TAMKO LA WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA
JAMII
MHE
DKT. SEIF SELEMAN RASHIDI (MB) KATIKA KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA UKOMA
DUNIANI TAREHE 26/01/2014
Ndugu
Wananchi,
Kwa zaidi ya miaka 50, siku
ya Ukoma Duniani imekuwa ikiadhimishwa ulimwenguni kote kila Jumapili ya mwisho
ya mwezi Januari. Siku hii iliasisiwa na mwandishi wa habari mfaransa Raoul
Follereau aliyetumia muda wake mwingi kuzunguka dunia kueleza hali duni ya maisha
ya watu walioathirika na ugonjwa wa ukoma. Siku hii ilianzishwa ili kuhimiza
jamii kutoa kipaumbele kwa kuwapatia huduma stahiki wagonjwa wa ukoma na watu
wenye machungu ya athari za ukoma.
Ndugu Wananchi,
Lengo kuu la maadhimisho haya ni kukumbusha umma wa watanzania juu ya
ugonjwa huu. Ni dhahiri kuwa ugonjwa wa ukoma umekuwa ukiogopwa sana katika
jamii yetu toka enzi na enzi hasa kutokana na ukweli kwamba unasababisha ulemavu
wa kudumu mwilini na kufanya waathirika kuwa tegemezi na kutothaminiwa.
Ndugu Wananchi,
Tanzania ni miongoni mwa nchi 17 duniani ambazo bado zina viwango vya
juu vya ugonjwa wa ukoma. Mwaka 2013, nchi yetu ilisaini makubaliano katika
mkutano uliofanyika Bangkok Thailand
yalioazimia kuwa na dunia bila ugonjwa wa ukoma. (Bangkok declaration
towards a leprosy - free world). Serikali yenu itaendelea kuwa mstari wa mbele
katika kubaini na kuendeleza jitihada sahihi za kutokomeza ukoma nchini.
Ndugu Wananchi,
Siku hii inatupa fursa ya kutathmini mwelekeo wa jitihada zetu nchini mwetu
na zile za kimataifa katika kupambana na ugonjwa huu. Kauli mbiu katika
maadhimisho ya mwaka huu ni “KABILI
CHANGAMOTO ZA KUTOKOMEZA UKOMA. ONGEZA UBUNIFU.” (OVERCOMING THE REMAINING
CHALLENGES. BE INNOVATIVE.” Kauli mbiu hii, inatutaka kubuni mikakati
endelevu ili tuweze kutoa utatuzi wa changamoto zilizobaki katika kuutokomeza
ugonjwa wa ukoma nchini Tanzania.
Miongoni mwa changamoto zinazotukabili ni uwezo wa watumishi wa afya
kutambua kwa urahisi ugonjwa wa ukoma, jamii kuendelea kushikilia imani potofu
juu ya ukoma na wagonjwa kuchelewa kujitokeza kupata matibabu hadi wanapopata
ulemavu.
Ndugu Wananchi,
Dalili ya awali kabisa ya ukoma ni baka au mabaka kwenye ngozi yasiyo
na uwezo wa kuhisi. Kwa kawaida hayawashi wala hayaumi. Mabaka haya hukosa
hisia ya joto, mguso au maumivu.
Dalili nyingine za ukoma ni pamoja na vijinundu vyenye rangi ile ile ya ngozi sehemu yo yote
ya mwili. Naomba kutoa rai tuonapo mojawapo ya dalili hizi unashauriwa kwenda
kwenye Kituo cha Afya kilicho karibu na wewe kwa uchunguzi na matibabu. Ni
jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa anawahi kwenda kwenye Kituo cha Afya
kwa uchunguzi pindi anapoona kuwa ana mabaka ya aina yoyote katika ngozi ya
mwili wake. Hii itawawezesha wataalam wa afya kuchunguza na kubainisha kama
mgonjwa ana Ukoma katika hatua za awali ili apate tiba sahihi mapema na kupona
na hata kuepusha ulemavu usio wa lazima.
Ugonjwa wa ukoma hutibiwa na dawa mseto (Multi drug therapy au MDT).
Tiba ya ukoma inachukua kati ya miezi sita hadi mwaka mmoja kulingana na aina
ya ukoma. Mgonjwa ambaye ameanza tiba, siyo rahisi kuambukiza mtu mwingine na
hivyo hakuna sababu ya kumtenga na anaweza kuendelea na shughuli za kawaida za
maisha. Tiba ya Ukoma inapatikana nchini kote na hutolewa bila malipo kwa
wagonjwa wote.
Ndugu Wananchi,
Kwa sasa takwimu zetu zinaonyesha ya kuwa nchini Tanzania, kwa miaka
mitano iliyopita, idadi ya wagonjwa wapya wa ukoma inazidi kupungua kutoka
3,248 mnamo mwaka 2008 hadi 2,548 kwa mwaka 2012. Kampeni kabambe
zinazoendeshwa katika maeneo ambayo ugonjwa wa ukoma bado ni tatizo kubwa na haujatokomezwa,
zimeweza kupelekea wagonjwa kuzidi kupungua mwaka hadi mwaka. Kushuka huku kwa
takwimu za ugonjwa wa ukoma kumetokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali na Wahisani
kwa kushirikiana na jamii kuhamasisha ugunduzi wa mapema wa wagonjwa wa ukoma.
Kwa mwaka 2012, kampeni mahsusi zilifanyika katika wilaya za Liwale, Nanyumbu
na Nkasi na kugundua wagonjwa Nanyumbu (74), Nkasi (100) na Liwale (91). Wote
hawa wanaendelea kupata matibabu.
Kwa ujumla bado kuna wilaya 15 ambazo hazijafikia kiwango cha
kutokomeza ukoma cha chini ya mgonjwa 1 kati ya watu 10,000 katika jamii
husika. Wilaya hizi ni Liwale, Nachingwea, Mkinga, Pangani, Muheza, Rwangwa,
Mvomero, Kilwa, Masasi DC, Chato, Nanyumbu, Lindi DC, Kisarawe, Newala na
Songea DC.
Napenda kutoa rai kwa Halmashauri ambazo bado zina wagonjwa wengi, kutenga
fedha kwa ajili ya kuhamasisha wananchi
kutambua dalili za awali za ukoma ili kuwahi matibabu na kuzuia maambukizi
mapya. Kumbuka ukoma ni ugonjwa wa kuambukiza unaoletwa na vimelea hai na
unaosambazwa kwa njia ya hewa kutoka kwa mgonjwa kwenda kwa mtu ambaye hana
vimelea hivyo. Hivyo basi, ni muhimu kumuhimiza mwenzio aliyeathirika kwenda
kupata tiba, ili kukata mnyororo wa maambukizi.
Ndugu Wananchi,
Athari
kuu ya ugonjwa wa ukoma ni ulemavu wa kudumu. Ulemavu unatokana na kuchelewa
kwa uchunguzi na matibabu sahihi. Hapa Tanzania asilimia kumi na moja (11%)
ya wagonjwa wapya wa ukoma wanaojitokeza katika vituo vyetu kwa ajili ya uchunguzi
na kuanza matibabu wanakuwa tayari wana ulemavu wa kudumu. Aidha, mgonjwa
yeyote wa ukoma akigundulika tayari ameshapata ulemavu, ni dalili mbaya. Hii
ina maana kuwa mgonjwa amechelewa kugundulika mapema na akapata ulemavu. Vile
vile, ameendelea kusambaza vimelea vya ukoma katika jamii na kuaambukiza
wengine.
Wito wangu kwenu leo hii, ni sote tujenge tabia ya kuchunguza miili
yetu na pale tunapoona mabadiliko yoyote yanajitokeza twende mapema katika
vituo vyetu vya huduma kuchunguzwa ili tupate ushauri na matibabu stahili.
Ndugu Wananchi,
Tatizo jingine ni unyanyapaa kwa wale waliougua na walioathirika na ukoma.
Sababu kuu ni imani, mila potofu na ukosefu wa uelewa kuhusu ugonjwa huu.
Ukweli ni kwamba ukoma ni ugonjwa unaoambukizwa kwa njia ya hewa na chanzo cha
maambukizi ni mgonjwa wa ukoma ambaye hajagunduliwa wala kuanza matibabu. Mgonjwa
akianza na kuzingatia matibabu hawezi kuambukiza tena na wale wote wanaouguza
athari za ukoma baada ya kukamilisha matibabu ni walemavu wa viungo na siyo
wagonjwa.
Ndugu Wananchi,
Ningependa kuchukua fursa hii kuwahakikishia ya kwamba, Serikali
kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii itaendelea kushirikiana na Wahisani
pamoja na Halmashauri zote kuhakikisha
kuwa:
1. Dawa
za kutosha zinapatikana na kusambazwa nchi nzima katika Zahanati, Vituo vya Afya
na Hospitali zote.
2. Huduma
kwa wagonjwa wa ukoma zinapanuliwa kwa kushirikisha sekta binafsi na kutolewa
bila usumbufu wowote kwa wagonjwa.
3. Tiba
sahihi kwa wale waliopata ulemavu utokanao na ukoma inatolewa ipasavyo.
Ndugu Wananchi,
Tunapofanya
maadhimisho haya napenda kuchukua nafasi hii kwa niaba ya Serikali ya Tanzania
kuyashukuru Mashirika mbalimbali ya ndani na nje kwa michango yao katika kuimarisha
mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukoma hapa Tanzania. Aidha,
inatubidi
kukabili changamoto zilizopo na kuongeza ubunifu katika harakati zetu za
kutokomeza ukoma. Asanteni sana kwa kunisikiliza.
No comments:
Post a Comment