Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza rasmi Mart Nooij kutoka Uholanzi kuwa
kocha mkuu mpya wa timu ya Taifa (Taifa Stars).
Rais
wa TFF, Jamal Malinzi amemtambulisha kocha huyo leo (Aprili 26 mwaka huu) kwenye
mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akiwa
amefuatana na Makamu wake Wallace Karia, amesema anafurahi kumtangaza Nooij na
ana matarajio kuwa Tanzania itanufaika na uzoefu wake mkubwa wa ukocha, hasa
katika bara la Afrika.
“Nawaahidi
Watanzania kuwa sitomuingilia kocha katika kazi yake. Kama mimi sitomuingilia
kocha, basi hakuna mtu yeyote atakayemuingilia. Tumemwajiri yeye kwa vile ni
mtaalamu, hivyo hakuna sababu ya kumuingilia,” amesema Rais Malinzi.
Naye
Nooij ambaye amepewa mkataba wa miaka miwili amesema yeye ni mtu wa maneno
mafupi, hawezi kuahidi kitu lakini ana matarajio ya kuifanya Taifa Stars ifanye
vizuri katika mashindano mbalimbali.
Amesema
kabla ya kukubalia kufundisha Taifa Stars alikuwa na klabu ya St. Georges ya
Ethiopia, lakini vilevile amewahi kufundisha mpira wa miguu barani Afrika
katika nchi za Burkina Faso, Mali na Msumbiji.
Wasifu
wa Nooij umeambatanishwa (attached).
NGORONGORO
HEROES, KENYA UWANJANI DAR
Timu
ya vijana ya Tanzania (Ngorongoro Heroes) na Kenya zinapambana kesho (Aprili 27
mwaka huu) katika mechi ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya
miaka 20 itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Matokeo
ya mechi hiyo ya marudiano itakayochezwa kuanzia saa 10 kamili jioni ndiyo
yatakayoamua ni timu ipi kati ya hizo itakayocheza raundi inayofuata katika
michuano hiyo dhidi ya Nigeria.
Ngorongoro
Heroes inayofundishwa na John Simkoko ilitoka suluhu na Kenya katika mechi ya
kwanza iliyochezwa Machakos, Kenya wiki tatu zilizopita, na imekuwa kambini
jijini Dar es Salaam kwa wiki mbili kujiwinda kwa mechi hiyo.
Viingilio
katika mechi hiyo vitakuwa sh. 2,000 na sh. 5,000 ambapo Kenya iliyowasili
nchini jana (Aprili 25 mwaka huu) usiku imefanya mazoezi yake ya mwisho leo
(Aprili 26 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa..
Mechi
hiyo itachezeshwa na waamuzi kutoka Burundi wakiongozwa na Pacifique
Ndabihawenimana wakati Kamishna ni Tarig Atta Salih kutoka Sudan.
BEACH SOCCER YAZINDULIWA RASMI
Michuano ya mpira wa miguu ya ufukweni (Beach
Soccer) inazinduliwa rasmi kesho (Aprili 27 mwaka huu) kwenye ufukwe wa Escape
One uliopo Mikocheni, Dar es Salaam na kushirikisha timu 13.
Uzinduzi huo utaanza saa 2 asubuhi. Michuano hiyo
inayofanyika kwa mara ya kwanza nchini inashirikisha timu 13 kutoka vyuo
mbalimbali vya jijini Dar es Salaam.
Vyuo hivyo ni Chuo Kikuu cha Ardhi (AU), Chuo Kikuu
cha St. Joseph Tanzania (SJUIT), Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam
(TUDARCO), Chuo cha Ustawi wa Jamii (ISW), Chuo cha Uandishi wa Habari Dar es
Salaam (DSJ) na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Vingine ni Chuo cha Utumishi wa Umma Magogoni, Chuo
cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Taasisi ya
Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Chuo cha
Utawala wa Kodi (ITA) na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).
Michuano hiyo itakuwa inachezwa Jumamosi na
Jumapili kwenye fukwe za Escape One na Gorilla Beach iliyopo Kigamboni, Dar es Salaam.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment