Na Anna Nkinda-Maelezo,
Washington
Wanawake wa kitanzania waishio
Ughaibuni wamewatakiwa kuondoa tofauti zao za mitizamo, maoni, dini na makabila
bali wapendane, kuaminiana na kushirikiana ili kwa pamoja waweze kukabiliana na
changamoto mbalimbali zinazowakabili na
hivyo kujiletea maendeleo.
Rai hiyo imetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati
akiongea na wanawake wafanya biashara na wajasiriamali kutoka majimbo ya Washington DC, Wilaya ya
Colombia, Maryland na Virginia katika ukumbi wa mikutano wa ubalozi wa Tanzania
uliopo mjini humo.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema mwanamke wa kiafrika anazo
changamoto nyingi za kihistoria na kimfumo ambazo humkwaza katika juhudi zake
za kujiendeleza na kuendeleza wanawake wengine hivyo inapotokea wanawake wenzie
wanamuandama na kumpiga vita jambo hilo humvunja nguvu na kumkatisha tamaa.
“Katika mazingira ya
sasa ndani ya jamii nyingi tatizo hili
lipo, wanawake wanaendelea kupigana vita, kushambuliana kwa maneno na kashfa
mbalimbali matokeo yake ni kupungua kwa fursa ya kukutana na kutokuaminiana. Acheni
kufanya hivyo kwani kila mmoja wenu
anamuhitaji mwenzie na nchi yenu inawahitaji nyote ili muweze kuwasaidia
wenzenu mliowaacha nyumbani.
Kwa mfano matumizi mabaya ya mitandao ya
kijamii ambayo mara nyingi yameharibika ushirikiano baina ya wanawake wa
Tanzania hususani vijana na wanawake wa umri wa kati inafikia hatua mtu anapohudhuria sherehe au mijumuiko hajui ni picha
na ujumbe gani utakaosambazwa kumhusu yeye”, alisema Mama Kikwete.
Kwa upande wa malezi ya
watoto aliwataka kuwalea katika maadili mema yanayoendana na utamaduni wa mtanzania
kwani hivi sasa kutokana na utandawazi baadhi ya wanawake wamesahau jukumu ya
kuwalea watoto wao na kuwaachia wadada wa kazi kitendo ambacho kinasababisha watoto kuwa na mienendo mibaya.
Mama Kikwete alisema, “Hivi
sasa jamii imekuwa na tabia ya kulalamika kuwa tabia za watoto si nzuri lakini ukiangalia chanzo ni wazazi wenyewe
hasa kina mama ambao wamesahau wajibu
wao wa malezi na kuwaachia wadada wa kazi. Wewe kama mzazi unatakiwa kuwa mfano
wa kuigwa ili mtoto wako akue katika malezi na maadili yanayofaa”.
Mama Kikwete pia aliwataka
wanawake hao kushiriki katika chaguzi mbalimbali ili waweze kufika katika ngazi
ya maamuzi pia wakipata fursa wahakikishe wanakuwa mfano mwema kwa wanawake wengine na kuwa kichocheo cha
kuhamasisha wenzao kwa kuonesha kwamba mwanamke anaweza na anapopata nafasi ya uongozi jamii hunufaika.
Aidha Mwenyekiti huyo
wa WAMA aliwashukuru wanawake hao kwa
tuzo waliyompatia na kusema kwamba tuzo hiyo ni ya wanawake wote wa Tanzania
ambao kwa ushirikiano wao wameweza kupata mafanikio kadhaa katika jamii yao.
Alimalizia kwa kuwaomba waweze kushirikiana na kufanya
kazi pamoja na Taasisi ya WAMA ya kuwasaidia wanawake na watoto wa Tanzania kwa
manufaa ya nchi yao.
Akisoma hotuba ya
ukaribisho kwa niaba ya Balozi Liberata Mulamula Mkuu wa Utawala wa Ubalozi wa
Tanzania nchini Marekani Lilian Munanka alisema wanawake waisho ughaibuni
nchini humo wamekuwa wakifanya shughuli mbalimbali za maendeleo na uchumi sio
tu kwa ajili yao na familia zao bali pia kwa ajili ya jamii nzima.
Alisema wanawake hao
wamekuwa wakihakikisha kuwa nchini Tanzania wanawake wenzao waliokosa fursa ya
kupata huduma za kijamii nao wanazipata zikiwemo huduma za afya na upatikanaji
wa maji safi ya visima.
Kwa upande wa msoma risara ya wanawake hao Harrieth Shangarai alimpongeza
Mama Kikwete kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwasaidia wanawake na watoto wa
Tanzania na kuwataka watu wengine kuiga mfano wake.
Shangarai alisema
katika jumuia yao kuna wanawake wanaofanya kazi ya kuwasaidia wanawake na
watoto walioko Tanzania na kuwaomba wanawake wenzao kutumia muda wao ili waweze
kuelimishana na kuisaidia jamii yenye matatizo hasa kina mama wenye ugonjwa wa
Fistula.
Wanawake hao walimpatia
Mama Kikwete tuzo kutokana na kazi anayoifanya ya kuwasaidia wanawake na watoto wa kitanzania ili waweze kupata
elimu bora na huduma nyingine sahihi za maisha katika jamii na kujenga familia
zenye afya njema na kuleta maendeleo ya
taifa.
No comments:
Post a Comment