KWA MAWASILIANO ZAIDI: E-mail: yusuf.badi2@gmail.com.

NSSF

TANGAZO

Monday, April 28, 2014

Tanzania Homes Expo na EAG Group Kufanya Maonesho Dar es Salaam Agosti 23-24.

 Mkurugenzi wa Tanzania Homes Expo,Zenno Ngowi (kulia) akizungumza na waandishi Dar es Salaam jana kuhusu Uzinduzi wa maonesho ya 4 ya Tanzania Homes Expo na EAG Group Ltd yatakayofanyika Dar es Salaam kuanzia Agosti 23-24 mwaka huu.Kushoto ni Meneja Biashara,Mathew Gugai.

Mkurugenzi wa Tanzania Homes Expo,Zenno Ngowi (katikati) akizungumza na waandishi Dar es Salaam jana kuhusu Uzinduzi wa maonesho ya 4 ya Tanzania Homes Expo na EAG Group Ltd yatakayofanyika Dar es Salaam kuanzia Agosti 23-24 mwaka huu.Kushoto ni Meneja Biashara,Mathew Gugai na Meneja Masoko,Oscar Mpejiwa.


Hotuba Fupi ya Mkurugenzi wa Tanzania Homes Expo Zenno Ngowi wakati wa kuzindua maonyesho ya 4 ya Tanzania Homes Expo.





Ndugu wana habari,

Ndugu wafanyakazi wenzangu wa Tanzania Homes Expo,

Ndugu wafanyakazi wa EAG Group LTD,



Habari za asubuhi,

Heri ya miaka 50 ya kuzaliwa Tanzania !

Awali ya yote napenda kuwashukuru sana kwa zawadi ya muda na kuwepo kwenu hapa, tunatambua ukubwa na umuhimu wa kazi yenu na pia muda mchache mlionao.

Inanipa faraja kukutana nanyi tena hapa kwenye ukumbi wa idara ya habari maelezo, hii ni mara ya nne kukutana nanyi juu ya suala hili la msingi; Uchocheaji kasi ya upatikanaji wa makazi na vifaa vya ujenzi kwa Watanzania. Maonyesho ya Tanzania Homes Expo yamekua na kufikia kiwango cha kuwa maonyesho makubwa zaidi  na yanayokutanisha watoa huduma mbalimbali za nyumba na wanunuzi wengi zaidi nchini Tanzania. Maonyesho ya mwaka 2013, jumla ya watu 20,000 walitembelea maonyesho ya Tanzania Homes Expo na pia Makampuni zaidi ya 90 kutoka Tanzania na nje ya Tanzania yalishiriki. Maonyesho ya mwaka 2013, yalishirikisha washiriki toka Tanzania, pia Kenya, Uturuki na Ujerumani.



Ndugu wanahabari;

Upatikanaji wa makazi ni kati ya mambo muhimu sana katika maisha yetu ya kila siku, hivyo taarifa juu ya sekta hii ni muhimu zaidi ili kusaidia wananchi kupata taarifa sahihi, kupunguza bei na kujua njia mbadala za kujenga au kupata makazi, hivyo basi maonyesho ya Tanzania Homes Expo ni jukwaa muhimu la kuwawezesha Watanzania kupata taarifa za sekta ya nyumba kutoka kwa watoa huduma wengi mahali pamoja.

Utafiti umeonyesha kwamba maonyesho ya nyumba ndio njia bora zaidi ya uuzaji na upatikanaji wa taarifa za nyumba kuliko njia nyingine yeyote. Ni ukweli usiofichika kuwa kabla ya kufanya manunuzi ya nyumba, au kuchukua mkopo au vifaa vya ujenzi kuna maswali mengi mnunuzi anajiuliza; Kwa mafano je hii ndio bei bora zaidi nitakayopata, Je ni vifaa imara,  Je kuna watoa huduma wengine wanaotoa huduma kama hii? Je wapi naweza kupata ushauri juu ya ujenzi?. Haya ni kati ya maswali ambayo mwananchi anapotembelea maonyesho ya Tanzania Homes Expo anapata majibu yake kwa mapana zaidi pia anapata fursa ya kulinganisha bidhaa na watoa huduma wengi zaidi wa sekta ya nyumba.

