NA:
VERONICA KAZIMOTO, KAMPALA UGANDA.
WITO umetolewa kwa
washiriki wote wa Mkutano wa Kumi wa Maendeleo ya Takwimu Afrika kuelendelea
kutoa takwimu sahihi na kwa wakati ili kuleta maendeleo yanayokusudiwa ya kiuchumi
na kijamii barani Afrika.
Wito huo umetolewa jana
na Waziri Mkuu wa Uganda Mhe. Dkt. Ruhakana Rugunda wakati akifungua Mkutano wa
Kumi wa Maendeleo ya Takwimu Afrika uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa
Speke Munyoyo Kampala, Uganda.
Dkt. Rugunda amesema
kuwa, ili kupata maendeleo kwa haraka, ni lazima takwimu zitolewe kwa wakati na
ziwe sahihi kwa ajili ya kusaidia kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo.
"Ili Bara la
Afrika liweze kuendelea kwa haraka, linahitaji takwimu sahihi na zinazotolewa
kwa wakati ili takwimu hizo zisaidie katika kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo",
amesema Waziri Mkuu Rugunda.
Dkt. Rugunda ameongeza
kuwa ili kuweza kufanikisha hilo, kuna umuhimu kwa nchi za Afrika kusaidia
program mbalimbali za uzalishaji wa takwimu na matumizi yake kwa ajili ya
kupanga mipango ya maendeleo.
Kwa upande wa Waziri wa
Fedha wa Uganda Matia Kasaija amesema kuwa, ili kuweza kulinganisha takwimu za
nchi mbalimbali, ni vyema takwimu zinazozalishwa zikafuata mbinu bora za
uzalishaji wa takwimu.
Matia Kasaija amesema
mbinu bora za uzalishaji wa takwimu ni zile zinazofuata viwango vinavyopendekezwa na Umoja
wa Kimataifa - Kitengo cha Takwimu.
Mkutano wa Kumi wa Maendeleo
ya Takwimu Afrika umewakutanisha washiriki takribani 400 kutoka nchi mbalimbali
za Afrika ikiwemo Tanzania. Mkutano huu ni wa siku tatu na unatarajia
kumalizika kesho tarehe 15 Januari, 2015.
No comments:
Post a Comment