Na Anna Nkinda- Maelezo
Mke wa Rais,
Mama Salma Kikwete amewataka Watanzania kujenga tabia ya kufanya maombi ili
waweze kuwa karibu na Mwenyezi Mungu na kupata faraja pale wanapokabiliana na matatizo
mbalimbali wanayokutana nayo katika maisha yao.
Mama Kikwete aliyasema
hayo hivi karibuni wakati wa mazishi ya mtoto wa Naibu Waziri wa Nishati na
Madini, Vedastus Kitwaga yaliyofanyika katika kijiji cha Usagara wilaya ya
Misungwi mkoani Mwanza.
Mama Kikwete ambaye ni
Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema kila nafsi hai ni lazima itaonja
mauti na hakuna mtu anayejua siku yake ya kufa hivyo basi ni lazima watu
wajenge tabia ya kufanya ibada ili waweze kuwa karibu na Mwenyezi Mungu.
“Ukiwa na tabia ya
kufanya maombi ni rahisi kwako kupata faraja hasa pale unapokutana na mambo
mazito katika maisha yako hii ikiwa ni
pamoja na kuondokewa na wapendwa wako kwani maombi ni majibu ya kila jambo”,
alisema Mama Kikwete.
Akihubiri katika Misa
hiyo ya mazishi, Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Yohana Mwinjili Padri John
Somers aliwataka watu waliohudhuria mazishi hayo kuiga mfano wa marehemu ambaye
kwa umri wake mdogo alionyesha upendo kwa jamii iliyomzunguka kwani alikuwa kiongozi wa kanisa hii ikiwa ni pamoja
na mlezi wa Umoja wa Vijana wa Kanisa la Katoliki (VIWAWA) na Katibu wa Jumuia.
“Kabla ya mauti kumkuta
Marehemu alikuwa amelala nyumbani kwao Usagara tarehe 16/8/2014 ndipo akapigiwa
simu na rafiki yake aliyepata ajali eneo la Tanesco Mwanza Mjini , aliamka na
kwenda kutoa msaada akiwa amesimama pembeni mwa barabara akitoa huduma na
wenzake ndipo gari lingine lilikosea njia na kuwagonga na hatimaye kupelekea
kifo chake. Alikuwa tayari pale alipoitwa na kwenda kutoa msaada”, alisema
Padri Somers.
Akiongea kwa Niaba ya
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza Mhashamu Yuda Thadei Padre Robert Kitambo
aliwataka wanasiasa waliohudhuria mazishi hayo kutokumsahau Mwenyezi Mungu
katika maisha yao na kutosahau kuwakimbilia watu wenye shida na kuwasaidia.
Padre Kitambo alisema
kutokana na kazi nyingi za wanasiasa wengi wao wanakosa hata muda wa kuhudhuria
ibada lakinijambo la muhimu ni kumkumbuka Mwenyezi Mungu wakati uko hai.
Nawaomba muwe watetezi
imara wa amani, haki, upendo na mshikamano. Angalieni leo hii tumekusanyika
pamoja kwa upendo katika ibada hii ya kumuaga kijana wetu Vedastus huku kila
mtu akiwa na imani yake lakini
chokochoko za dini na siasa zinatoka wapi?”, aliuliza Padre Kitambo.
Alimalizia kwa kuwataka
watanzania kutumia vyombo vya moto kwa uangalifu na kufauta sheria za usalama
barabani kwa kufanya hivyo ajali zitapungua na watu wengi hawatapoteza maisha
kutokana na ajali hizo.
Marehemu Vedastus Kitwanga
alizaliwa tarehe 25/05/1985 na kupata
elimu yake ya msingi katika shule za Usagara na Muhimbili, elimu ya Sekondari
mwaka 2007 katika shule za Maua Seminari, St. Gaspar Msolwa na Mzumbe, ambapo
mwaka 2010 alihitimu shahada yake ya Bishara na kuajiriwa na Mfuko wa Pensheni wa
PSPF mwaka 2012.
No comments:
Post a Comment