Ndugu wanahabari,

Kuanzishwa kwa Tanzania Homes Expo kunaenda sambamba na kukua kwa kasi kwa sekta ya makazi na hivyo kupelekea umuhimu wa kuwako maonyesho yanayokutanisha watoa huduma na wateja wa sekta hii. Maonyesho ya mwaka huu yatavutia watoa huduma wa sekta mbalimbali kama; Mabenki, wajenzi na wauzaji wa nyumba, Mashirika ya bima, Makampuni ya vifaa vya ujenzi, Makampuni yanayotoa huduma ya nishati mbadala, mapambo na bidhaa nyingine za ujenzi.

Ndugu wana habari,

Kama wengi wenu mnavyofahamu na kama nilivyosema awali, upatikanaji wa makazi ni moja kati ya changamoto kubwa kwa wakati huu, hili linatokana na uwiano uliopelea wa uwepo wa makazi na mahitaji pia ongezeko la idadi ya watu hususani mijini imechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza kwa changamoto ya makazi. Aidha, gharama za ujenzi na uwezo mdogo wa kifedha pia yamechangia kupunguza kasi ya upatikanaji wa makazi. Tunapenda kuipongeza Serikali kwa sera ambazo zimeanza kuzaa matunda hususani;

·         Sera ya Maendeleo ya Makazi ya mwaka 2000. Sera hii imewezesha upimaji wa viwanja kupitia miradi mbalimbali kufanyika. Vilevile ili kuendana na utekelezaji wa Mkakati wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania (MKURABITA). Tunafurahi kuwa Wizara ya Aridhi wapo hapa kuwaeleza Watanzania mambo mbalimbali yanayohusu sekta hii.

·        Maboresho ya Shirika la Nyumba (NHC) ambalo sasa linatekeleza mkakati wa ujenzi wa nyumba 15,000. Ni Furaha yetu kubwa kwamba NHC wameshiriki maonyesho haya tangu mwanzo  na wana nyumba za kuuza.  Tunapenda kutumia fursa hii kutoa pongezi nyingi na dhati kwa NHC kwanza kwa kuleta mabadiliko makubwa kwenye shirika na kuwezesha Watanzania wengi kumiliki nyumba kuliko awali.

·        Aidha uanzishwaji wa Mortgage Refinance Company ambayo inawezesha upatikanaji wa mikopo ya nyumba kwa wananchi kupitia mabenki. Pia tunafurahi kuwa TMRC kuwa mmoja wa wadau wakubwa sana wa Tanzania Homes Expo tangu yalipoanzishwa.



Ndugu wanahabari,

Kwa mara nyingine tena na kwa kutambua kuwa huu ni muda muafaka tukielekea kwenye bajeti ya mwaka 2014-2015 tunapenda kutoa rai kwa serikali kuondoa tozo ya ongezeko la dhamani VAT kwenye vifaa vya ujenzi. Tunaamini kwa dhati kwa kufanya hivi Tanzania itafaidika na;

·        Kupunguza bei za nyumba kwa wanunuzi.

·        Kupunguza bei ya vifaa vya ujenzi na hivyo kupunguza mzigo mkubwa wa ujenzi wa nyumba kwa Watanzania.

Tumeona mambo mengi ambayo serikali ya Tanzania imekua sikivu na kuyafanyia mabadiliko, tunaamini kuwa hili ni jambo muhimu katika kuboresha upatikanaji wa makazi kwa Watanzania.



Ndugu wanahabari,

Kupitia kwenu tunapenda kutangaza rasmi kuwa Maonyesho ya sekta ya nyumba yaani Tanzania Homes Expo mwaka 2014 yatafanyika tarehe 23-24 Agosti jijini Dar es salaam. Mwaka huu tunatarajia makampuni zaidi ya 100 kushiriki na pia kwa mara ya kwanza wabunifu wa mapambo ya ndani, wabunifu wa michoro ya nje, washauri wa miradi ya nyumba nao wataungana na washiriki wengine kutoka sekta za; mabenki, mifuko ya jamii, wajenzi, makampuni ya vifaa vya ujenzi, watoa huduma za nyumbani, sekta ya afya ya familia, makampuni ya bima, vifaa vya majumbani na watoa huduma nyingine kwenye maonyesho ya Tanzania Homes Expo 2014.

Kwa njia ya pekee tunapenda kushukuru Wizara ya Aridhi na Maendeleo ya Makazi kwa kutuunga mkono na kuyatumia maonyesho ya Tanzania Homes Expo kama jukwaa muhimu la kutoa elimu kwa umma juu ya maendeleo ya makazi na mambo mengine yahusuyo nyumba.

No comments: