Na Anna Nkinda –
Maelezo, Lindi
Wazazi na
walezi wilayani Lindi mjini wametakiwa
kuwekeza katika elimu ya watoto wao kwa
kuhakikisha wanakwenda shule kwa wakati kwani elimu ni ukombozi wa maisha na kuolewa katika
umri mdogo kwa watoto hao hakutawasaidia kimaisha.
Mwito huo umetolewa
jana na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa (NEC)
wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete wakati akiongea kwa nyakati tofauti na viongozi wa Halmashauri kuu ya tawi ya
Chama hicho katika matawi yaliyopo kweye kata za Chikonji, Tandangongoro na Ng’apa
wilaya ya Lindi mjini.
Mama Kikwete ambaye pia
ni Mke wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete alisema
ni jukumu la mzazi na mlezi kusimamia elimu ya mtoto wake pamoja na
kumpa malezi mazuri kwa kufuata malezi
ya zamani yanayoendana na mila na utamaduni wa mtanzania kwani hivi sasa kutokana na utandawazi
mienendo ya vijana wengi siyo mizuri.
MNEC huyo pia aliwataka
watoto waliofika kumsalimia mara baada ya kumaliza mkutano wake wa ndani na
viongozi hao wa CCM kusoma kwa bidii na kuacha tabia ya utoro kwani elimu
pekee ndiyo itakayowakwamua na hali
ngumu ya maisha.
Aidha Mama Kikwete aliwahamasisha viongozi wa Halmashauri kuu ya
tawi ya CCM kujiunga katika vikundi mbalimbali vya maendeleo na kuandika maandiko ya kibiashara ili wapate
mkopo kutoka Serikalini na kuweza
kufanya miradi kama ufugaji wa kuku, mamalishe, ufundi seremala, kwa kujishughulisha
na biashara hizo watakuwa wamejikwamua kiuchumi.
“Mkijiunga katika
vikundi vya ujasiriamali mtaweza kukopa fedha kutoka Serikalini jambo la muhimu
mkumbuke kuwa fedha hizi hampewi
bure mnatakiwa kuzirudisha ili na
wenzenu waweze kukopa”, alisema Mama Kikwete.
Kwa upande wa Afya
aliwahimiza kina mama kujitokeza kwa
wingi kupima afya zao ikiwemo saratani
ya matiti na shingo ya kizazi ambayo inatibika ikiwa itagundulika mapema mgonjwa atapata matibabu
na kupona.
“Hivi sasa kuna maradhi
mengi ikiwemo saratani ya matiti na
shingo ya kizazi msiogope kwenda kupima na kujua afya zenu. Nanyi kinababa wahimize wake zenu wakapime ugonjwa huu, mkiona dalili wawapeleke Hospitali mapema kwani ugonjwa huu unatibika kama mgonjwa
atawahi mapema kupata matibabu”,
alisisitiza.
Alimalizia kwa kuwataka
viongozi hao kuonyesha mfano kwa wananchi kwa kujenga nyumba bora za matofali
ya kuchoma na kuezeka kwa bati na siyo za miti kwani moja ya sera ya CCM ni kuwahamasisha wananchi kutunza mazingira na kutokukata miti hovyo.
Akiwa katika Kata ya
Chikonji MNEC huyo alikagua mradi wa maji wa Kwamtokama na kujionea maendeleo
ya mradi huo ambao ukikamilika
utawanufaisha wananchi wapatao elfu saba
kutoka vijiji vya Jangwani, Nanyanje , Chikonji
Kusini na Kaskazini.
Mama Kikwete ambaye ni
mjumbe wa NEC Taifa kupitia wilaya ya Lindi mjini alikutana na viongozi hao wa
Halmashauri kuu ya matawi ya CCM katika
matawi ya Chikonji Kusini na Kaskazini,Nandambi, Kilolombwani na Cheleweni kwa
ajili ya kuimarisha kazi za chama hicho ikiwa ni pamoja na kufanya vikao vya
ndani na viongozi na kuangalia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010.
No comments:
Post a Comment