Na Anna Nkinda –
Maelezo
Msichana
mmoja kati ya wanne wenye umri wa miaka 15
hadi 19 ni mjamzito au anamtoto idadi hii inawakilisha maisha yao halisi na
kuonyesha kwamba kama jitihada za makusudi hazitachukuliwa wasichana wataendelea
kukosa haki zao za msingi na kuzidi kuwa
wategemezi.
Hayo yamesema na Mke wa
Rais Mama Salma Kikwete wakati akifungua mkutano wa kimataifa wa utafiti katika ukunga ulioandiwa na LUGINA Afrika
Midwives Research Network (LAMRN)
uliofanyika katika Hoteli ya Kunduchi
jijini Dar es Salaam.
Mama Kikwete ambaye ni
Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema vifo vya kina mama wajawazito na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano ni tatizo
katika nchi zote zilizopo Kusini mwa Bara la Afrika hata hivyo jitihada
mbalimbali zinafanyika ili kuhakikisha
tatizo hilo linapungua au kumalizika kabisa.
“Naamini utafiti
uliofanywa na LAMRN kwa kipindi cha miaka miwili utasaidia kuongeza utendaji
kazi wa wakunga na kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na watoto katika
bara letu la Afrika”, alisema Mama Kikwete.
Kuhusu mimba za utotoni
Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema tafiti zilizofanyika zinaonyesha wasichana wanaanza kufanya mapenzi mapema zaidi wakiwa
na umri mdogo ukilinganisha na wavulana jambo linalopelekea kupata mimba za
utotoni na hivyo kukosa elimu kwa kukatisha masomo yao.
Mama Kikwete alisema, “Takwimu
za Ulimwengu zinaonyesha zaidi ya wasichana milioni 58 wameolewa kabla ya kufikisha
umri wa miaka 18 kati ya hao milioni 15
wanaumri wa miaka 10 hadi 14”.
Nchini Tanzania asilimia
13 ya wasichana wanaanza kufanya mapenzi wakiwa na umri wa miaka 15 na kwa upande wa wavulana kwa umri huo huo ni asilimia saba".
Akiongea kwa niaba ya Waziri wa Afya na
Ustawi wa Jamii Dkt. Seif Rashid, Mkuu wa wilaya ya Kinondoni Paul Makonda alisema kauli mbiu ya mkutano huo ambayo ni utendaji wa kazi kwa kutumia ushahidi wa
utafiti : utaimarisha afya ya mama na
watoto wachanga imekuja wakati muafaka wa kuweka suala la afya ya mama na
mtoto kwanza hii ni moja ya mipango ya shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kwa
mwaka 2010-2015 katika bara la Afrika.
Makonda alisema hatua mbalimbali zimeshachukuliwa
ikiwa ni pamoja na kutoa wataalam kwa nchi wanachama ili waweze kupunguza vifo
vya watoto na kuimarisha afya ya mama mjamzito.
“Ninategemea kwamba kwa kutumia ushahidi uliopatikana katika utafiti kwa
pamoja tutaweza kutimiza malengo yetu kwa kuimarisha afya ya mama na watoto
wachanga katika Bara la Afrika ninaamini mawazo na jitihada zenu zitaendelea ili
kuleta mabadiliko katika sekta ya afya”, alisema Makonda.
Naye Dkt. Rose Laisser ambaye
ni msimamizi wa LAMRN nchini alisema wakunga wanahudumia asilimia 42 ya kina
mama wajawazito wakati wa kujifungua hii
ikiwa ni uwiano wa mkunga mmoja kwa wazazi 40 wakati katika hali halisi mkunga
mmoja anatakiwa kuhudumia wanawake sita.
Dkt. Rose alisema, “Pamoja
na wakunga kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhudumia
wajawazito wengi lakini bado wanafanya kazi
kwa bidii na kujituma ya kuwahudumia
kinamama na watoto wachanga”.
Chuo Kikuu cha Manchester cha nchini Uingereza na Partnerships for
Global Health (THET)
walitoa
fedha kwa nchi sita Barani Afrika kwa kipindi
cha miaka miwili ili wakunga 20 kutoka kila nchi waweze kufanya utafiti na kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu kazi
hiyo.
Jumla ya wakunga
120 kutoka nchi za Tanzania,
Zambia, Malawi, Kenya, Uganda na Zimbabwe walifanya utafiti na kuwasilisha
mambo waliyojifunza na changamoto walizokutana nazo katika mkutano huo .
Mkutano huo wa siku nne
ulihudhuriwa na wadau wa afya wakiwemo wakunga wapatao 220 kutoka Tanzania,
Zambia, Kenya , Uganda, Zimbabwe, Malawi, Uingereza, Sweden, Switzeland na
India na Namibia.
No comments:
Post a Comment