Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) imekubali malalamiko ya Stand United dhidi ya JKT Kanembwa kulalamikia
timu hiyo kuchezesha wachezaji waliosajiliwa dirisha dogo kwenye mechi yao ya
kiporo ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
Mechi hiyo ya kundi C namba 22 awali ilichezwa
mjini Shinyanga na kuvurugika, ambapo Bodi ya Ligi Kuu ya TFF iliagiza irudiwe
kwenye uwanja huru, hivyo kuchezwa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
JKT Kanembwa ilishinda mechi hiyo iliyochezwa
Februari 16 mwaka huu bao 1-0, lakini Stand United katika malalamiko yake
ilidai timu hiyo ilichezesha wachezaji wanane waliosajiliwa katika usajili wa
dirisha wakati mechi hiyo ilikuwa ni ya kiporo.
Kamati ya Nidhamu iliyokutana leo (Aprili 5 mwaka
huu) chini ya Mwenyekiti wake Tarimba Abbas imeyakubali malalamiko hayo, hivyo
kuipa Stand United ushindi wa pointi tatu na mabao mawili kwa mujibu wa Kanuni ya
8(22) ya FDL.
Upande wa walalamikiwa (JKT Kanembwa)
uliowakilishwa na Mwenyekiti wake Luteni Menauri ulikiri kupokea maelekezo
kutoka TFF kuwa wachezaji waliosajiliwa katika dirisha dogo wasitumike katika
mechi hiyo kwa vile ilikuwa ni ya kiporo.
Pia aliyekuwa Kamishna wa mechi hiyo Khalid Bitebo aliimbia
Kamati kuwa baada ya kupokea maelekezo ya TFF alizifahamisha timu zote, lakini
JKT Kanembwa iliondoa wachezaji wawili tu huku ikiwachezesha wengine wanane.
Nayo timu ya Gwasa Sports Club ya Dodoma
iliyolalamika mbele ya Kamati hiyo kupingwa kunyang’anywa pointi sita na Kamati
ya Mashindano ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dodoma (DOREFA) kwa kumchezesha
mchezaji asiye halali kwenye Ligi ya Mkoa, malalamiko yake yametupwa.
Kamati imesema Gwasa imeshindwa kuonesha ushahidi
kuwa ilimhamisha mchezaji huyo (Jeremiah Haule Jeremiah) kutoka timu ya AC
Angry ya mjini Dodoma, na leseni iliyowasilishwa kuwa ndiyo aliyokuwa akiitumia
AC Angry haoneshi msimu aliochezea timu hiyo.
Hivyo, Kamati ya Nidhamu imeridhia uamuzi wa Kamati
ya DOREFA juu ya suala hilo ambapo Katibu wa Gwasa, Khalifa Ismail Ibrahim
alikiri kuitwa kwenye kikao kilichofanya uamuzi huo na kuoneshwa vielelezo
vilivyotolewa vya picha na fomu kuwa mchezaji huyo msimu wa 2013/2014 alichezea
timu ya Katesh katika Ligi ya Mkoa wa Manyara.
Vilevile Kamati ya Nidhamu imebaini kuwa malalamiko
ya Gwasa dhidi ya DOREFA hayakustahili kusikilizwa kwa vile kwa mujibu wa
Kanuni, uamuzi uliofanywa dhidi yao haupaswi kukatiwa rufani.
KAMATI YA MAADILI YAWARUDISHA DARASANI AKINA MBAGA
Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) imesikiliza malalamiko dhidi ya waamuzi wa FIFA, Oden Mbaga na
Samwel Mpenzu na kuagiza wakafanye upya mitihani ya utimamu wa mwili (physical
fitness test) katika robo (quarter) inayofuata.
Katibu Mkuu wa TFF alikuwa amewalalamikia waamuzi
hao pamoja na Mkufunzi wa CAF, Riziki Majala na Mkufunzi wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Mchungaji Army Sentimea kwa kuwafanyisha waamuzi hao mtihani huo
kinyume na utaratibu ikiwemo pia kughushi matokeo.
Waamuzi hao wametakiwa kufanya mtihani huo katika
robo inayofuata ambapo wakifaulu waendelee kuchezesha mechi. Waamuzi wa FIFA
hufanya mitihani hiyo mara nne kwa mwaka.
Mbaga alifeli mtihani wa robo ya nne uliofanyika
Desemba mwaka jana wakati Mpenzu hakufanya kabisa kwa vile alikuwa mgonjwa.
Baadaye Majala aliwafanyisha mtihani mwingine waamuzi hao ambao haukutambuliwa
na TFF kwa vile uliandaliwa kinyume cha taratibu, huku Mkufunzi huyo akidai ana
mamlaka ya kuandaa mafunzo hayo.
Kamati hiyo iliyokutana jana (Aprili 4 mwaka huu)
chini ya Mwenyekiti wake William Erio, imesema imebaini hakuna utaratibu
unaoeleweka wa kuendelesha mitihani hiyo, hivyo kuagiza TFF kufanyia kazi suala
hilo ili kubainisha mamlaka na mipaka ya kila mhusika wakiwemo wakufunzi.
Vilevile Kamati ilibaini kuwa Mchungaji Sentimea
hakuhusika kwa lolote katika uendeshaji wa mtihani huo ulioandaliwa na Majala,
hivyo kumuondoa kwenye malalamiko hayo.
Kwa upande wa Ofisa Takwimu wa TFF, Sabri Mtulla ambaye
alilalamikiwa kwa kuidanganya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kuwa
hakukuwa na pingamizi dhidi ya mchezaji Emmanuel Okwi wakati wa kipindi cha
usajili wakati akijua lilikuwepo, Kamati ya Maadili imeagiza suala hilo
liwasilishwe kwao upya pamoja na ushahidi wa kuthibitisha kama kweli
mlalamikiwa alifahamu juu ya suala hilo.
Mtulla alijitetea mbele ya Kamati ya Maadili kuwa
hakuwahi kuona wala kukabidhiwa barua ya Simba iliyokuwa ikipinga usajili wa
Okwi katika klabu ya Yanga.
YANGA YAMLALAMIKIA STRAIKA WA MGAMBO SHOOTING
Klabu ya Yanga imewasilisha malalamiko Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuwa mshambuliaji wa Mgambo Shooting Stars
ambaye alicheza dhidi yao katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), Mohamed
Neto si raia wa Tanzania na hana Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC).
Ingawa malalamiko hayo yamewasilishwa nje ya muda
(time barred), TFF imeyapokea na itayawasilisha kwenye Kamati husika kwa ajili
ya kupitiwa na baadaye kutolewa uamuzi.
Kwa mujibu wa kanuni, malalamiko yote kuhusu mchezo
yanatakiwa kuwasilishwa ndani ya saa 24 baada ya mchezo kumalizika.
No comments:
Post a Comment