Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF imekutana
Machi 30 mwaka huu kujadili utekelezaji wa maagizo ya TFF kwa wanachama wake
kurekebisha Katiba zao ili ziendane na Katiba ya TFF pamoja na ile ya FIFA
kabla ya Machi 30 mwaka huu.
Vyama vya mikoa Lindi na Dar es Salaam na Chama cha
Mpira wa Miguu cha Wanawake (TWFA) viliomba kuongezewa muda wakati vingine
vimeomba Katiba mama kama angalizo lao la mabadiliko hayo. Klabu ya Simba Sports ndiye mwanachama pekee
aliyewasilisha mabadiliko ya Katiba. TFF
inawapongeza viongozi na wanachama wa klabu hiyo kwa kufanya mkutano wao kwa
utulivu.
Kamati itatangaza nyongeza ya muda wa kufanya mabadiliko
hayo baada ya kuviandalia vyama vya mikoa na vyama shiriki katiba mfano kwa
ajili ya kurahisisha shughuli hiyo.
Baada ya kupitia uamuzi wa wanachama wa Simba S.C. Kamati ya Sheria na Hadhi za
Wachezaji imeamua ifuatavyo:
(i)
Kwa kuwa
pendekezo la wanachama wa Simba kubadili kipengele na 26 kuhusu sifa za mgombea
kinapingana na kipengele na 29 (4) cha
Katiba ya TFF, hivyo basi Kamati imeagiza kipengele cha Katiba ya Simba kibaki
vilevile bila kubadilishwa.
(ii)
Vipengele
vingine vyote vimepitishwa na vitapelekwa kwa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo kwa ajili ya kusajiliwa.
(iii) Mchakato wa uchaguzi wa Klabu ya Simba uendelee kama ulivyopangwa
wakizingatia uamuzi huu wa Kamati. TFF
inaitakia Klabu ya Simba uchaguzi mwema.
Pia Kamati ya
Sheria na Hadhi za Wachezaji imeshauri TFF kuwasiliana na FIFA kupata mwongozo
kuhusu katazo la watu wenye rekodi ya kifungo kugombea.
TFF imepokea
ushauri huo na itaufanyia kazi na kama kuna mabadiliko yoyote kiutaratibu
yataanzia katika Katiba ya TFF kupitia Mkutano Mkuu.
RAMBIRAMBI MSIBA WA DK HEMED MZIRAY
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea
kwa masikitiko kifo cha daktari wa tiba ya michezo, Dk. Hemed Mziray
kilichotokea juzi jijini Dar es Salaam.
Dk.
Mziray ambaye alikuwa mfanyakazi wa Hospitali ya Manispaa ya Temeke na mjumbe
wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Tiba ya Michezo Tanzania (TASMA) amesafirishwa
kwenda kwao mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya mazishi.
Msiba
huo ni mkubwa katika fani ya mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti Dk.
Mziray ameshirikiana na TFF na wadau wengine wa mpira wa miguu katika masuala
ya tiba na uongozi.
Alikuwa
kiungo kati ya Uwanja wa Taifa ambapo mechi za kimataifa, za ligi na za
kirafiki zimekuwa zikichezwa na Hospitali ya Temeke kwa wagonjwa wanaohitaji
huduma zaidi, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.
TFF
tunatoa pole kwa familia ya marehemu Dk. Mziray, TASMA na wafanyakazi wa
Hospitali ya Temeke na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki
kigumu cha msiba huo mzito. Pia TFF inatoa ubani wa sh. 200,000 kwa familia ya
marehemu kama rambirambi zake.
Bwana
alitoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. Amina
MECHI YA AZAM,
SIMBA YAINGIZA MIL 26/-
Mechi
ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Azam na Simba iliyochezwa jana (Machi 30
mwaka huu) Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam imeingiza sh. 26,455,000.
Watazamaji
4,741 walikata tiketi kushuhudia pambano hilo ambapo Azam iliibuka na ushindi
wa mabao 2-1. Viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 15,000 na sh. 20,000.
Mgawanyo
kwa mapato ulikuwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 4,035,508.47, gharama
za kuchapa tiketi sh. 3,908,686 wakati kila klabu ilipata sh. 5,460,687.63.
Uwanja
sh. 2,776,620.83, gharama za mechi sh. 1,665,972.50, Bodi ya Ligi sh.
1,665,972.50, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 832,986.25 na
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 647,878.19.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment