Na Anna Nkinda – Maelezo, Dubai
Mke wa Rais Mama Salma
Kikwete ametunukiwa tuzo ya kimataifa ya Uongozi wenye Hamasa kwa mwaka 2013 (Global
Inspirational Leadership Award 2013) kutokana na kazi anazozifanya za kuwasaidia wanawake na
watoto wa kike nchini ambazo zimewahamasisha watu mbalimbali Duniani kuweza kuzisaidia
jamii zenye mahitaji.
Hafla ya kukabidhi tuzo hizo ambazo zilitolewa
jana na Kituo cha Maendeleo ya
kiuchumi na Uongozi (CELD) cha nchini Nigeria zilifanyika katika Hoteli ya
Atlantis, The Palm iliyopo Dubai , Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Akiongea mara baada ya kukabidhiwa tuzo
hizo Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo
(WAMA) aliwashukuru waandaaji wa tuzo hizo kwa kuona na kutambua umuhimu wa kazi
anazozifanya na kukipongeza kituo hicho
kwa kazi wanayoifanya ya kuinua uchumi wa wanawake.
Mama Kikwete alisema vifo vingi vya
wanawake vinatokana na uzazi, majeraha
yanayosababishwa na ukeketwaji, ukatili wa kijinsia vinaleta wasiwasi na changamoto za kibinadamu hivyo
basi ni lazima wanawake wafanikiwe kukabiliana na hali hii kwa kuwa wengi
wanakufa kutokana na sababu zinazoweza kuzuilika pia wanakosa nafasi ya kujikwamua
kiuchumi.
“Hatuna muda wa kupoteza lazima
tuchukuwe hatua sasa bila ya kurudi
nyuma kwa sababu zisizoeleweka nia ni kuweka nafasi yetu ya uongozi wa kimataifa ambao utakuwa ni mfano
wa kujivunia kwa wanawake huku tukiona kuzaliwa kwa watoto kuwe ni hali ya kufurahia
na siyo kipindi cha huzuni na kuomboleza”, alisema Mama Kikwete.
Alimalizia
kwa kusema tatizo la vifo vya uzazi litaisha pale ambapo juhudi za makusudi zitafanyika,
kuinua hali ya maisha ya wanawake wa
Afrika na nchi zinazoendelea jambo linalotakiwa ni kutambua kuwa Dunia ina
rasilimali za kutosha, utaalamu na ujuzi wa kuweza kufanya mambo hayo.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa Kituo cha CELD Mama Furo Giami aliwapongeza wanawake hao
viongozi kwa tuzo walizopewa na kusema hivi sasa wanawake wameweza kufanya njia
kwa kuthubutu kupita njia ambayo wanaume walipita hapo zamani na kufanya kazi nzuri zaidi ambayo imewaletea
maendeleo.
Mama
Giami alisema wanawake wengi wenye sauti
ndogo wameweza kuzitumia sauti zao kusikika katika jamii na kukabiliana na changamoto mbalimbali katika
maisha yao. Wameweza kujitegemea na hivyo kupambana na hali ngumu ya uchumi.
Kituo hicho ambacho kilitoa tuzo kwa
wanawake viongozi 15 kutoka nchi za
Afrika, Asia na Mashariki ya kati kinafanya kazi za kuwainua wanawake na watoto
wanaoishi katika mazingira hatarishi na kuhakikisha kuwa wanatimiza malengo yao.
Wengine waliopewa tuzo hiyo ni pamoja na
Mke wa Rais wa Namibia Mama Penehufipo Pohamba, Mke wa Rais wa Burundi Mama Dk.
Mchungaji Denise Nkurunziza na Mke wa waziri Mkuu wa Malaysia Mama Datin Paduka
Seri Rosmah Monsor.
Utoaji wa tuzo hizo ulifanyika mara
baada ya kumalizika kwa mkutano wa siku tatu wa wanawake kutoka nchi za Afrika,
Asia na Mashariki ya Kati ambao ulihudhuriwa na wajumbe kutoka mataifa 28
na kujadili kuhusu Uongozi ni Elimu: Ufunguo wa mustakabali wa wanawake katika
nchi zenye uchumi unaoibuka.
No comments:
Post a Comment