KWA MAWASILIANO ZAIDI: E-mail: yusuf.badi2@gmail.com.

NSSF

TANGAZO

Friday, June 20, 2014

TFF, PLAN INTERNATIONAL KUHAMASISHA HAKI ZA MTOTO.

Wakati mamilioni ya Watanzania wakifuatilia Fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil, Shirika la kutetea haki za watoto la Plan International limeingia ubia na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa ajili ya kutetea na kuhamasisha juu ya ulinzi wa haki za mtoto hapa nchini.

Kwa lengo hilo, mkataba wa ushirikiano umesainiwa leo katika ofisi za makao makuu ya TFF jijini Dar es Salaam baina ya Mkurugenzi wa Plan International Tanzania, Jorgen Haldorsen na Rais wa TFF, Jamal Malinzi. Ushirikiano huo unalenga kufanya kazi pamoja katika kushughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia, ndoa na mimba za utotoni.

Kwa mujibu wa Haldorsen, mchezo wa mpira ndio unaoongoza nchini na kote duniani kwa kuwa na ushabiki mkubwa na kwamba joto kali juu ya Fainali za Kombe la Dunia linaloendelea Brazil ni ushahidi tosha.

“Tunatambua uwezo wa mchezo huu wa kuwajumuisha watu. Sasa tunataka tuwajumuishe watu sio tu kwa ajili ya furaha lakini pia kama njia ya kuleta mabadiliko juu ya usawa wa kijinsia kwa kutetea na kuhamasisha juu ya haki za mtoto wa kike,” aliongeza.

Mkurugenzi huyo alidokeza kuwa ushirikiano na TFF ni sehemu ya kampeni ya kimataifa inayoendeshwa na shirika hilo kote ulimwenguni inayoitwa ‘Because I Am A Girl’-BIAAG au kwa Kiswahili- KWA SABABU MIMI NI MSICHANA ambayo inalenga kuwatoa mamilioni ya wasichana kutoka katika umaskini kupitia uhamasishaji juu ya haki zao, elimu na stadi za maisha.

“Kwa kupitia ubia huu tutakuwa na uwezo wa kuwafikia mamilioni ya Watanzania na tutawapa wasichana ujumbe kuwa KWA SABABU MIMI NI MSICHANA, lazima nipate fursa sawa na wavulana. KWA SABABU MIMI NI MSICHANA, lazima niwe na uwezo wa kufunga magoli ya kufikia ndoto zangu katika maisha,” Haldorsen alieleza.

Kwa upande wake, Rais wa TFF, ambaye ni mjumbe katika Kamati ya Huduma kwa Jamii ya Shirikisho   la Mpira wa Miguu Ulimwenguni- FIFA, alisema kuwa ubia huo ni sehemu ya utekelezaji wa sera za huduma kwa jamii ya TFF na kwamba wana furaha kushirikiana na Plan International kwa lengo hili muhimu.

“Ushirikiano huu ni muhimu sana kwetu kwani unakileta chombo kikubwa kabisa cha michezo hapa nchini pamoja na shirika la Plan International hususan kwa ajili ya haki za mtoto wa kike. Tunategemea kutumia mtandao wetu nchi nzima kuelimisha juu ya usawa wa kijinsia na uhamasishaji wa haki za mtoto wa kike,” alisema Rais Malinzi.

Kwa pamoja tutashughulikia masuala ya usawa wa kijinsia, hususan kupambana na ndoa za utotoni ambazo zinawazuia mamilioni ya watoto wa kike nchini wasiweze kumaliza shule, kufikia ndoto zao katika maisha, na vile vile kuwaacha waendelee kuteseka katika umaskini,” Rais Malinzi aliongeza.

KUHUSU PLAN INTERNATIONAL: Plan International ni shirika la kimaendeleo la misaada ya kibinadamu, linalomlenga mtoto lisilofungamana na mrengo wowote wa kidini, kisiasa au kiserikali.
Plan International ilianzishwa zaidi ya miaka 70 iliyopita na inaendesha shughuli zake katika nchi 70 duniani. Plan International imekuwa inafanyakazi hapa Tanzania tangu mwaka 1991 ikiwasaidia watoto na jamii kupata huduma za afya, elimu, maji, usafi na mazingira, kujikimu na ulinzi. Inaendesha miradi Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Geita, Pwani, Mwanza na Rukwa.
KAMPENI YA KWA SABABU MIMI NI MSICHANA –BIAAG: Kampeni ya Kwa Sababu Mimi ni Msichana-BIAAG (2012-2016) ni kampeni ya Plan ulimwenguni kote inayolenga kuelimisha na kutetea haki za mtoto wa kike na kuwatoa mamilioni ya wasichana kutoka kwenye lindi la umaskini kupitia elimu na utoaji wa stadi za maisha na kazi.
Kampeni hii inalenga kupambana na ubaguzi wa kijinsia na kuboresha maisha ya wasichana milioni 4 duniani na zaidi ya laki 3 hapa Tanzania kwa kuwawezesha kujiunga shuleni, kupata stadi za kiufundi na maisha, kujikimu, na kushiriki katika shughuli mbalimbali katika jamii na kulindwa, kwa kukabiliana na vikwazo dhidi ya maendeleo ya mtoto wa kike.
KOZI YA UKOCHA LESENI B YAFIKIA TAMATI
Kozi ya makocha wa mpira wa miguu ya Leseni B inayotambuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) iliyodumu kwa wiki mbili inafungwa kesho (Juni 20 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.

Makocha 26 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wameshiriki katika kozi hiyo chini ya wakufunzi wa CAF, Sunday Kayuni, Salum Madadi wa Tanzania na Honory Janza kutoka Zambia. Ufungaji wa kozi hiyo unatarajiwa kufanywa saa 5 asubuhi kwenye hosteli za TFF zilizopo Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.

Walioshiriki kozi hiyo ni Abdalla Mohammed Juma (Zanzibar), Abdul Banyai (Temeke), Abdul Nyumba (Temeke), Abdulmutik Haji (Zanzibar), Aley Mohammed (Zanzibar), Ali Vuai Shein (Zanzibar), Dennis Kitambi (Morogoro), Dismas Haonga (Ilala), Emmanuel Massawe (Shinyanga), Fikiri Elias (Arusha), Fulgence Novatus (Mwanza), Hababuu Ali Omar (Zanzibar), Juma Mgunda (Tanga) na Kidao Wilfred (Ilala).

Wengine ni Maka Mwalwisi (Mbeya), Malale Hamsini Keya (Zanzibar), Mecky Maxime (Morogoro), Mohammed Tajdin (Temeke), Mussa Furutuni (Dodoma), Nassor Salum Mohamed (Zanzibar), Peter Mhina (Ruvuma), Said Mohamed Abdulla (Zanzibar), Salim Makame (Zanzibar), Salum Ali Haji (Zanzibar), Sebastian Nkoma (Ilala), Wane Mkisi (Dar es Salaam).

26 WAITWA STARS SAFARI YA GABORONE
Wachezaji 26 wa Taifa Stars wanaingia kambini Jumatatu (Juni 23 mwaka huu) kwa ajili ya safari ya Gaborone, Botswana.

Kwa mujibu wa Kocha Msaidizi wa timu hiyo Salum Mayanga, wachezaji hao wanatakiwa kuripoti katika hoteli ya Accomondia jijini Dar es Salaam kujiandaa kwa safari hiyo inayotarajiwa kuwa Juni 24 mwaka huu.

Wachezaji hao ni wanaotakiwa kuripoti kambini ni Deogratias Munishi, Aishi Manula, Benedictor Tinoko, Kelvin Yondani, Said Moradi, Nadir Haroub, Joram Nason, Shomari Kapombe, Oscar Joshua, Edward Charles, Aggrey Morris na Pato Ngonyani.

Wengine ni Frank Domayo, Amri Kiemba, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Said Juma, Haruna Chanongo, Himid Mao, John Bocco, Simon Msuva, Kelvin Friday, Ramadhan Singano, Khamis Mcha, Mrisho Ngasa na Mwegane Yeya.

BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments: