KWA MAWASILIANO ZAIDI: E-mail: yusuf.badi2@gmail.com.

NSSF

TANGAZO

Thursday, November 20, 2014

SDL SASA KUANZA KUTIMUA VUMBI DESEMBA 6.

Michuano ya Ligi Daraja la Pili (SDL) msimu huu iliyokuwa ianze kutimua vumbi Novemba 22 mwaka huu kwa mechi kumi katika viwanja vitano tofauti imesogezwa mbele hadi Desemba 6 mwaka huu.

Mechi hizo zimesogezwa ili kutoa fursa ya kukamilisha maandalizi mbalimbali ya ligi hiyo inayoshirikisha timu 24 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.

Mikoa yenye timu katika ligi hiyo ni Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Katavi, Kigoma, Lindi, Mara, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Njombe, Pwani, Rukwa, Ruvuma, Shinyanga, Singida na Tabora.

MASHINDANO YA TAIFA YA U12 YASOGEZWA
Mashindano ya Taifa kwa vijana wenye umri chini ya miaka 12 yanayoshirikisha kombaini za mikoa yote ya Tanzania yatafanyika jijini Mwanza kuanzia Desemba 30 mwaka huu hadi Januari 5 mwakani.

Awali mashindano hayo yalipangwa kuanza Desemba 6 mwaka huu, lakini yamelazimika kuyasogeza ili kutoa fursa ya kukamilika kwa matengenezo ya viwanja vitatu ambayo vitatumika.

Kila timu ya mkoa inatakiwa kuwa na ujumbe wa watu 16, wakiwemo wachezaji 14 na makocha wawili katika mashindano hayo ya timu yenye wachezaji saba (7 aside).

Timu zinatakiwa kuwasili jijini Mwanza kuanzia Desemba 28 mwaka huu tayari kwa ajili ya uhakiki wa umri na taratibu nyingine za mashindano. Timu zote zitafikia katika shule ya Alliance (Alliance Schools).

Wachezaji wanaotakiwa kushiriki mashindano hayo ni wenye umri chini ya miaka 12, hivyo ni wale waliozaliwa kuanzia Januari 2003 na kuendelea.

RAMBIRAMBI MSIBA WA MUNYUKU, KARASHANI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko vifo vya waandishi wa habari Innocent Munyuku na Baraka Karashani vilivyotokea jana (Novemba 19 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.

Msiba huo ni mkubwa katika familia ya mpira wa miguu, na tasnia ya habari nchini kwa ujumla kutokana na mchango mkubwa waliotoa katika ustawi wa mpira wa miguu nchini kupitia kalamu zao.

Munyuku alikuwa mmoja wa waandishi waanzilishi wa gazeti la Mwanaspoti wakati Karashani kwa nyakati tofauti alifanya kazi katika vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo kampuni ya New Habari 2006 akiripoti habari za mpira wa miguu.

Tunatoa pole kwa familia za marehemu, Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), na kampuni ya New Habari 2006 na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Bwana alitoa, Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

No comments: