Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Injinia Mbogo Mfutakamba (katikati) wakati wa akizindua chapisho la Kanuni na utaratibu wa kuzingatia kwa Mamlaka zinazohusika na usimamizi na usambazaji wa maji nchini wakati wa mkutano wa mwaka wa wataalaam na watendaji wa usimamizi wa sekta ya maji nchini.
.Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Injinia Mbogo Mfutakamba (katikati) wakati wa akitoa ufafanuazi kuhusu chapisho la Kanuni na utaratibu wa kuzingatia kwa Mamlaka zinazohusika na usimamizi na usambazaji wa maji nchini alilolizindua wakati wa mkutano wa mwaka wa wataalaam na watendaji wa usimamizi wa sekta ya maji nchini jijini Dar es salaam.
Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Injinia Mbogo Mfutakamba (katikati) akiwaonesha wataalam na watendaji wa usimamizi wa sekta ya maji nchini chapisho la Kanuni na utaratibu wa kuzingatia kwa Mamlaka zinazohusika na usimamizi na usambazaji wa maji nchini wakati wa mkutano wao wa mwaka jijini Dar es salaam.
Mkuu wa Uwezeshaji wa Maendeleo ya Miradi ya Maji kutoka shirika la GIZ nchini Dkt. Fred Lerise akitoa ufafanuzi kwa wataalam wa maji kuhusu chapisho la Kanuni na utaratibu wa kuzingatia kwa Mamlaka zinazohusika na usimamizi na usambazaji wa maji nchini wakati wa mkutano huo wa mafunzo wa mwaka uliowahusisha wataalam na watendaji wa mamlaka za maji kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Mtendaji JPIwa Shirikisho la Wasambazaji wa Maji nchini (ATAWAS) Bi. Martha Kabuzya akizungumzia umuhimu wa chapisho hilo kwa sekta ya maji nchini na kutoa wito kwa mamlaka zote nchini kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuhakikisha kuwa wateja wanaowahudumia wanapata huduma bora.
Sehemu ya Wataalam nawatendaji wa Mamlaka zinazohusika na usimamizi na usambazaji wa maji nchini waliohudhuria mkutano wa mwaka wa wataalaam na watendaji wa usimamizi wa sekta ya maji nchini.
Meneja wa Mamlaka ya Maji wilaya ya Mkuranga Injinia Filbert Pius (kushoto) akipokea chapisho la Kanuni na utaratibu wa kuzingatia kwa Mamlaka zinazohusika na usimamizi na usambazaji wa maji nchini kutoka kwa Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Injinia Mbogo Mfutakamba wakati wa mkutano wa mafunzo wa mwaka uliowahusisha wataalam na watendaji wa mamlaka za maji kutoka maeneo mbalimbali nchini. (Picha na Aron Msigwa - MAELEZO).
Na. Aron Msigwa- MAELEZO.
Dar es salaam.
Serikali imesema itaendelea na zoezi la kujenga miundominu mipya ya maji na kukarabati ile iliyopo ili kuhakikisha kuwa huduma ya maji safi na salama katika maeneo mbalimbali nchini inawafikia wananchi wengi zaidi.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es salaam na Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Injinia Mbogo Mfutakamba wakati wa akizindua chapisho la Kanuni na utaratibu wa kuzingatia kwa Mamlaka zinazohusika na usimamizi na usambazaji wa maji nchini wakati wa mkutano wa mwaka wa wataalaam na watendaji wa usimamizi wa sekta ya maji nchini.
Amesema serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata maji safi na salama kwa kujenga miundombinu mipya na ya kisasa ya kusambazia maji na kukarabati iliyopo kwenye maeneo yote yenye uhitaji mkubwa wa maji ikiwemo jiji la Dar es salaam ambalo linaongoza kwa kuwa na watu wengi.
Akizungumza kuhusu kanuni zilizozinduliwa Injinia Mfutakamba amesema kuwa zitatoa mwongozo wa matumizi bora ya maji nchini na kuongeza ufanisi na uwajibikaji kwa watendaji wa mamlaka za maji kufanya kazi kwa bidii na kuepuka mazoea.
“Suala la utekelezaji wa kanuni hizi sio la hiari kuanzia sasa utekelezaji wa kanuni hizi unaanza na kuondoa tabia ya kufanya kazi kwa mazoea iliyokuwa imejengeka, kila mmoja sasa atimize wajibu wake katika eneo analolisimamia” amesisitiza.
Amewataka watendaji hao kutumia muda mwingi kwenye maeneo yenye miradi ya maji na kufanya kazi kwa weledi na kwa wakati ili kuwafanya wananchi kufurahia huduma zinazotolewa na mamlaka zilizoko kwenye maeneo yao.
Kwa upande wake Mkuu wa Uwezeshaji wa Maendeleo ya Miradi ya Maji kutoka shirika la GIZ nchini Dkt. Fred Lerise awali akizungumza kuhusu mkutano huo wa mafunzo wa mwaka uliowahusisha wataalam na watendaji wa mamlaka za maji kutoka maeneo mbalimbali nchini amesema kuwa unalenga kuimarisha utoaji wa huduma bora za maji.
Amesema wao kama wadau wa sekta ya maji nchini wameendesha mafunzo hayo katika mikoa ya Dodoma, Mbeya, Mwanza na Dar es salaam na kueleza kuwa mafunzo hayo licha ya kuendeshwa katika mikoa hiyo mine yamejumuisha wataalam kutoka mamlaka zote nchini.
Naye Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Wasambazaji wa Maji nchini (ATAWAS) Bi. Martha Kabuzya ameeleza kuwa wao kama wadau muhimu wa sekta ya maji nchini kwa kushirikiana na mamlaka zote nchini wanafanya kazi kwa kushirikiana ili kuhakikisha kuwa wateja wanaowahudumia wanapata huduma bora.
Amesema ATAWAS kama shirikisho linalojumuisha wasambazaji wa maji nchini limekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa wananchi wanapata taarifa sahihi za matumizi ya maji ikiwemo kuweka msisitizo kwa mamlaka za maji kutoa matangazo ya taarifa kwa wateja wanaowahudumia pindi inapotokea hitilafu katika mitambo ya maji ambayo husababisha katizo la huduma ya maji.
Bi. Martha amefafanua kuwa ili kuhakikisha kuwa mamlaka za maji nchini zinafanya kazi kwa viwango na kukidhi mahitaji ya wateja tayari wameandaa Mkataba wa huduma kwa Mteja ambao amesema umeshaanza kutumika ili kuwezesha wateja kupata huduma bora.
Meneja wa Mamlaka ya Maji Kisarawe Bw. Listen Materu ambaye alikuwa miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo ya siku nne akizungumzia kuhusu kuzinduliwa kwa kanuni za usimamizi wa sekta ya maji kwa mamlaka zote nchini amesema hatua hiyo itaongeza ufanisi wa utendaji kazi na kuongeza uwajibikaji.
Amesema ili kuhakikisha ustawi wa mamlaka za maji nchini lazima hatua zichukuliwe ikiwemo suala la uboreshaji wa miundombinu ili kuondoa hasara ya upotevu wa maji.
“Kama hatutatunza miundombinu ya maji na kusababisha maji kupotea mamlaka zitakuwa zinafanya kazi ya hasara na hazitadumu” amesisitiza.
Aidha amesema kuwa mkakati uliopo sasa kwa mamlaka zote ni kuhakikisaha wateja wanapatiwa wanapatiwa maji katika maeneo yao ya makazi.
No comments:
Post a Comment