Na Anna Nkinda –
Maelezo, Lindi
Watu wenye
ulemavu wa viungo wametakiwa kutosikitika
kwanini Mwenyezi Mungu aliwaumba hivyo na kujiona wanyonge bali wajione wako sawa na watu wengine kwani katika maisha ya binadamu kila jambo lina
makusudi yake.
Hayo yamesemwa leo na
Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wazee wenye mahitaji maalum
wanaoishi katika kituo cha Rasbura kilichopo wilaya ya Lindi mjini.
Mama Kikwete ambaye pia
ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alifika kituoni hapo
kwa ajili ya kuwajulia hali wazee hao na kuwapatia zawadi mbalimbali za mchele,
nyama, sukari, unga wa ugali, vitunguu, mafuta ya kupikia, nyanya na soda kwa
ajili ya sikukuu ya Pasaka.
Alisema inawezekana
Mwenyezi Mungu aliwaumba hivyo walivyo ikiwa ni kwa makusudi ili iwe njia rahisi
ya kumfikia yeye na kuwataka kushukuru kwa yote. Jambo la muhimu aliwaomba waendelee kuishi kwa amani na upendo kama ndugu.
“Nilipanga siku ya leo kusherehekea sikukuu ya Pasaka
pamoja nanyi huwa nafanya hivi katika sikukuu mbalimbali kama X-Mass na Mwaka mpya, nasherehekea
na watoto yatima na watu wazima wa dini mbalimbali nawaomba adhimisheni siku
hii katika mazingira ya upendo, amani na utulivu”, alisema Mwenyekiti huyo wa WAMA.
Akielezea Historia ya
kituo hicho kinachomilikiwa na kanisa Katoliki Jimbo la Lindi Mkurugenzi wa KARTAS Mzee Saimoni Mnimbo alisema miaka ya nyuma kituo
hicho kilikuwa ni Gereza la wafungwa lakini mara baada ya
kujengwa kwa gereza jipya ndipo Serikali ililipatia jengo hilo Idara ya Ustawi
wa jamii na ikaanza kulitumia kama kituo cha wazee wasiojiweza.
Mzee Mnimbo alimshukuru
Mama Kikwete kwa moyo wake wa huruma na kuamua kwenda kuwatembelea na kuwapatia
zawadi mbalimbali vikiwemo vyakula na
vinywaji na kuwaomba viongozi wengine kuiga mfano ingawa kanisa linawahudumia
wazee hao bali nao wanatakiwa kuwasaidia.
“Tunawashukuru wadau
mbalimbali wanaotuunga mkono na kuwahudumia wazee hawa. Hapa kwetu hakuna tatizo la maji, kuna kipindi
mji mzima wa Lindi haukuwa na maji lakini katika kituo hiki tulikuwa na
maji ya kutosha tunaishukuru ofisi ya
Mkuu wa mkoa kwa kutulipia bili ya maji kila
mwezi”, alisema Mzee Mnimbo.
Kwa upande wake Mwenyekiti
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Lindi Mzee Ally Mtopa alisema katika kituo
hicho hakuna mambo ya udini kwani
binadamu wote ni sawa na kwa yeyote anayejijuwa kuwa yeye ni binadamu basi
akili yake ikitazame kituo hicho na kuweza kukisaidia .
Naye Mzee Mohamed Chitawala
ambaye anaishi katika kituo hicho alisema
wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za afya kwani wakienda Hospitali
kupata matibabu wanapata usumbufu na katika kituo hicho hakuna dawa za huduma ya kwanza.
Tangu mwaka 1995 kituo
hicho kinamilikiwa na kanisa Katoliki jimbo la Lindi, wazee wanaoishi hapo wana ulemavu wa macho na viungo kutoka dini zote ambao wametelekezwa na jamaa zao. Idadi yao ni
10 kati yao wanawake ni sita na wanaume ni wanne kutoka maeneo mbalimbali ya
mkoa huu.
No comments:
Post a Comment