Baadhi ya Waandishi wa Habari wakiwa kazini wakati Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii Epraim Kwesigabo wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu akizungumza na waandishi jijini Dar es Salaam kuhusu taarifa ya kuongezeka kwa Mfumuko wa Bei nchini kwa mwezi Februari, 2015.
Na Veronica Kazimoto,
Dar
es Salaam,
Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwezi Februari, 2015
umeongezeka kwa asilimia 4.2 kutoka
asilimia 4.0 mwezi Januari mwaka 2015.
Hayo yamesemwa leo na
Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii Epraim Kwesigabo kutoka Ofisi ya Taifa
ya Takwimu (NBS) ambapo amesema kuwa kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na
huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Februari, 2015 imeongezeka kidogo ikilinganishwa
na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Januari, 2015.
“Kuongezeka kwa Mfumuko
wa Bei wa mwezi Februari, 2015 kumechangiwa na kuongezeka kwa bei za baadhi ya
bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi Februari,
2015 zikilinganishwa na bei za mwezi Februari, 2014, amesema Kwesigabo”.
Bidhaa
za vyakula zilizoonyesha kuongezeka mwezi Februari, 2015 zikilinganishwa na bei
za mwezi Februari, 2014 ni pamoja na bei za mchele (asilimia 18.5), unga wa mihogo
(asilimia 9.3), nyama (asilimia 8.9), samaki (asilimia 12.4) na maharagwe kwa asilimia
7.1.
Kwa
upande wa bidhaa zisizo za vyakula zilizoonyesha kuongezeka mwezi Februari, 2015
zikilinganishwa na bei za mwezi Februari, 2014 ni pamoja na bei za mavazi ya
wanaume (asilimia 4.7), mavazi ya wanawake (asilimia 3.3), mkaa (asilimia 5.1),
mashuka (asilimia 3.1) na gharama za kumuona daktari kwa asilimia 11.2.
Akizungumzia
kuhusu Mfumuko wa Bei kwa kipimo cha mwezi Mkurugenzi Kwesigabo amesema kuwa Mfumuko
wa Bei wa mwezi Februari, 2015 unaopimwa kwa kipimo cha mwezi umeongezeka kwa
asilimia 1.6 ukilinganisha na ongezeko la asilimia 1.0 mwezi Januari, 2015.
Aidha,
Kwesigabo amesisitiza kuwa Fahirisi za Bei zimeongezeka hadi kufikia 154.83
mwezi Februari, 2015 kutoka 152.43 mwezi Januari, 2015 ambapo kuongezeka kwa
fahirisi kumechangiwa na kuongezeka kwa bei za bidhaa za vyakula na bidhaa
zisizo za vyakula.
Kwa
upande wa thamani ya shilingi, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii Epraim
Kwesigabo amesema uwezo wa Shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na
huduma umefikia Shilingi 64 na senti 59 mwezi Februari, 2015 kutoka mwezi
Septemba, 2010 ikilinganishwa na Shilingi 65 na senti 60 ilivyokuwa mwezi Januari,
2015.
Hata hivyo, Mfumuko wa
Bei nchini Tanzania una mwelekeo unaofanana na baadhi ya nchi nyingine za
Afrika Mashariki kwa kuwa Mfumuko wa Bei wa mwezi Februari, 2015 nchini Uganda umeongezeka
hadi asilimia 1.4 kutoka asilimia 1.3 mwezi Januari, 2015; na nchini Kenya,
Mfumuko wa Bei wa Mwezi Februari, 2015 umeongezeka hadi asilimia 5.61 kutoka
asilimia 5.53 mwezi Januari, 2015.


No comments:
Post a Comment