Na. Aron Msigwa-MAELEZO.
Dar es salaam.
Mfumuko wa Bei wa Taifa
kwa mwezi Desemba 2014 umepungua hadi kufikia asilimia 4.8 kutoka asilimia 5.8 iliyokuwepo
mwezi Novemba kutokana na kupungua kwa bei ya bidhaa na huduma katika maeneo
mbalimbali nchini.
Akitoa taarifa ya
Mfumuko wa Bei wa Taifa leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Sensa na
Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Bw. Ephraim Kwesigabo amesema kuwa
kupungua kwa bei za bidhaa za vyakula zikiwemo Mahindi, Unga wa mahindi, mbogamboga,
mihogo ,sukari ,Mafuta ya taa, dizeli, petroli na Simu za kiganjani kumechangia
kupunguza mfumuko wa bei nchini
Amesema kuwa wastani wa
Mfumuko wa Bei wa Taifa wa mwaka mzima kutoka Januari hadi Desemba 2014
umepungua hadi kufikia asilimia 6.1 kutoka asilimia 7.9 uliokuwepo kuanzia
Januari hadi Desemba mwaka 2013.
Ameeleza kuwa Tanzania inaendelea kufanya Vizuri katika nchi za
Afrika Mashariki katika kudhibiti Mfumuko wa bei kwa kuendelea kuchukua hatua
za kudhibiti viashiria vinawezakuchangia kuwepo kwa mfumuko wa bei.
Akitoa ufafanuzi kuhusu mfumuko wa bei katika baadhi
ya nchi za Afrika Mashariki Kwesigabo amesema kuwa umekuwa na mwelekeo
unaofanana, Kenya ukipungua na kufikia asilimia 6.02 mwezi Desemba kutoka 6.09
za mwezi Novemba na Uganda ikiwa na mfumuko wa bei wa asilimia 1.8 kutoka
asilimia 2.1 za mwezi Novemba, 2014.
Aidha, amesema mwenendo
wa Fahirisi za bei ambacho ni kipimo kinachotumika kupima mabadiliko ya bei za
bidhaa na huduma zinazotumiwa na kaya nchini katika kipindi cha mwezi Desemba 2014 amesema kuwa Fahirisi hizo zimeonyesha
kuongezeka hadi kufikia150.92 kutoka 150.54 za mwezi Novemba 2014.
Amefafanua kuwa kuongezeka
kwa Fahirisi hizo kunatokana na kuongezeka kwa bei za bidhaa za vyakula na
bidhaa zisizo za vyakula zikiwemo mchele, unga wa mahindi, samaki, matunda
jamii ya machungwa, mbogamboga, mavazi ya wanaume na wanawake na viatu vya
wanaume.
Kwa upande wake Meneja
Utafiti wa Uchumi wa Benki Kuu ya Tanzania Bw. Johnson Nyella ameeleza kuwa
kuendelea kupungua kwa Mfumuko wa Bei nchini kunatokana na hatua mbalimbali
zinazochukuliwa na Serikali kupitia Benki hiyo kwa kuangalia utekelezaji wa
Sera na Mipango ya maendeleo.
Amesema kuwa katika kuhakikisha kuwa Tanzania
inaendelea kuwa na utulivu wa Uchumi kwa kipindi kirefu, Benki Kuu ya Tanzania imekuwa
ikifuatilia mwenendo wa bei katika Soko la Dunia, bidhaa na huduma zinazozalishwa
nchini na ufuatiliaji wa mwenendo wa uchumi wa nchi zinazoizunguka Tanzania.
Amesema malengo ya muda
mrefu ya Benki kuu ya Tanzania ni
kuhakikisha kuwa Mfumuko wa bei unapungua na kufikia asulimia 5.
No comments:
Post a Comment