ulikua asilimia 0.6 ikilinganishwa na
asilimia 0.5 za mwezi Septemba kutokana na kuongezeka kwa bei za bidhaa za
vyakula na bidhaa zisizo za vyakula katika maeneo mbalimbali nchini.
Amezitaja baadhi ya
bidhaa za vyakula zilizochangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa mfumuko wa bei
kwa kipimo cha mwezi kuwa ni pamoja na unga wa mahindi kwa asilimia 1.5, unga
wa Muhogo kwa silimia 3.5, nyama kwa asilimia 1.2, kuku kwa asilimia 3.7,
samaki wabichi kwa asilimia 4.1 na kuku kwa asilimia 3.7.
Bidhaa nyingine ni
pamoja na samaki wakavu kwa asilimia 9.0, dagaa kwa asilimia 2.5, maziwa ya ng’ombe
kwa asilimia 1.2, matunda kwa asilimia 2.9, nazi kwa asilimia 2.6, viazi vitamu
kwa asilimia 4.2 na asali kwa asilimia 5.0.
Ameongeza kuwa mchango
wa bidhaa zisizo za chakula zilizochangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa
mfumuko wa bei kwa kipimo cha mwezi ni pamoja na mavazi ya watoto kwa asilimia
0.4, mafuta ya taa kwa asilimia 2.1 na vifaa mbalimbali vya usafi ambavyo kwa
ujumla wake ni aslimia 0.4.
Hata hivyo kufuatia
hali hiyo ya mfumuko wa bei Bw.
Kwesigabo ameeleza kuwa uwezo wa
shilingi ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma za jamii umeonyesha kuwa
na mwelekeo imara kwa kipindi chote cha mwaka kuanzia mwezi Januari hadi Oktoba
2013.
“Napenda niwahakikishie
kuwa fahirisi za bei za Taifa zimeonyesha kuwa na mwelekeo imara kwa kipindi
chote, kwa hiyo uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na
huduma umeonyesha kuwa na mwelekeo imara” amesema.
Kuhusu ulinganifu mfumuko wa bei wa Tanzania na baadhi ya nchi
za Afrika Mashariki amesema kuwa una mwelekeo unaofanana na kueleza kuwa
mfumuko wa bei nchini Kenya umefikia asilimia 7.76 kwa mwezi Oktoba 2013 huku
nchini Uganda Ukifikia asilimia 8.1 kwa mwezi Oktoba kutoka asilimia 8.0 za
mwezi Septemba.
No comments:
Post a Comment