Na Anna Nkinda- Maelezo,
Bagamoyo
Wanafunzi wa
shule za Sekondari wilayani Bagamoyo
wametakiwa kusoma kwa bidii na kufanya vizuri kwenye mitihani yao kwa
kufanya hivyo wataweza kufanikiwa katika maisha yao kwani elimu ni mkombozi wa maisha
ya binadamu.
Mwito huo umetolewa
hivi karibuni na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) Mama
Salma Kikwete wakati akiongea kwa
nyakati tofauti na wanafunzi wa shule ya Sekondari ya wasichana ya Mandera na
Mboga zilizopo wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani.
Mama Kikwete ambaye pia
ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete alisema kama wanafunzi hao watasoma na kufanya vizuri katika mitihani yao wataweza
kufanikiwa kimaisha, watapata kazi na kuwasaidia ndugu zao na hivyo kupunguza tatizo
la umaskini ndani ya jamii zao.
“Mjenge tabia ya kusoma
kwa makundi msione fahari kukaa nyumbani hasa mwisho wa wiki tumieni muda wenu
wa ziada kusoma kwa pamoja , mchague viongozi wa makundi na
kila mmoja wenu awe na somo la kuwafundisha wenzake hii itasaidia kila mtu
kufaidika na mwenzake”, alisema Mama Kikwete.
Mwenyekiti huyo wa WAMA
aliwaasa wanafunzi wa kike kutokubali kudanganywa na wanaume na kujiingiza
katika mahusiano ya kimapenzi wangali wanafunzi kwa kufanya hivyo watapata
mimba zisizotarajiwa na ugonjwa wa Ukimwi hivyo kukatisha masomo yao na kutotimiza
ndoto zao .
Alionya, , “Msikubali
kudanyanywa na wanaume na kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi wakati uko
shule hata kama mzazi wako hana hela za kutosha za kukupatia usikimbilie kwa
mwanaume bali unaweza ukatumia kipindi cha likizo kufuga kuku wa asili na
unaporudi shuleni unawaomba walezi wako wanakuangalizia kuku hao wakikua utawauza
na kujipatia pesa”.
Mama Kikwete pia aliwaasa
wanafunzi hao kuvaa mavazi ya heshima na kujiheshimu na kuacha kuiga mambo
ambayo hayawasaidii katika maisha yao ambayo yanaonyeshwa katika Televisheni bali wapambane katika masomo ili waweze
kufanikiwa katika maisha yao na kama wataona wenzako hawahudhurii darasani kwa ajili ya
utoro wawakanye.
Kwa upande wa walimu
aliwata kuwalea wanafunzi hao kama kama watoto wao wa kuwazaa kwani wao ndiyo
wanadhamana kubwa katika malezi ya wanafunzi.
Aidha Mama Kikwete
alitumia muda huo kuwataka wanafunzi hao kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Dengue ambao na hauna
kinga na unaenezwa na mbu aina ya Aedes Egyptiae ambaye hupenda kuuma watu nyakati za mchana.
“Chukueni hatua dhidi
ya ugonjwa huu kwani unaua watu kwa kusafisha mazingira na kuua mazalia yote ya
mbu kwani mbu huyu mazalia yake ni maji masafi meupe yaliyotuama pia huweza
kuwepo hata ndani ya nyumba.
Alizitaja dalili za
ugonjwa huo ni kuumwa kichwa, maumivu ya viungo na uchovu, homa kali, dalili
hujitokeza siku ya tatu hadi ya 14 tangu kuambukizwa na kutokwa damu sehemu
mbalimbali za mwili.
Kwa upande wake Mkuu wa
wilaya ya Bagamoyo Ahmed Kipozi alimshukuru
Mama Kikwete kwa kazi kubwa anayoifanya na moyo alio nao wa kuwalea na kusimamia elimu
ya watoto wa kike jambo ambalo linawapa nguvu watendaji wa Serikali na kuwapa moyo wanafunzi
ambao wapo katika safari ya kujijengea
maisha yao ya baadaye.
Akisoma taarifa ya
Shule ya Sekondari ya wasichana Mandera Mkuu wa Shule Rose Umila alisema shule
hiyo ina wanafunzi 428 wa kidato cha kwanza 144, cha pili 107, cha tatu 84 na
cha nne 93 na walimu 22 kati ya hao walimu wa wasanaa 17, biashara mmoja na
sayansi wanne.
Mwalimu Umila alisema,
“Kwa upande wa taaluma bado tuna changamoto ya wanafunzi kutofanya vizuri sana
ukilinganisha na matokeo ya mwaka juzi ingawa tulijitahidi kupunguza daraja la
sifuri.
Tatizo kubwa lilikuwa
ni upungufu wa walimu pamoja na wanafunzi kutokuwa makini kwenye masomo yao, wanafunzi
kuchelewa kurudi kutoka likizo fupi na
ndefu hata kwa wale wanaofadhiliwa na mashirika kama CAMFED na wale wanaotoka
katika kijiji cha Mandera wanachelewa kurudi bila sababu yoyote”.
Alizitaja changamoto zinazowakabili
kuwa ni pamoja na uhaba wa mabweni,
ukosefu wa bwalo la chakula, walimu ya Fizikia na Hisabati, nyumba za walimu na
shule kutokuwa na usafiri ni tatizo hasa pale wanafunzi wanapoogua ghafla na
hasa usiku kwani huduma inapatikana
Hospitali ya Miono.
Naye Mkuu wa Shule ya
Sekondari Mboga George Elias alisema
Shule hiyo ni shule ya kata ya Msoga inajumla ya wanafunzi 273 kati ya hao
wavulana ni 162 na wasichana 111, walimu 23 na watumishi wasio walimu wanne.
“Tunakabiliwa na tatizo
la kuripoti kwa wanafunzi wanaopangwa
kuanza kidato cha kwanza , uongozi wa
Shule na Kata unashirikiana kwa karibu kudhibiti suala zima la kutoripoti na
utoro wa wanafunzi Shuleni kutokana na
matatizo hayo wapo wazazi waliofikishwa Polisi na Mahakamani”, alisema Mwalimu
Elias.
Alisema kutokana na
idadi ya wanafunzi na mikondo iliyopo ambayo ni sita hakuna upungufu wa vyumba
vya madarasa kwani wanavyumba saba lakini kulingana na mpango wa maendeleo wa shule bado
kuna upungufu wa majengo.
Changamoto zingine ni upungufu wa vitabu, vifaa vya
michezo, walimu wa Sayansi, vifaa vya kufundishia na kujifunzia na vifaa vya
mabara, kutokuwa na nyumba za walimu na kutokuwa na nishati ya umeme.
Mama Kikwete ni Mlezi
wa Shule ya Sekondari ya wasichana Mandera na katika shule ya Sekondari Mboga
anawalea wanafunzi wa kike. Akiwa katika shule hizo aliwapatia zawadi za vyakula
kama mchele, maharage, unga wa ugali, mafuta ya kupikia, sukari, majani ya
chai, vyombo vya kupikia ikiwa ni pamoja
na majiko, masufuria na vyombo vya kulia vyakula ambavyo ni sahani, vijiko,
vikombe, majagi, majaba ya kuhifadhia maji na kandambili.
No comments:
Post a Comment