Na Anna Nkinda – Maelezo,
Lindi
Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia wilaya ya
Lindi mjini Mama Salma Kikwete amewataka wanachama wa chama hicho pamoja na
wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajia
kufanyika mwishoni mwa wiki hii.
Mama Kikwete ambaye ni
Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alitoa rai hiyo jana wakati akiongea na wanachama
pamoja na wagombea wa nafasi za Uenyeviti na Wajumbe wa Serikali za mitaa
katika kata za Ndoro na Mikumbi zilizopo wilaya ya Lindi mjini.
Alisema kuna baadhi ya
watu hawajiandikishi na wengine siku ya uchaguzi ikifika hawaendi kupiga kura, wanabaki
kulalamika viongozi hawafai. Lakini kama wangeshiriki katika uchaguzi kusingekuwa
na malalamiko kwa kuwa wangekuwa wamechagua viongozi wanaowataka.
“Siku ya uchaguzi ikifika amkeni mapema
mkapige kura na msipoteze kura zenu kwa kuchagua watu wengine, chagueni
viongozi wa CCM ambao chama chetu kimefanya
mambo mengi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma za afya, ujenzi wa
shule na kuendelea kuimarisha amani ya nchi yetu”, alisema Mama Kikwete.
Aidha MNEC huyo pia aliwasisitiza
wanachama hao wakati wa kujiandikisha majina katika daftari la kudumu la wapiga
kura kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali Kuu ukifika wawahamasishe wananchi wakajiandikishe ili waweze kuwachagua viongozi
wao.
Akiwa katika mkutano wa kampeni uliofanyika mtaa wa Mto Mkavu Mama Kikwete aliwanadi kwa wananchi wagombea wa chama hicho
wanaowania nafasi za Wenyeviti na Wajumbe wa Serikali za mitaa kutoka Kata ya
Mbanja.
Aliwasihi vijana
kubadilika na kujifunza historia ya nchi yao hapo ndipo watajua wapi nchi imetoka
na wapi inakwenda kwani hivi sasa kuna watu wanapita na kuwadanganya hakuna
maendeleo yoyote yaliyopatikana ukilingamisha na miaka ya nyuma.
Mama Kikwete
alisisitiza, “Lazima mtambue kuwa Serikali ya CCM imeleta maendeleo kwa
wananchi wake kwa kujenga barabara na hivi sasa kutoka Lindi hadi Dar es Salaam kwa gari dogo unatumia
masaa matano na unaweza kwenda na
kurudi, kwa basi siyo zaidi ya masaa saba. Leo watu wanapita na kuwadanganya
hakuna maendeleo yaliyofanyika jambo ambalo siyo kweli”.
Naye Mwenyekiti wa CCM
wilaya ya Lindi Mjini Muksini Rafii alisema kuna propaganda zinazosambazwa na
wapinzani kuwa Serikali imesogeza mbele
siku ya uchaguzi hadi tarehe 17 kitu
ambacho siyo sahihi kwani uchaguzi
utafanyika tarehe 14 mwezi huu kama ilivyopangwa.
Muksini alimalizia kwa kuwaomba
wananchi kuwa makini katika uchaguzi wa viongozi kwani kuna watu wanapita na
kuwadanganya wasiwachague wagombea wenye
dini na makabila tofauti na yao wasiwasikilize,
Tanzania haina dini wala kabila watu wote ni sawa na kuwasisitiza kuwachagua
viongozi wa CCM ambao watawaletea maendeleo.
Katika mkutano huo wa
kampeni wanachama wanne kutoka chama cha
Wananchi (CUF) walimkabidhi Mama Kikwete kadi za chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi.
No comments:
Post a Comment