Timu ya Taifa ya
Tanzania (Taifa Stars) imethibitisha kushiriki michuano ya kombe la COSAFA nchini
Afrika Kusini kufuatia mwaliko wa Baraza la vyama vya soka Kusini mwa Afrika
(COSAFA).
Michuano ya kombe
la COSAFA inatrajiwa kuanza kutimua vumbi katikati ya mwezi Mei mwaka huu
nchini Afrika Kusini, na ratiba ya hatua ya awali ya makundi inatarajiwa
kutangazwa leo jioni saa 1:00 kamili jioni kwa saa za Afrika Mashariki moja kwa
moja na kituo cha Luninga cha Supersport 4.
Taifa Stars itakuwa
juu (seeded) katika hatua ya makundi, ambapo nchi nane zitagawanya katika
makundi mawili na washindi wa kila kundi wataingia hatua ya robo fainali, nchi nyingine zitakazoanzia kwenye makundi ni
Lesotho, Madagascar, Marutius, Namibia, Seychelles, Swaziland.
Katika kila kundi,
timu zote zitacheza michezo mitatu na mshindi wa kila kundi ataingia katika
hatua inayofuata ya robo fainali itakayozijumuisha nchi za Afrika Kusini, Botswana, Ghana, Malawi,
Msumbuji na Zambia ambazo zimeingia katika hatua ya pili kutokana na nafasi zao
kwenye msimamo wa viwango vya FIFA.
Kombe la COSAFA lilianza
mwaka 1997 linajumuishaa nchi 16 wanchama kutoka Kusini mwa Bara la Afrika,
limekua likifanyika kwa kushirikisha nchi wanachama waliopo Kusini mwa bara la
Afrika.
Nchi wanachama wa
COSAFA ni Afrika Kusini, Angola, Botswana, Comoros, Lesotho, Madagascar,
Malawi, Maurtius, Mayotte, Msumbuji,Namibia, Reunion, Sychelles, Swaziland,
Zambia na Zimbabwe.
SALAMU ZA RAMBIRAMBI.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini – TFF amepeleka
salamu za rambirambi kwa familia ya Bw. Nyama, kufuatia kifo cha mwamuzi
mstaafu Mohamed Nyama ambaye pia aliwahi kuwa mjumbe wa kamati ya waamuzi ya TFF kilichotokea jana kwao Nachingwea-
Lindi.
Marehemu Mohamed Nyama wakati wa uhai wake alikuwa mwamuzi
wa daraja la kwanza ambaye pia alitambuliwa na FIFA, Nyama anatarajiwa kuzikwa
leo jioni kwao Nachingwea mkoani Lindi na TFF itawakilishwa na Mjumbe wa Kamati
ya Utendaji Bw. Athumani Kambi.
Katika salam zake kwa familia ya Nyama, kwa niaba ya TFF,
familia ya mpira wa miguu na watanzania Rais Malinzi amewapa pole wapenzi wa
mpira wa miguu nchini katika kipindi
hiki kigumu cha maombelezo.
KILA LA KHERI AZAM, YANGA, KMKM NA
POLISI
Shirikisho la Mpira
wa Miguu nchini Tanzania (TFF), limezitakia kila la kheri na ushindi timu za
Azam na Young Africans katika michezo yao ya marudiano itakayofanyika mwishoni
mwa wiki hii .
Azam FC itakuwa
ugenini siku ya jumamosi mjini Khartoum, Sudan kucheza mchezo wa marudiano na
wenyeji timu ya El Merreikh ambapo katika mchezo wa awali uliofanyika Chamazi
jijini Dar es salaam Azam iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Jijini Gaborone
nchini Botswana katika kombe la Shirikisho, timu ya Young Africans watacheza na
wenyeji timu ya jeshi ya BDF XI siku ya ijumaa katika mchezo wa marudiano pia,
ambapo katika mechi ya awali Young Africans iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Mjini Zanzibar KMKM
wataikaribisha timu ya AL Hilal ya Sudan siku ya jumamosi katika Uwanja wa
Aman, huku kikosi hicho Maalum cha Kuzuia Magendo kikihitaji ushindi wa kuanzia
mabao 3-0 ili kuweza kusonga mbele, kufuatia kupoteza mchezo wa kwanza Khartoum
kwa mabao 2-0.
Timu ya Polisi
Zanzibar itakuwa mwenyeji wa timu ya FC Mounana kutoka nchini Gabon siku ya
jumapili katika mchezo wa kombe la shirikisho barani Afrika,ikihitaji ushindi
wa mabao 5-0 ili kufuzu hatua inayofuata baada ya kupoteza mchezo wa awali kwa
mabao 4-0.
Kwa niaba ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF, famili ya mpira na watanzania wote
wanawatakia kila la kheri na ushindi katika michezo hiyo ya marudiano ambapo
timu hizo zitakua zikipeperusha bendera ya Taifa.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment