Na Anna Nkinda –
Maelezo, Washington
Rais wa
zamani wa Marekani George W. Bush amempongeza Mke wa Rais Mama Kikwete kutokana
na kazi nzuri anayoifanya ya kuhamasisha jamii na wanawake kwa ujumla
kujitokeza kwa ajili ya kupima saratani ya matiti na mlango wa kizazi.
Pongezi hizo zilitolewa jana na Rais huyo mstaafu ambaye pia ni
mwanzilishi wa Taasisi
ya George W. Bush wakati akifungua mkutano wa wake
wa Marais wa Afrika uliofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo kituo
cha Kennedy (Kennedy Center) kilichopo mjini Washington.
Mzee Bush alisema Taasisi yake inasimamia mradi wa upimaji wa
saratani ya matiti na mlango wa kizazi, ili nchi za Afrika ziweze
kupunguza idadi ya wanawake wanaosumbuliwa na ugonjwa huo na hadi sasa zaidi ya
wanawake 100000 wamefanyiwa uchunguzi katika nchi za Tanzania, Zambia na
Botswana lakini tatizo lililopo ni unyanyapaa kwa wagonjwa
wanaukutwa na tatizo hilo.
Alisema uchunguzi huo umefanyika kwa kipindi cha miaka mitatu
kwani saratani ya mlango wa kizazi ni moja kati ya magonjwa makubwa yanayoua
wanawake wengi katika nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara kwakuwa
wanawake wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) wako katika hatari kubwa zaidi ya
kuugua ugonjwa huo.
Taasisi
ya George W. Bush inafadhili mradi wa Utepe wa
Pinki Utepe Mwekundu (PRRR) ambao ndiyo wasimamizi wa mradi huo uliogharibu
zaidi ya dola za kimarekani milioni
mbili ambao pia utazinduliwa hivi karibuni katika nchi za Namibia na Ethiopia
na zikufanya nchi zinazofadhiliwa kufikia tano.
“Tatizo kubwa ni
Ujinga , upatikanaji wa taarifa zisizo sahihi na unyanyapaa vinazuia maendeleo
ya afya ya jamii na hivyo wanawake kushindwa kwenda kupata chanjo ya
kuzuia ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi (Human Papilloma Virus Vaccine)
lakini watu wengi wanakufa kutokana na unyanyapaa ambao uko juu. Naamini unaweza kuvunjwa mara moja kama
kioo”, alisema Mzee Bush.
Aliwahimiza wake hao wa Marais kuungana kwa pamoja ili kuweza
kuimarisha afya ya mama na wasichana kwani njia moja ya kuwasaidia watoto
ni kuwasaidia mama zao. Na kusisistiza
kwamba ni jambo la muhimu kwa watu wanaoishi na VVU kutokufa kwa magonjwa yanayoweza kutibika na kuzuilika.
Kwa upande wake Mke
wa Rais wa Marekani Mama Michelle Obama alisema wake wa Marais wa Afrika wana
kazi kubwa ya kuzisaidia jamii zao kutokana na matatizo yanayowakabili
kwani wanawake wengi na watoto wanakabiliwa na changamoto mbalimbali hasa
za afya na elimu.
Kwa upande wa
vijana alisema wanafanya kazi sana katika jamii lakini bado wanakabiliwa
na changamoto nyingi zikiwemo za ugonjwa wa Ukimwi. Wao kama viongozi wanatakiwa kuhakikisha kuwa
matatizo yao yanatatuliwa.
“Tunaweza kuwakusanya
watu hawa katika meza moja ili kuweza kutatua changamoto zao, nyie ni
sauti za wanyonge wakiwemo wanawake na watoto jitahidini kuwafikia wanawake
wengi zaidi.
Wakati tunatoa
kipaumbele kwa wasichana wetu tunakazi kubwa ya kufanya naamini majadiliano haya
yatatoa jitihada mpya na nini cha kufanya ili tuweze kuwasaidia vijana wetu, ”
alisema Mama Obama.
Mama Salma Kikwete ni mmoja wa
wake wa Marais wa Afrika waliohudhuria mkutano huo uliandaliwa na Mke wa Rais
wa Marekani Mama Michelle Obama kwa kushirikiana na Taasisi ya George W.
Bush ambao ulijadili uwekezaji katika elimu, upatikanaji wa afya ya
wanawake na wasichana na kuimarisha mahusiano kati ya sekta za umma na binafsi.
No comments:
Post a Comment