Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk.Agnes Kijazi
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk.Agnes Kijazi (kulia), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana, kuhusu mwelekeo wa mvua kwa kipindi cha Januari na Februari, 2015 nchini. Kushoto ni Mkurugenzi, Huduma za Utabiri, Dk.Hamza Kabelwa.
Wana habari wakiwa kwenye mkutano huo leo
..........................................................................
Habari/ Picha na Dotto Mwaibale
wa mtandao wa www.habari za jamii.com
SIKU moja baada ya mvua kubwa kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini na kusababisha madhara Watanzania wametakiwa kuchukua tahadhari kutokana na kuendelea kunyesha kwa mvua kubwa za vipindi.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dk. Agness Kijazi Dar es Salaam jana wakati akiwasilisha tathmini ya mvua za vuli kuanzia Ocktoba hadi Disemba mwaka huu na mwelekeo wa mfumo ya hali ya hewa na mvua kwa kipindi cha Januari na Febduari 2015.
Alisema kutokana na mifumo iliyopo ya hali ya hewa inatarajiwa kusababisha vipindi vya ongezeko la mvua katika baadhi ya maeneo ya Magharib kwenye mikoa ya, Nyanda za juu Kusini-Magharibi na mikoa ya Kusini mwa nchi kuanzia Januari na Febduari 2015.
Hata hivyo alisema kuwa katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka hususan Nyanda za Juu Kaskazini-Mashariki, Pwani ya Kaskazini, Kanda ya Ziwa Viktoria na Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma mvua zinatarajia kuisha mwishoni mwa Disemba mwaka huu.
Alisema matukio ya mvua katika maeneo ya mvua za nje ya msimu yanatarajiwa katika kipindi cha miezi ya Januari 2015.Hali hiyo inatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya Kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, Kusini mwa Mkoa wa Pwani na baadhi ya meneo ya Mikoa Arusha , Manyara, Kagera, Geita, Shinyanga na Mwanza.
Dk. Kijazi alisema katika maeneo mengine yaliyosalia yanatarajia kuwa makavu huku maeneo ya Magharibi mwa nchi, Kanda ya Kati, Nyanda za Juu Kusini-Magharibi, Kusini mwa nchi na Pwani ya Kusini ambayo yanayopata msimu mmoja wa mvua yanatarajiwa kupata mvua za juu ya wastani.
"Izingatiwe kuwa pamoja na kuwepo kwa uwezekano wa matukio mengi ya mvua kubwa katika maeneo yatakayopata mvua za juu ya wastani, hali hiyo pia itajitokeza katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani," alisema.
Aliongeza kuwa matukio ya vimbunga katika eneo la kusini magharibi mwa bahari hindi yanatarajiwa kuchangia katika mwenendo wa mvua nchini.
"Maeneo ambayo hali ya mvua inaweza kuathiriwa zaidi na vimbunga ni pamoja na kanda ya kati, nyanda za juu kusini magharibi, magharibi mwa nchi na maeneo ya ukanda wa Pwani," alisema.
No comments:
Post a Comment