KWA MAWASILIANO ZAIDI: E-mail: yusuf.badi2@gmail.com.

NSSF

TANGAZO

Monday, February 9, 2015

MFUMUKO WA BEI NCHINI WAPUNGUA.

Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Ephraimu Kwesigabo akitoa taarifa ya kupungua kwa mfumuko wa bei nchini kwa mwezi Januari, 2015 jijini Dar es salaam. 

Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
Dar es salaam.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu imesema kuwa Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Januari, 2015  umepungua hadi kufikia asilimia 4.0 kutoka asilimia 4.8 ya mwezi Desemba, 2014 kutokana na kuendelea kupungua kwa kasi ya bei ya bidhaa na huduma mbalimbali nchini.

Akitoa taarifa ya mfumuko huo leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Ephraim Kwesigabo amesema kuwa kupungua kwa mfumuko wa Bei katika maeneo mbalimbali nchini kumesababishwa na kupungua kwa kasi ya bei ya bidhaa za vyakula na  zile zisizo.

Amesema kiwango cha badiliko la kasi ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya kimeonyesha kupungua katika maeneo mbalimbali nchini kikihusisha bei ya mahindi, Unga wa mahindi , ndizi, ndizi za kupika na mihogo.

Aidha, Bw. Kwesigabo ameeleza kuwa bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia kupungua kwa mfumuko wa bei nchini ni pamoja na mafuta ya taa asilimia 8.4, dizeli asilimia 10.2, Petroli kwa asilimia 6.8 na  gesi ya kupikia kwa asilimia 2.9.

Akitoa ufafanuzi kuhusu  kiwango cha badiliko la kasi ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi kwa kipimo cha mwezi kati ya mwezi Desemba 2014 na Januari 2015 , amesema kuwa mwezi Januari umekuwa na ongezeko la asilimia 1.0 ikilinganishwa na ongezeko la asilimia 2.0 la mwezi Desemba , 2014.

Kuhusu Fahirisi za bei kwa maana ya kiwango cha badiliko la kasi ya bei  za makundi ya bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na Kaya binafsi kwa kuzingatia kipimo cha mwezi zimeonyesha kuongezeka hadi kufikia 152.43 kwa mwezi Januari 2015 kutoka 150.92 za mwezi Desemba, 2014.
 
Amebainisha kuwa kuongezeka kwa Fahirisi hizo kumechangiwa na bidhaa za mchele, nyama, samaki ,lishe kwa watoto, mbogamboga, mavazi ya wanawake, kodi ya pango na mkaa kwa asilimia 1.6 .

Kwa upande wa uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma za mlaji kwa mwezi Januari , 2015 Kwesigabo amesema kuwa umefikia shilingi 65 na senti 60 ikilinganishwa na kiasi cha shilingi 66 na senti 26 za mwezi Desemba 2014.

“Uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma zilezile kwa mlaji kwa mwezi Januari 2015 na Desemba 2014 umepungua kidogo, hii inamaanisha sasa mtu hahitaji kuongeza ziada ili aweze kununua bidhaa na huduma anazozihitaji”

Kwa upande wa mfumuko wa Bei wa mwezi Novemba 2014 katika nchi za Afrika Mashariki amesema una mwelekeo unaofanana , Kenya ukipungua  na kufikia  asilimia 5.53 kwa mwezi Januari 2015, kutoka asilimia 6.02 za mwezi Desemba 2014, Uganda  mfumuko wa bei kwa mwezi Januari 2015 umepungua hadi asilimia 1.3 kutoka asilimia 1.8 za mwezi Desemba 2014.

No comments: