Mkutano wa Rais wa Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na wenyeviti wa klabu za Ligi Kuu
ya Vodacom (VPL) kupata maoni yao juu ya changamoto zilizojitokeza katika ligi
hiyo umefanyika juzi (Mei 11 mwaka huu).
Klabu za VPL zilizohudhuria mkutano
huo ni Azam, Coastal Union, JKT Ruvu, Mbeya City, Mgambo Shooting, Mtibwa
Sugar, Polisi Morogoro, Ndanda FC, Ruvu Shooting, Stand United na Tanzania
Prisons.
Simba na Yanga hazikuhudhuria
mkutano huo, na wala klabu hizo hazikutoa udhuru wowote wa kutokuwepo.
Maazimio ya mkutano huo ni kuwa kwa
misimu mitatu ijayo kuanzia msimu wa 2014/2015 klabu zimekubaliana ziruhusiwe
kusajili wachezaji watano wa kigeni. Kamati ya Utendaji ya TFF itatoa uamuzi wa
mwisho juu ya suala hilo katika kikao chake kijacho.
Pia klabu hizo zimekubali timu zao
za U20 kuanzia msimu ujao zicheze ligi ya mkondo mmoja. Hata hivyo, utekelezaji
wa hilo utategemea na upatikanaji wa mdhamini wa ligi hiyo ambapo TFF inafanya
jitihada za kumpata mdhamini huyo.
Vilevile Mwenyekiti wa Kamati ya
Mpira wa Miguu wa Wanawake, Lina Kessy amezishauri klabu za VPL kuanzisha timu
za wanawake, ambapo klabu hizo zimesema zitaufanyia kazi ushauri huo.
KIINGILIO MECHI YA TAIFA STARS 5,000/-
Kiingilio cha chini cha mechi ya kwanza ya raundi ya
mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika 2015 nchini Morocco kati ya
Tanzania (Taifa Stars) na Zimbabwe (Mighty Warriors) itakayochezwa Jumapili
(Mei 18 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni sh. 5,000.
Washabiki watakaolipa kiingilio hicho ni kwa wale
watakaokaa kwenye viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani. Kwa upande wa VIP
B na C kiingilio kitakuwa sh. 10,000 wakati kwa VIP A itakuwa ni sh. 20,000.
Tiketi zinatarajiwa kuanza kuuzwa siku moja kabla ya
mechi hiyo katika vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam, na uwanja siku ya
mchezo huo utakaoanza saa 10 kamili jioni.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium
Lager ikiwa chini ya Kocha Mart Nooij inatarajia kurejea jijini Dar es Slaam
kesho (Mei 14 mwaka huu) kutoka Mbeya kuendelea na maandalizi ya kuikabili
Zimbabwe.
RAMBIRAMBI MSIBA WA MKUFUNZI KASINDE
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea
kwa masikitiko kifo cha Mkufunzi wa waamuzi nchini, Omari Kasinde kilichotokea
jana (Mei 12 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
Mbali
ya kuwa Mkufunzi, Kasinde ambaye anazikwa leo (Mei 13 mwaka huu) mchana katika
Makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam pia alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati
iliyopita ya Waamuzi ya TFF iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Kapteni mstaafu
Stanley Lugenge.
Msiba
huo ni mkubwa katika fani ya mpira wa miguu nchini kwani, Kasinde enzi za uhai
wake alitoa mchango mkubwa katika mchezo huu tangu akiwa mwamuzi na baadaye
mkufunzi na kiongozi..
TFF
tunatoa pole kwa familia ya marehemu Kasinde, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa
Dar es Salaam (DRFA), na Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT) na
kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo
mzito.
Bwana
alitoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. Amina.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment