Na Anna Nkinda –
Maelezo
Wanawake wajasiriamali nchini wametakiwa kutengeneza
bidhaa ambazo zinahitajika kwa wingi na watumiaji na kuacha kung’ang’ania kutengeneza bidhaa ambazo soko lake ni dogo.
Mwito huo umetolewa leo na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na
Maendeleo (WAMA) Mama Salma Kikwete wakati wa uzinduzi wa umoja wa vikundi vya kuweka
na kukopa Mbagala (UWAMBA) vilivyo chini
ya WAMA uliofanyika katika Ukumbi wa Dar Live jijini Dar es Salaam.
Mama Kikwete ambaye pia
ni Mke wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete alisema
changamoto kubwa inayowakabili wajasiriamali wengi ni upatikanaji wa soko la
bidhaa zao lakini kama wataamua kubadilika na kutengeneza bidhaa ambazo zinahitajika
kutapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo hilo.
“Ni jambo jema
kujifunza kutengeneza bidhaa mbalimbali , lakini kama utaona bidhaa
uliyojifunza haina soko unaweza kutengeneza bidhaa nyingine ambayo watu wengi
wanaihitaji jambo la muhimu ni kuwa makini katika umaliziaji wa kutengeneza
bidhaa nzuri na zinazovutia”, alisema Mama Kikwete.
Akizungumzia kuhusu
umuhimu wa vikundi hivyo kwa jamii Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema vikundi
hivyo vinatoa mafunzo ya kuweka akiba na kukopa kwa namna ambayo inamsaidia
mwanakikundi kujenga tabia ya kujichunga katika matumizi ya pesa na hivyo kuwa
na mawazo ya kuweka akiba mara kwa mara.
Aidha Mama Kikwete pia
aliwataka wanawake hao kujitokeza kwa wingi kugombea na kushiriki katika chaguzi
mbalimbali zinazokuja ili wapate nafasi
ya kutoa maamuzi.
Mwenyekiti wa WAMA alisema
, “Mkipendana, kushirikiana na kusaidiana mtafika mbali, ondoeni tofauti zenu na kila mmoja asimame na kuweza kumtetea mwenzake,
muwe na marafiki wanaopenda maendeleo na kama mwenzako akifanya vizuri usiache kumsifia”.
Akisoma risala ya
UWAMBA Halima Abrahman ambaye ni katibu wa kikundi cha Faraja kilichopo Tandika
alisema umoja huo wenye vikundi 11 huku wanachama wake wengi wakiwa ni wanawake
na wachache ni wanaume ulianzishwa mwaka
2013 wakiwa wanachangia hisa moja kwa shilingi 2000 kwa sasa wana akiba ya
zaidi ya shilingi milioni 15.
“Mbali na hisa mapato
ya kikundi chetu yanapatikana kutokana na wanachama kufanya biashara mbalimbali
zikiwemo za utengenezaji wa sabuni za maji, batiki, mishumaa, vikapu, mifuko ya
karatasi, siagi za karanga, kusuka mikeka, unga wa muhogo na achali”, Halima alisema.
Alizitaja changamoto zinazokikabili
kikundi hicho kuwa ni pamoja na ufinyu
wa bajeti, ukosefu wa ofisi na vifaa vya kuhifadhi taarifa za chama, kushindwa
kushiriki katika mafunzo na ukosefu wa masoko ya bidhaa zao.
Ili kukabiliana na
changomoto zinavyovikabili vikundi hivyo Mama Kikwete aliwakabidhi vyerehani vinne
ambavyo vitatumika kuanzisha mradi wa kushona nguo ambao utawaongezea kipato na
Kompyuta moja kwa ajili ya kuweka kumbukumbu zao.
Vikundi vinavyosimamiwa
na Taasisi ya WAMA vimetokana mradi wa majaribio wa MWANAMKE MWEZESHE ambao
ulianza mwaka 2011 uliolenga kuanzisha
mfumo wa vikundi ambavyo vitaweza kutoa fursa za mikopo, mafunzo na kujenga
uwezo wa wanachama kujiendesha wenyewe na kuanzisha miradi ambayo itawaongezea
kipato.
Mradi huo wa majaribio
ulifanikiwa na kuweza kuwafikia watu zaidi ya 1200 kwa kata zilizopo katika
maeneo ya Majohe, Gongo la Mboto, Mbagala , Manzese, Temeke na Tandika. Ambapo
jumla ya akiba ya zaidi ya milioni 200 zimekusanywa na mikopo ya shilingi
milioni 265 imeweza kufikia vikundi mwaka 2013.
Pia mradi huo umeweza
kuunganisha vikundi na kuvipatia fursa za kiuchumi na kijamii kwa kutoa mafunzo
na semina mbalimbali za wanavikundi ikiwa ni pamoja na mafunzo ya usindikaji,
kuwaunganisha na huduma ya bima ya afya na ushiriki wa maonyesho ya biashara
kwa ajili ya kutangaza bidhaa zao.
No comments:
Post a Comment